Social Icons

PATA HABARI NA BURUDANI MBALI MBALI POPOTE ULIPO!

Thursday, December 13, 2007

TUZO ZA KILI' 2007




TUZO za ‘Kili Music Award’ ambazo hutolewa kila mwaka, mwaka 2007 zimechukua sura tofauti na zilivyokuwa zimezoeleka miongoni mwa mashabiki wa muziki kwa takribani miaka sita iliyopita tangu kuanzisKatika miaka iliyopita, ilizoeleka kuona msanii, akinyakua tuzo zaidi ya moja katika nyanja tofauti, lakini juzi hali ilikuwa tofauti, kwani karibu kila msanii aliyebahatika, aliondoka na tuzo moja ndani ya ukumbi huo.
Hii inaonyesha kwamba muziki wa Tanzania umekuwa na ushindani mkubwa kwa baadhi ya wasanii kufanya kazi zenye viwango vinavyokubalika katika jamii.
Tuzo ya msanii bora wa kike, ilinyakuliwa na Rehema Chalamila ‘Ray C’ baada ya kuwashinda Afua Suleiman, Hafsa Kazinja, K-Lynn na Mwanahawa Ally.
Mwanamuziki bora wa kiume aliibuka Banana Zorro, ambaye aliwapiga kumbo, Jose Mara, Mzee Yusuf, Marehemu Omari Kopa na Shabani Katwila ‘Q Chillah’.
Tuzo ya albamu bora ya taarabu ilikwenda kwa kundi la East African Melody kupitia albamu yao ya ‘Hamniwezi’ ambayo iliwaacha midomo wazi kundi la Zanzibar Stars, na albamu yao ya ‘Najiamini’, ‘Two in One’ ya Jahazi Modern taarabu, ‘Udugu mchana’ ya East African Melody na ‘Vijimambo’ ya Dar es Salaam Modern taarab.
Kibao ‘Najiamini’ cha Zanzibar Stars kilishinda tuzo ya wimbo bora wa taarab na kuubwaga ‘Best Maridadi’ wa East African Melody, ‘Udugu mchana’ na ‘Mkuki kwa nguruwe’ za Jahazi Modern Taarab, na ‘Vijimambo’ wa Dar es Salaam Modern Taarab.
Seif Shabani ‘Matonya’ aliibuka na tuzo ya nyimbo bora ya mwaka kutokana na wimbo wake ‘Violet’, akizilambisha vumbi ‘Dunia Kigeugeu’ wa FM Academia ‘Wazee wa Ngwasuma’, ‘Hujafa hujasifiwa’ wa Twanga Chipolopolo, ‘Nilikataa’ wa Top Band na ‘Pressure’ wa Hafsa Kazinja.
Bendi iliyokuwa ikililia kupata tuzo hizo za Kili kwa muda mrefu kwa vigezo kuwa wana kila vigezo vya kunyakua tuzo hizo bali, fitna tu ilikuwa ikitembea, FM Academia juzi kwa mara ya walitwaa tuzo kwa kutoa, wimbo bora wa Kiswahili, ‘Dunia Kigeugeu’ na kuzishinda African Stars na kibao chao ‘Furaha ya harusi’, ‘Hujafa hujasifiwa’ wa Twanga Chipolopolo, ‘Maisha mzunguko’ wa Msondo Ngoma na ‘Ugumu wa Maisha’ wa TOT Plus.
Tuzo ya albamu bora ya bendi ilikwenda kwa wakongwe Msondo Ngoma na albamu yao ‘Maisha mzunguko’ na kuwashinda FM Academia, DDC Mlimani Park, Twanga Chipolopolo na African Stars.
Naye msanii chipukizi Q Jay na wimbo wake ‘Sifai’ alionyesha ukali wake kwa kuchukua tuzo ya wimbo bora wa R ‘n’ B, akiwamwaga PNC, Joslin, Top Band na Matonya.
Moja ya tuzo inayotiliwa shaka ni hii ya mkali wa Hip hop ambayo ilikwenda kwa Ambwene Yessaya ‘AY’ kwa kuwamwaga wasanii wanaotambulika kwa kufanya muziki huo kama akina Fid Q ambaye ni mwanamapinduzi wa Hip hop mwenye uwezo wa kuwapoteza wasanii wanaomualika katika maonyesho yao kutokana na kukubalika kwake, Nako 2 Nako Solders kundi ambalo lilimvutia rapa wa Marekani, Loon kwa uchanaji wao na kuwaomba kufanya nao kazi kutokana na Hip hop yao iliyosimama, Joh Makini jina ambalo lipo juu midomoni mwa watu wa rika zote wapenda hip hop na Rado, msanii anayesifika kwa misimamo yake ya hip hop.
Wasi wasi nilionao ni katika tuzo ya mwanamuziki bora wa rap iliyokwenda kwa msanii chipukizi, Chid Benzino na kuwaacha wakongwe na wakali kama Fid Q, Joh Makini, Mansu-Li na Rado.
Tuzo iliyonifanya niwaondolee imani waandaaji wa tuzo hizi kuwa washiriki walipatikana bila kura ni hii ya mwanamuziki bora wa Afrika Mashariki iliyokwenda kwa Nameless ambayo ilikuwa ikiwaniwa pia na wasanii Nyota Ndogo, Ngoni, E.A Bashment Crew (Kenya/Uganda) na Amani.
Swali linakuja, hivi kweli kuna Mtanzania anayeweza kuwachagua wasanii wa Afrika Mashariki pasipo kumtaja msanii wa nyumbani hata mmoja? Hapa napata shaka na kuona hata hawa wengine walichaguliwa na kamati ya waandaaji.
Tuzo nyingine ambayo ilinishangaza ni hii ya muandaaji bora wa muziki iliyokwenda kwa Said Commorien, na kumuacha mwanamuziki kama Hassan Bitchuka aliyetunga nyimbo zaidi ya 200 zinazojulikana, hiki ni kioja, tuzo hiyo pia iliwashindanisha Ally Choki, Mzee Yusuph na Marehemu Omari Kopa.
Bendi ya muziki wa asili ya Che Mundu & Mbega Arts haikubaki katika tuzo hizo, ilipong’ara na wimbo wake wa ‘Makonde’ na kunyakulia tuzo ya wimbo bora wa asili na kuiacha Makonde Group.
Albamu bora ya asili iliibuka ‘Kila munu ave na kwao’ ya Makonde Group baada ya kuishinda Chemundu & Mbega Arts.
Abbas Khamis ‘20%’ aliibuka na tuzo ya mwanamuziki bora wa Reggae/Ragga akiwabwaga Besta Prosper, Jhikoman, Lady E na Juma Mhina ‘Pijei’.
Tuzo ya waandikaji mashairi bora ya muziki ilikwenda kwa Said Commorien, aliyewabwaga Ally Choki, Hassan Bitchuka, Mzee Yusuf na Marehemu Omari Kopa.
Master Jay alijinyakulia tuzo ya mtayarishaji bora wa muziki akiwashinda Allan Mapigo, Makochali, Roy Bukuku na Said Commorien.
Tuzo ya mtunzi bora ilikwenda kwa Mzee Yusuf, aliyewashinda Q Chillah, Feresh na Ally Choki wakati tuzo ya waandaaji bora wa video ilikwenda kwa Visual Lab, iliyozishinda Empyt Soulz Production na Chapakazi Production.
Wimbo bora wa Zouk uliibuka ‘Pressure’ wa Hafsa Kazinja akiwashinda Mwasiti Almasi na wimbo wake ‘Niambie’, ‘Binti Kimanzi’ wa 20%, ‘Mama Kumbena’ wa Banana Zorro na ‘Wasiwasi wa Mapenzi’ wa Stara Thomas.
MwanaFA aliibuka kidedea katika wimbo bora wa ushirikiano, kutokana na kibao chake ‘Hawajui’ alichomshirikisha Lady Jaydee. Pia tuzo hiyo ilikuwa ikiwaniwa na K-lynn na Squeezer na kibao chao ‘Crazy over you’, ‘Dhahabu’ wa Dully Sykes aliowashirikisha Joslin na Mr Blue, ‘Nipe mimi’ wa Mheshimiwa Temba na Ray C na ‘Pressure’ wa Kazinja na Banana.
Mtoto wa marehemu Morris Nyunyusa alichukua tuzo ya heshima ya milele kwa niaba ya marehemu baba yake, ambayo pia ilishawahi kutolewa kwa marehemu Cool James ‘Mtoto wa Dandu’.
Hafla hiyo ilipambwa na burudani kutoka kwa rapa wa zamani bendi ya Stone Musica, ‘Wajelajela Original’, Ndanda Cossovo ‘Kichaa’ aliyeibuka na bendi yake mpya akitokea Marekani alipokuwa amekwenda kwa shughuli zake za kimuziki.
Burudani nyingine ilitoka kwa msanii Jose Chameleon, Ali Kiba, Malima Lawrence ‘Marlow’ na wengineo.

0 comments:

 

Sample text

Sample Text

PATA HABARI NA BURUDANI MBALI MBALI POPOTE ULIPO!

Sample Text