JOHANNESBURG, Afrika Kusini
HUKUMU iliyosomwa na Jaji Seun Moshidi wa Mahakama kuu ya Johannesburg kwa kuwahukumu kifungo cha maisha watu watatu kwa kosa la kumuua mwanamuziki, Luck Dube imeamsha hisia za wapenzi na mashabiki wa mwanamuziki huyo.
Watu hao waliohukumiwa kifungo hicho ni Sifiso Mhalanga (34) , Julius Ngxowa (32) na Mbuti Mabe (31) siku ya hukumu hiyo mahakama ilijaa na lundo la watu wakiwa na huzuni mara baada ya kutangazwa hukumu watu waliokuwa hapo walishindwa kujizuia na kujikuta wakishangilia hukumu hiyo.
Kifo chake
Kifo cha Philip Luck Dube kilitokea, Oktoba 18, baada ya kupigwa risasi katika Kitongoji cha Rosettenville, kilichopo Johannesburg. Siku aliyokuwa na watoto wake wawili ambao hawakujeruhiwa katika tukio hilo.
Watu hao watatu walimuua Dube majira ya saa 2 usiku baada ya kumteka akiwa na gari lake la kifahari aina ya Chrysler.
Dube aliyeaga dunia akiwa na umri wa miaka 43, ni mmoja kati ya wanamuziki walioweka historia ya kuutambulisha muziki wa reggae nje ya Afrika ikiwa ni pamoja na kuweka historia ya kuwa mwanamuziki wa kwanza Afrika Kusini kuachia CD nyingi zaidi na zenye ubora kuliko mwanamuziki mwingine.
HISTORIA YAKE:
Lucky Dube alizaliwa katika eneo lililokuwa likijulikana kwa jina la Ermelo, mashariki ya Transvaal. Kwa sasa linajulikana kama Mpumalanga.
Mama yake, Sarah aliamini maishani mwake asingepata mtoto, kutokana na mara kadhaa kupata ujauzito na kuharibiki, hivyo kumzaa Lucky ‘Bahati’, kwake ilikuwa sawa na miujiza.
Wazazi wake waliachana kabla ya kuzaliwa kwake na alikulia kwa mama yake akiwa na ndugu zake wawili - Thandi na Patrick.
Akiwa kinda Dube alijihusisha na kufanya kazi ya utunzaji wa bustani, kazi ambayo haikuwa ikimuingizia fedha za kutosha kwa ajili ya kujikimu kimaisha na familia yake, na wakati huo akiwa anasoma shule ya Sekondari.
Kimuziki Luck alianza mara baada ya kumaliza shule wakati huo akiwa na umri wa miaka 18, akijiunga na bendi ya binamu yake ya The Love Brothers, akiwa mpenzi wa muziki wa kitamaduni wa Kizulu uliokuwa ukijulikana kama ‘mbaqanga’.
Wakati Dube akijihusisha na masuala ya kimuziki kwenye bendi hiyo, alikuwa akisoma na masuala ya kimuziki alikuwa akiyafanya wakati wa likizo.
Alizindua albamu yake ya kwanza kwa jina la ‘Lucky Dube’ na albamu yake ya pili aliita ‘Super soul’, albamu aliyoiachia mapema iliyokuwa katika lugha ya Kiafrikana na Kizulu wakati albamu zake hizo zikiwa hewani Dube alianza kujifunza Kiingereza.
MGUSO WA REGGAE:
Mwaka 1984 aliachia albamu ya reggae ya ‘Rastas Never Die’ lakini haikuwa bora katika utengenezaji ila iwagusa mashabiki wengi jambo hilo lilimpa moyo na kutengeneza albamu nyingine ya reggae iliyojulikana kama ‘Think About The Children’ aliyoitoa mwaka 1985 na ilifanikiwa kuuza nakala zaidi ya milioni moja na kupata tuzo ya mwimbaji bora wa reggae Afrika Kusini.
Mwaka 1989 Dube alijikusanyia jumla ya tuzo nne za OKTV kupitia albamu yake ya ‘Prisoner’, pia alishinda tuzo nyingine ya Captured Live na mwaka uliofuata alipata kwa kupitia albamu yake ya ‘House of Exile’.
Mwaka 1996 chama kinachoangalia tathmini za mauzo ya reggae kilimtaja kama muuzaji bora wa muziki wa reggae Afrika kwa kupitia albamu yake ya ‘Serious Reggae Business’, ikiwa ni pamoja na tuzo za World Music Awards kwa kuwa ‘Mwanamuziki Bora wa Kimataifa wa Mwaka’. Pia alipata tuzo za muziki nchini Ghana ikiwa ni pamoja na kupata tuzo tatu za albamu zake tatu nchini Afrika Kusini.
Pamoja na kwamba kumekuwa na imani ya wanamuziki wengi wa reggae kuvuta bangi, sigara au kunywa pombe kupita kiasi, kwa Lucky Dube ilikuwa ni tofauti kwani alikuwa havuti sigara, hanywi pombe wala havuti bangi, kitu ambacho si cha kawaida kwa watu wa madhehebu ya Rastafarian.
Amewahi kushinda jumla ya tuzo 20 za kimataifa na Afrika Kusini alizozipata kutokana na ubora wa nyimbo zake. Mbali na muziki, Dube alikuwa mshabiki mkubwa mchezo wa farasi, pia alikuwa na shamba la mchezo huo huko eneo la Kwa-Zulu Natal.
Mwisho
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment