Social Icons

PATA HABARI NA BURUDANI MBALI MBALI POPOTE ULIPO!

JPM; Siasa za kibaguzi hazitaleta maendeleo

HAYATI Nelson Mandela kwa mara ya kwanza wakati anaingia katika siasa na kutambulishwa kwa mwanaharakati wa chama cha ANC, Walter Sisulu, alitamka maneno haya “siasa safi huzaa demokrasia safi, lakini kamwe siasa ya kibaguzi haziwezi kuzaa demokrasia safi na kama demokrasia safi isipopatikana hiyo itakuwa inaanisha kwamba wananchi hawawezi kupata maendeleo”. Mandela alitoa kauli hiyo wakati ambao wananchi weusi wa nchini Afrika Kusini wakibaguliwa na serikali ya kikaburu ya watu weupe. Sababu kubwa ya kukumbuka kauli hii na kuitumia katika makala yangu inachangiwa na hali halisi inayoendelea nchini Tanzania kwa wananchi kukabiliwa na hali ngumu ya maisha huku hali ya uchumi ukiendelea kusogea kwa mwendo wa kinyonga. Sababu ya hayo yote jibu lake nikabaini kosa ni ubaguzi wa siasa unaofanywa na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), John Magufuli kwa uamuzi wake wa kuendesha serikali kwa kufanya ubaguzi wa vyama. Hakuna asiyejua kwamba Magufuli amekuwa akibagua vyama vya upinzani huku akitumia vyombo vya dola kuzuia vyama vya upinzani kufanya shuguli za siasa wakati mwenyewe na chama chake wakitaka kufanya hakuna wa kuwazuia kama ilivyokuwa kwa makaburu walivyokuwa wakifanya Afrika Kusini. Viongozi weusi wa siasa walipokuwa wakitaka kufanya mikutano walikuwa wakikabiliwa na polisi, wanasiasa pekee waliokuwa wakiruhusiwa kufanya mikutano walikuwa ani weupe pekee. Uamuzi huo huwa najiuliza je, wamesahau maneno ya kada wao namba moja, Mwalimu Julius Nyerere aliyefundisha kwamba “Kaburu si lazima awe mweupe bali yule anayefanya matendo ya kikaburu hata kama ni mweusi ni kaburu tu,” Uteulizi wa kujali maslahi ya vyama umeonekana katika uteuzi wa wakurugenzi wapya wa halmashauri za majiji matano, manispaa 21, miji 22 na wilaya 137 (DED) ambao uliibua mijadala kwa wachambuzi na wafuatiliaji wa mwenendo wa Serikali yake. Sababu kubwa ya uteuzi huo ambao haukufanyika kwa bahati mbaya ulikuwa na lengo la kumrahisishia Magufuli na chama chake ushindi katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 kwa kuwa ndio watakaokuwa wasimamizi wa uchaguzi katika halmashauri na manispaa zao. Tatizo linaanzia hapa; nafasi za DED zinahitaji wataaluma zaidi na watu wenye uwezo katika utawala na uendeshaji wa halmashauri hivyo kitendo cha kuteuliwa baadhi ya makada kitasababisha uendeshaji wa miradi ya maendeleo kuwa mgumu na utoaji wa huduma za kijamii kushindikana kutokana na kutokuwa na weledi katika kazi hiyo, na pia watumishi hawa wa umma watageuzwa kuwa watumishi wa chama tawala. Ubaguzi huo umechangia kwa kiasi kikubwa kushindwa kuimarisha mambo mengi kutokana na kuathiriwa na kuyatazama katika jicho la kisiasa la kutazama manufaa zaidi katika chama chake. Sababu hiyo imechangia hata kusita kuiacha huru mihimili ya dola ambayo ni Bunge na Mahakama, kwani pamoja na vyombo hivyo kudaiwa kuwa huru watendaji wake wamekuwa wakitakiwa kuomba ruhusa katika mhimili wa Serikali(Ikulu) wakati ni mhimili uliokamilika. Jambo hilo ni sawa na kuwapatia haki kwa mkono wa kulia huku wakipokonywa kwa mkono wa kushoto. Ubaguzi huo umechangia kwa kiasi kikubwa kushindikana kukamilisha ahadi ya Rais Magufuli ya kuzalisha ajira hasa kwa vijana waliosoma viwango mbalimbali vya elimu na wasio na ujuzi kwa kutumia ajira za viwanda hasa vile vinavyoajiri watu wengi, na sekta ya kilimo na uvuvi na mifugo. Lipo swali la kujiuliza je, hadi sasa ni vijana wangapi wamewezeshwa kujiajiri kama ambavyo iliahidiwa wakati wa uchaguzi kwa kuwawezesha vijana wanaohitimu Elimu ya Juu na vyuo vya ufundi kupata mitaji ya kuwasaidia kuanzisha makampuni yao kulingana na fani walizosomea. Je, ni vijana wangapi wamewezeshwa kuanzisha Saccos zao ili kupata mikopo zaidi ya wengi kuzagaa mitaani baada ya serikali kusimamisha ajira. Ubaguzi huo unaweza ukawa sababu ya wataalamu wa halmashauri kushindwa kubuni njia za serikali kujipatia kipato na kujikuta wakipambana kupata mapato kupitia ushuru wa akina mama lishe, wachuuzi mbalimbali, Machinga, waendesha Boda Boda na Maguta ambao wakati wa uchaguzi tuliahidiwa watu hawa hawatabughudhiwa na mgambo watatafuta kazi ya kufanya lakini hadi leo mgambo wanapiga kazi hiyo. Tatizo la kutazama mambo katika jicho la kisiasa hasa kujitafutia mtaji ndiko kumemuibua Rais Magufuli na kutangaza eti, ameokoa bilioni 6 kutokana na kuzuia posho na fedha nyingine katika shughuli ya kuzima Mwenge mkoani Simiyu. Jambo ambalo wale wenye akili za kushabikia mambo pasipo kupima Kwanini tusiambiwe imetumika shilingi ngapi tangu mwenge uanze safari yake mwezi April pale uwanja wa Jamhuri Morogoro kwa baraka za makamu wa Rais?? Fanya hesabu hii: Chukua gharama za kukimbiza mwenge nchi nzima alafu linganisha na gharama za miradi ya maendeleo iliyo zinduliwa na mwenge! Hapo ukipata jibu liweke pembeni kwanza. Alafu tazama shughuli ya kuzima mwenge mkoani Simiyu imeokoa bilioni 6, je siku ya uzinduzi zilitumika kiasi gani?? Je, kwa majiji makubwa kama Mwanza, Dar es Salaam, Mbeya na Arusha kwa hali yake ya kijographia zilitumika fedha kiasi gani kwenye mafuta ya magari na posho na mavazi??? Leo kijana ambaye hawezi kufikiri kwa kina ana simama na kushangilia na kupongeza kwamba ni uwajibikaji na kubana matumizi! Tangu Mwanzo walikuwa wapi?? Hawakuona gharama hizo??? Hutakiwi kuwa na akili za Profesa (Bwana Yule) ili kujua kwamba hizi ni siasa nyepesi sana!! Kama hasara zina onekana sasa hivi, kwanini mwenge usipigwe marufuku?? MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan leo atawasha Mwenge wa Uhuru na kuzindua rasmi mbio zake ili kukimbizwa katika halmashauri za wilaya na Manispaa zipatazo 179 za mikoa ya Tanzania Bara na Visiwani. Uzinduzi huo utakaofanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro ambao utatanguliwa na shamrashamra za halaiki kutoka kwa vijana zaidi ya 1,000 na vikundi vya utamaduni kutoka wilaya za Morogoro na nje ya mkoa huo. Zaidi ya bolioni 100 Mwisho.

Thursday, January 30, 2014

 Lipumba: Viongozi wabovu ni sababu ya uchumi tegemezi



MWENYEKITI wa Chama Cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba amesema kuwa sababu za kuwa na uchumi tegemezi zinachangiwa na kuongozwa na viongozi wabovu wanaoendesha nchi kwa kutokuwa na dira.
Akizungumza hivi karibuni jijini Dar es Salaam, Profesa Lipumba ambaye ni mtaalamu wa uchumi alisema uongozi bora ni jambo muhimu katika maendeleo ya kiuchumi.
Alisema kama uongozi unakuwa mbovu hauwezi kuwa na dira ya kuweza kujenga uchumi usiokuwa tegemezi ila utakachofanya ni kushiriki katika biashara.
Profesa Lipumba alifafanua kwa kusema “Uchumi tegemezi ni ule ambao serikali haina uwezo wa kuendesha shughuli zake za ndani ila kwa kupata misaada kutoka nje,”.
Akielezea matatizo ya uchumi yanayolikumba taifa kwa sasa alisema ni matatizo yaliyoanza mwanzoni mwa mwaka 1960 katika nchi nyingi za kiafrika kama Tanzani, Ghana, Guinea ambazo zilikuwa na mikakati ya kujaribu kujenga ujamaa.
Anasema kuwa katika ujenzi wa ujamaa Tanzania haikuweza kutoa fursa kwa wajasiliamali wa ndani kuwawezesha kuwa wawekezaji na kuwawezesha kujua mbinu za kibiashara kwa nia ya kuwawezesha kuongeza uzalishaji .
“Kwa mfano hapa Tanzania mkulima aliyekuwa na ekari 10 alihesabika kama Bepari na Kabaila, wakati heka hizo ni kidogo sana. Hali iliyosababisha kuwa na sera za kujenga ujamaa wa vijijini ambapo wakulima wote walitakiwa kuwa na shamba la pamoja la ujamaa ambalo lilitakiwa kuwa na manufaa kwa watu wote,”.
Anaongeza kuwa sera hizo ziliondoa motisha kwa wakulima wadogowadogo kuwekeza katika sekta ya kilimo ikiwamo kuweza kujiendeleza na kuweza kukuza kilimo chao.
Alisema kuwa “Matatizo zaidi yalionekana mwaka 1970, ingawa kulikuwa na matatizo ya uchumi wa dunia na kuanguka kwa bei ya bidhaa zetu ikiwamo kuongezeka kwa bei ya mafuta hali iliyotufanye tujikute tumeingia katika matatizo makubwa ya  ukosefu wa fedha za kigeni,”.
Alisema kuwa baada ya kujikuta katika hali hiyo ilibidi kujikuta nchi ikiangukia katika mikono ya mashirika ya Kimataifa ya Fedha hususani Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Benki ya dunia kwa sababu nchi haikuwa na fedha za kigeni hivyo ikawa inahitaji kupata misaada iweze kujiendesha.
“Tatizo hilo liliendelea kwa muda mrefu na kusababisha kushindwa kujinasua na kujenga uchumi ambao unatoa fursa kwa wananchi wenyewe kuwa wajasiliamali ili waweze kuwekeza na hapo ndipo tukaacha kilimo pembeni na wakulima wadogowadogo bila msaada,” alisema Profesa Lipumba.
Akielezea kuhusu aina za utegemezi Profesa anasema kuwa ni utegemezi wa masoko ambao nchi nyingi za Afrika zimekuwa zikizalisha mali ghafi na kuziuza katika nchi za Magharibi ikiwamo na zile za Asia ya Mashariki.
Utegemezi mwingine ni ule wa Teknolojia ambazo huagizwa kutoka nchi za nje na mwingine ni ule wa mitaji kutoka kwa wawekezaji wa nje hasa katika sekta binafsi unafanyika kwenye maeneo ya madini na viwanda.
Utegemezi mwingine ni misaada ambayo huingia katika bajeti za serikali ambayo karibu theluthi moja inategemea misaada kutoka nje pamoja na kujitawala katika miaka 52, nchi imeshindwa kujinasua katika wimbi la utegemezi kutoka nchi za Magharibi.
Utegemezi mwingine aliouzungumzia ni ule ambao hauepukwi wa kushirikiana katika kujenga uchumi wa kisasa ambao ni kushirikina katika biashara na nchi zilizopiga hatua katika Maendeleo makubwa.
“ili uweze kuendelee lazima ushirikiana nazo ili uweze kujijengea uwezo, jambo ambalo tumeshindwa ni kuweka mkakati wa kujenga uwezo wa ndani, wa kuweza kuwa na viwanda vinavyotengeneza bidhaa kwa kuweza kuongeza thamani ya malighafi tunazozalisha ndani ya nchi, na kuweza kutrumia vizuri rasilimali zetu na kuweza kujiletea maendeleo, tumekuwa na udhaifu katika matumizi ya fedha za umma, tumekuwa na udaifu katika ukusanyaji wa mapato ya serikali na kutumiwa kwa tija ili kuongeza uzalishaji, kukipa kipaumbele kilimo cha mkulima mdogomdogo ili aweze kuongeza uzalishaji kwa kuwa anakuwa soko la bidhaa za viwandani,” alisema.  



Tuesday, December 24, 2013



Sudan Kusini yatimiza utabiri wa Nyerere

Bashir, Machar na Kiir
KATIKA moja ya hotuba zake, Rais wa Kwanza wa Tanzania, marehemu Julius K. Nyerere, aliwahi kusema kuwa, dhambi ya ubaguzi ni mbaya kama ilivyo tabia ya kula nyama ya mtu, kwamba ukianza kula nyama ya mtu, hutaacha.
Aliyasema hayo mwaka 1995 alipokuwa katika Hoteli ya Kilimanjaro (kwa sasa Hyatt Regency Dar es Salaam), jijini Dar es Salaam alipoonya juu ya madhara ya kutaka kuuchezea na hatimaye kuuvunja Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliozaa Tanzania.
Nyerere akasema, “Watu wazima wameuzungumza Muungano kwamba tuuvunje au uendelee. Mtu mwenye akili hawezi kufikiri Uzanzibari ni fahari.” Akasema kuwa, nje ya Muungano, kuna Wapemba na Waunguja. “Mtamaliza kutengana na Watanganyika, mara mtakuta kumbe sisi si Wazanzibari.”
Mwalimu Nyerere akasema, “Mtajikuta kuna Wapemba na Waunguja. Wapemba watapata msukusuko kidogo na mara mtakuta kuna Wazanzibari na Wazanzibara. Hamtakaa salama. Hamuwezi mkakaa salama baada ya kutenda dhambi ya kuwabagua watu wa nchi yenu ileile moja mkawaita wale wao na hao sisi. Dhambi ile haiishii hapo….”,
Tofauti na Mwalimu alivyokuwa akitabiria Tanzania, utabiri huo umetimia katika nchi mpya ya Sudan Kusini iliyojipatia uhuru wake, Julai 9, 2011.
Uhuru huo ni zao lililotokana na hatu ya Januari 2011 baada ya wakazi wa Sudan Kusini kupiga kura juu ya swali la kujitenga na Sudan wakaamua karibu kwa kauli moja kuwa nchi huru.
Sababu kubwa inayoelezwa ya kujitenga kwa nchi hiyo inaelezwa kuwepo kwa tofauti kubwa kati ya nchi hizo ni kwamba katika Sudan yenyewe idadi kubwa ya watu wamekuwa Waislamu na utamaduni wao una mchaganyiko wa tabia za Kiarabu na Kiafrika na wengi wakizungumza lugha ya Kiarabu.
Kumbe kusini kuna Waislamu wachache, wengi ni wafuasi wa dini za jadi na wengine wakiwa wakristo.
Ukizungumzia upande wa kiuchumi na elimu nchi ya kusini ilielezwa kuwa nyuma ukilinganisha na nchi ya kaskazini.
Shinikizo la kimataifa lilizidi kuuandama uongozi wa Bashir ambako mwaka 2001, viongozi wa Umoja wa Mataifa walitoa wito kufanyika kwa jitihada za kumaliza mgogoro na kuruhusu misaada ya kibinadamu na wafanyakazi wa kimataifa kutoa msaada kusini mwa Sudan.
Amani ilipatikana baada ya kusainiwa rasmi kwa Mkataba wa Amani jijini Nairobi kwa pande zote mbili na Januari 9, 2005 na al-Bashir alikubali mkataba wa amani uliomaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe na kuiwezesha Sudan Kusini kupata haki ya kujitawala.
Lakini vita vingine vya ndani vilianza katika eneo la Darfur (Sudan Magharibi) na kutokea kwa mauaji mengi na kufanyika matendo ya kinyama dhidi ya raia hali iliyomfanya al-Bashir mpaka leo kukabiliwa na mashtaka mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai(ICC), kama mshtakiwa wa makosa ya jinai dhidi ya haki za binadamu.
Baada ya kutengana kwa sababu hizo na nyingine nyingi na baadaye kufanikiwa kupata uhuru wakagundua kuwa nchi hiyo lazima itawalike kwa kuchanganya viongozi wa makabila mawiliu makuwa ambayo ni Lou Nuer analotokea aliyekuwa Makamu wa Rais Riek Machar na kabila la Dinka analotokea Rais Silva Kiir.
Lakini baada ya kuingia madarakani chokochoko zilianza na baada ya kufanyika kwa uchunguzi iligunduliwa kwamba Machar alikuwa na nia ya kutaka kumpindua Rais Kiir hali iliyofanya Julai mwaka huu achukue uamuzi mgumu wa kumtimua wadhifa huo.
Baada ya kumtimua Machar alisahau kwamba nchi hiyo ilijengwa kwa misingi ya makabila mawili hivyo ndani ya jeshi kulikuwa na makananda wengi waliokuwa wakitokea katika kabila la kiongozi huyo.
Mara baada ya kumuondoa wanajeshi hao walilichukulia suala hilo sawa na kutengwa na hivyo kumuona Kiir kama msaliti wao kwa kutaka kutawala mwenyewe na kabila lake kwa kugawana keki ya taifa.
Wanajeshi hao waliamua kumuunga mkono Machar na kutangaza kuasi jeshi na kuingia msituni kwa nia ya kuung’oa utawala wa Kiir.
Wanajeshi hao kwa sasa wameshafanikiwa kuteka baadhi ya miji katika nchi hiyo hali inayoweonesha uwezekano wa kuzuka kwa mapigano makubwa zaidi na kufanya hali katika taifa hilo jipya changa kabisa duniani kutibuka kwa haraka ambapo hivi sasa maelfu ya raia wakihama nchi hiyo kwa kukimbia vita.
Inaripotiwa kwamba idadi ya vifo mpaka sasa imefikia 1,000 huku mapigano yakiendelea kwa zaidi ya wiki.
Machar ameapa kumuondowa Kiir madarakani na vikosi vyake tayari vimeuteka mji wa Bor ambao ni mji Mkuu wa jimbo lenye vurugu la Jonglei ukiwa kama kilomita 200, kaskazini mwa mji mkuu wa Juba na pia wameuteka mji wa Bentiu ambao ni mji mkuu wa jimbo muhimu lenye kuzalisha mafuta la Unity.
Serikali ya Juba imekiri kwamba waasi wamefanikiwa kuchukua udhibiti wa majimbo ya Joglei na Unity huku maelfu ya watu wakikimbilia katika Mako Makuu ya Umoja wa Mataifa (UN) kupata hifadhi.
Msemaji wa jeshi la Sudan Kusini Philip Aguer mpaka jana alisema kuwa serikali imechukuwa hatua kwa ajili ya kufanya mashambulizi ya kurejesha miji yao iliyotekwa na waasi.
Anasema kuwa wanajeshi wao wataukombowa mji mwa Bor kutoka kwa vikosi vya waasi ambao bado unadhibitiwa na vikosi vya Machar lakini wanajiandaa kuudhibiti tena.
Matamshi hayo yanaibuka licha ya kuwepo kwa juhudi za kidiplomasia za mataifa ya Afrika na wito kutoka Marekani, Uingereza na Umoja wa Mataifa wa kutaka kusitishwa kwa mapigano hayo.
Mratibu mkuu wa masuala ya misaada ya kibinaadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini Toby Lanzer ameutembelea mji huo wa Bor juzi na kusema kwamba hali inazidi kuwa mbaya.
Amesema kuna maelfu ya raia wa Sudan Kusini waliokimbilia vichakani au kurudi kwenye vijiji vyao ili kuepuka madhara.
Ameongeza kusema ana wasi wasi mkubwa wa vita vinavyounyemelea mji huo ambapo amekiri kwamba ni jambo lisilofikirika kwa wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa kuwa katika uwezo wa kuwalinda raia wanaokadiriwa kufikia 15,000 wanaotafuta hifadhi katika kambi ya UN iliyoko huko.
Kwa mujibu wa Lanzer raia wa Australia,Uganda na Ethiopia ni miongoni mwa watu wanaotafuta hifadhi katika kambi ya UN huko Bor.
Ofisa huyo mwandamizi wa UN pia amesema helikopta za kiraia zimewahamisha raia wa Marekani kutoka mji huo ulioshuhudia mashambulizi mazito ya bunduki za rashasha lakini kuna raia 3,000 wa nchi kama vile Canada,Uingereza na Kenya wameendelea kuwaondoa katika mji huo.
Lanzer ambaye anatafuta msaada wa kifedha wa haraka kutoka Jumuiya ya Kimataifa amesema idadi ya wakimbizi wa ndani ya nchi inaweza kupindukia na kufikia 100,000.
Rais Barack Obama wa Marekani mwishoni mwa wiki ametuma barua kwa viongozi wa bunge la nchi hiyo akiwajulisha kwamba huenda akachukua hatua zaidi za kijeshi Sudan Kusini ili kuwalinda raia wa Marekani, wafanyakazi na mali zao.

Sunday, December 22, 2013

PACQUIAO: Mbabe anayemkuna David Beckham

pacquiao na familia yake
MARA baada ya Desemba mwaka jana kupoteza pambano lake dhidi ya mbabe Juan Manuel Marquez kwa ‘KO’ mbabe na mbunge Manny Pacquiao alionekana kama zama za utawala wake katika masumbwi zilikuwa zimefikia ukomo.
Mbabe huyo amefuta wale waliokuwa na dhana hiyo baada ya kurejesha heshima yake kwa kumchakaza kwa pointi Brandon Rios mjini Macau, katika pambano alilolifanya kwa ajili ya kusaidi waathirika wa mafuriko yaliyotokea nyumbani kwao Ufilipino na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 4000 na wengine milioni nne wakikosa makazi.
Alishinda kwa jumla ya pointi 120 kwa 109 na baada ya kumalizika kwa pambano hilo Pacquiao alitamka bayana kwamba yuko tayari kupambana na bondia yeyote akiwamo mbabe asiyepigika Floyd Mayweather.
Bob Arum ambaye ni promota wa Pacquiao ametenga kiasi cha dola milioni 300 kwa ajili ya pambano hilo lakini Mayweather ameshalitolea nje kwa kusema kuwa “sina mpango wa kufanya kazi na promota huyo, kwa sababu ni mbabaishaji amekuwa akikataa kuweka pambano hilo katika miezi ninayotaka ya May na Septemba,”.
USICHOKIJUA
Usichokijua ni kwamba mwanasoka maarufu kutoka Uingereza, David Beckham amebainisha kwamba ni shabiki mkubwa wa mbabe Manny Pacquiao na kwa kuthibitisha hilo hata katika pambano lake lililopita alisafiri hadi Macau kwenda kumshangilia.
Jambo jingine ni kwamba Manny Pacquiao amekuwa ni mpenzi wa hayati Bruce Lee na amekuwa akipenda kuuweka mwili wake kama mpambanaji huyo wa zamani aliyejipatia sifa kubwa duniani.
Kuingia katika katika medani za siasa haikuwashangaza sana Wananchi wa Ufilipino kwa kuwa alishaanza kukuzwa na rais wan chi hiyo, Arroya.
Mwaka 2012, Pacquiao aliweka rekodi ya kushika nafasi ya pili ya kuwa mwanamichezo na bondia anayelipwa zaidi duniani akilipwa dola milioni 62 huku nafasi ya kwanza ikikamatwa Floyd ‘Money’ Mayweather.
Ukiachilia masuala ya ngumi pia ni mwigizaji mzuri wa filamu akiwa amecheza tamthilia kadhaa zinazoratibiwa na ABS-CBN
UTAJIRI
Mbabe huyo anamiliki utajiri unaofikia kiasi cha dola milioni 100 (sawa na shilingi bil. 160).
Fedha hizo amekuwa akiziingiza kwa mchezo wa ngumi na kufanya matangazo mbalimbali ya kibiashara ikiwamo tangazo la bia za San Migue.
Ukiachilia hayo mbabe Manny anamiliki baada yake kubwa katika maeneo maarufu kwa starehe katika kisiwa Boracay huko Aklan akiwa ameshirikiana na mfanyabiashara mwingine, Crisostomo ‘Cris’ Aquino waliyoianzisha tangu mwaka 2006.
Baa ya wawili hawa inajulikana kwa jina la Boracay West Cove ikiwa inakarabatiwa kila mwaka kwa kufanya kuwa na muonekano mzuri na mpya.
NYUMBA
Mbabe huyo anamiliki mjengo mkubwa nchini mwao, ikiwa na vyumba vya kulala saba, nyumba hiyo iko kwenye eneo lenye ukubwa wa mita za mraba 2,300.
Paa lake limejengwa kwa vigae maalum kutoka nchini Japan ikiwa ni pamoja na geti la kufunguliwa kwa rimoti.
Jumba hilo lina bwawa la kuogelea ambalo lina sura ya glovu ya ngumi, kwa pembeni ya bwawa hilo kuna vitu kwa ajili ya waogeleaji na wageni wa nyumba hiyo. Jumba hilo pia lina gereji yenye uwezo wa kuhifadhi magari saba.
Bondia huyo ametumia gharama kubwa za fedha kwa ajili ya kulifanyia ukarabati jumba hilo na kuliwezesha kuwa na muonekano mzuri na wa kuvutia.
USAFIRI
Pamoja na kwamba mbabe huyo amekuwa na magari mengi lakini amekuwa akipenda zaidi kutumia gari aina ya Brand-new Ferrari 458 Italia.
MAHUSIANO
Jinkee Pacquiao 2006, Ara Mina aliyekuwa naye tangu mwaka 2007 na Krista Ranilo aliyedumu naye tangu mwaka 2009 hadi 2010.
Mbabe huyo anaishi na mkewe anayejulikana kama Maria Geraldine Jamora na wamefanikiwa kupata watoto wanne ambao ni Emanuel, Princess, Michael na Queen Elizabeth.
WASIFU
JINA: Emanuel  Manny Pacquiao
UMRI: Desemba 17, 1978
ENEO LA KUZALIWA: Bukidnon, Mindanao, Philippines
KIMO: Futi 5 na inchi 6
UTAIFA: Ufilipino


Wanigeria waandamana kupinga shirika la Ufaransa

LAGOS, Nigeria
MAMIA ya raia nchini humo wamefanya maandamano kupinga kutekelezwa mapatano kati ya nchi yao na Shirika la Kifaransa la Arva.
Maandamano hayo yaliyowajumuisha wafanyakazi, wanafunzi wa vyuo vikuu, waandishi wa habari, wanasiasa na viongozi wa taasisi zisizo za kiserikali, yalifanyika juzi mbele ya bunge la Nigeria na karibu na ofisi ya shirika hilo la Ufaransa.
Waandamanaji walishindwa kufika ofisi za Arva baada ya polisi kuweka uzio karibu na ofisi za shirika hilo.
Mmoja wa waratibu wa maandamano hao Ali Idris amesema “Kwa miaka 45 sasa Ufaransa imekuwa ikishirikiana na viongozi wa Nigeria katika kupora madini ya uran ya nchi yetu.”
Aidha mwanaharakati huyo ameongeza kwa kusema kuwa, karibu taa 135 zimekuwa zikiwaka katika makazi na makampuni ya wafaransa, zinawaka huku raia wa Nigeria wenyewe wakiendelea kutumia kuni.
Amesema kuwa, mikataba yote iliyowekwa kati ya serikali ya Abuja na  Shirika la Arva la Ufaransa, haina usawa wowote na miongoni mwa asilimia 70 ya madini ya urani yanayozalishwa nchini Nigeria ni asilimia 5 pekee ya madini hayo ndiyo hubaki nchini humo.
Raia wa Nigeria wanataka kubatilishwa mikataba hiyo kati ya serikali na shirika hilo.


Chama tawala cha Gabon chashinda uchaguzi wa majimbo

LIBREVILLE, Gabon
CHAMA tawala cha Democratic(PDG), ambacho kimeongoza nchi hiyo kwa muda wa miaka 45, kimeshinda kwenye uchaguzi wa majimbo uliofanyika Desemba 14.
Akitangaza matokeo rasmi ya uchaguzi huo juzi, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Gabon Jean Francois Ndongou amesema Madiwani 1,500 kati ya 2,404 wa Chama cha PDG wameshinda kwenye uchaguzi huo.
Chama hicho kimechukua majimbo 122, lakini kimepoteza majimbo ya Mouila, Bakoumba Oyem na Mitzic.
Matokeo hayo yanaweza kurekebishwa au kutenguliwa na mahakama ya katiba, ambayo ina uwezo wa kushughulikia mizozo ya uchaguzi.
Juzi asubuhi, Waziri Mkuu wa zamani Jean Eyeghe Ndong, ambaye chama chake cha Libreville kimechukua nafasi ya tatu, alisema yupo tayari kwa mazungumzo na chama tawala ili kuunda serikali ya muungano.


Obama avionya vikosi vya uasi Sudani Kusini

JUBA, Sudan Kusini
RAIS wa Marekani Barack Obama juzi amevionya vikosi vya waasi nchini Sudan Kusini vinavyofanya mapinduzi ya kijeshi baada ya kuwajeruhi wanajeshi wanne wa Marekani.
Hayo yamebainishwa kwenye taarifa kutoka ya Ikulu ya nchi hiyo imeeleza kuwa juhudi zozote za kunyakua madaraka kwa nguvu za kijeshi zitakazosababisha kukoma kwa msaada wa muda mrefu kutoka Marekani na Jumuiya ya kimataifa.
Rais Obama amesisitiza kuwa viongozi wa Sudan Kusini wanalo jukumu la kusaidia juhudi za Marekani kuwaokoa wamarekani na raia wengine huko Juba na Bor mji ambao unashikiliwa na waasi.
Onyo la rais Obama linatolewa baada ya ndege tatu za Marekani kushambuliwa kwa risasi wakati zikielekea Bor kusaidia juhudi za kuwaondoa Wamarekani nchini Sudani Kusini kutokana na kuchachamaa kwa mapigano baina ya serikali na waasi.
Jeshi la Serikali ya Sudan Kusini lipo kwenye harakati za kutaka kuukomboa mji wa Bor, ulioko kaskazini mwa mji mkuu Juba, kutoka wanajeshi walioasi na kumuunga mkono makamu wa rais wa zamani, Riek Machar aliyefukuzwa kazi hivi karibuni na rais wa nchini humo, Silva Kiir.
Baada ya kutangazwa kutekwa kwa mji huo mara moja, Marekani ilipeleka wanajeshi wake 45 kuwalinda raia wake wanaofanyashughuli zao hapo na mali zao.
Kuna taarifa zinasema kuwa ndege za Uganda pia zimekuwa zikihusika katika kusaidia serikali ya Sudan kuukomboa mji wa Bor kutoka kwa wanajeshi walioasi.
Wakati hayo yakijili kiongozi wa waasi wa Sudan Kusini Riek Machar amesema kuwa, vikosi vyake vimefanikiwa kuchukua udhibiti wa jimbo muhimu la uzalishaji mafuta la Unity nchini humo.
Makamu huyo wa zamani wa rais amedai kuwa, vikosi vyake ambavyo vinapambana na askari wa serikali vinadhibiti sehemu kubwa ya nchi hiyo. Kabla ya hapo pia jeshi la Sudan Kusini lilikuwa limetangaza habari ya kujiengua serikalini kwa Jenerali James Kwang Chol aliyekuwa kiongozi wa kijeshi katika jimbo hilo la Unity nchini humo na kujiunga na waasi.
Habari kutoka Addis Ababa, Ethiopia zinasema kuwa, ripoti iliyotolewa na Umoja wa Mataifa zinasema kuwa AU imelaani vikali mauaji dhidi ya askari wa kulinda amani wa UN na raia wasio na hatia, yaliyotekelezwa katika kambi ya nchini hapa.
Mapigano hayo yalizuka siku ya Jumapili iliyopita mjini Juba, ambao ni mji mkuu wa Sudan Kusini na hatimaye kuenea katika maeneo mengine ya nchi hiyo.
 

Sample text

Sample Text

PATA HABARI NA BURUDANI MBALI MBALI POPOTE ULIPO!

Sample Text