
Tuzo za MTV Afrika kufanyika Kenya
*Majina ya wanaowania yaanikwa
*Afrika Mashariki, wamo Kenya, Uganda, Tanzania hoi
Na Shabani Matutu
TUZO za Muziki za MTV Africa zilizowahi kufanyika katika Ukumbi wa The Velodrome, Abuja, Novemba 22, 2008 zimetangazwa kufanyika jijini Nairobi, Kenya mwaka huu.
Nchi ya Kenya inaandaa tuzo hizo kwa mwaka huu ikiwa imeshirikiana na Zain (MAMA).
Tuzo hizo zinatarajiwa kufanyika Oktoba 10, 2009 katika ukumbi wa Indoor Arena, Kituo cha Michezo cha Kimatifa cha Moi, Nairobi.
Mpaka sasa yameshatajwa baadhi ya majina ya makundi na wasanii wanaowania tuzo hizo.
Kwa maeneo ya Afrika Mashariki pia yameweza kuonekana majina kadhaa ya wasanii na makundi lakini kwa hapa Tanzania hakuna msanii anayeshiriki kuwania tuzo hizo.
Mwaka jana tuzo hizo ambazo zilifanyika Abuja, Nigeria msanii Profesa Jay aliweza kuiwakilisha nchi, katika nafasi ya msanii bora wa Hip hop Afrika mashariki.
Pamoja na kwamba hakupata tuzo hizo lakini ilisaidia kuitangaza Tanzania kama moja ya nchi yenye wasanii wazuri.
Kutochaguliwa msanii hata mmoja kuingia kwenye kinyang’anyiro hicho kunaleta maswali kadhaa ya kujiuliza.
Moja ya swali hilo ni kwamba inawezekana wasanii wa hapa nchini uwezo wao umepungua? Swali ambalo jibu lake sitaki kuamini hivyo.
Swali jingine linalojengeka ni kwamba je wasanii wetu wamejibwetesha na mafanikio ya kujulikana hapa nyumbani na kushindwa kujitangaza nje?
Yote kwa yote jibu linabaki zaidi kwao ambao wanakuwa wanajua hasa nini sababu ya wao kukosa kutokea katika tuzo hizo kubwa duniani.
Kukosekana kwa wasanii wa Tanzania inanipa picha kwamba watakosa kujitangaza kwa watazamaji wanaokadiriwa kutazama sherehe hizo za utoaji wa tuzo wanaokaribia bilioni moja kupitia TV duniani kote.
Kwa mujibu wa Alex Okosi, makamu wa Rais na Mkurugenzi Mtendaji wa MTV Networks Africa, amesema kuwa wanatarajia kuingiza zaidi ya mashabiki 5,000 katika sherehe hizo zinazofanyika katika Ukumbi wa Indoor Arena, na mamilioni wengine watakuwa wakitazama kwa kutumia televisheni.
Katika sherehe za utoaji wa tuzo za mwaka jana wasanii wakubwa waliofanya onyesho walikuwa ni Kelly Rowland, Flo Rida, The Game, Jua Cali, P Square, 9ice, D’Banj, Asa, Cassette na Jozi.
Wengine walioimba siku hiyo ni pamoja na Wahu ambaye alitwaa tuzo ya muimbaji bora wa kike, D’Banj muimbaji bora wa kiume, Jozi muimbaji bora wa jukwaani na P Square waliotwaa tuzo ya Kundi Bora.
Kwa hapa nyumbani mashindano hayo yatakuwa yakioyeshwa moja kwa moja na Televisheni ya Taifa (TBC1).
Baada ya kumalizika kwa sherehe za utoaji wa tuzo inatarajiwa kufanyika kwa ziara katika nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Afrika Kusini, Kenya na Nigeria.
Shoo ya kwanza kufanyika itakuwa ile ya Novemba 11, itakayofanyika katika Ukumbi wa Halle de la Gombe, DRC na mgeni wa shoo atakuwa msanii wa nchini humo, Fally Ipupa.
Novemba 13, onyesho litafanyika Johannesburg, Afrika Kusini katika Ukumbi wa Standard Bank Arena.
Katika onyesho hilo la Afrika Kusini wasanii wanaounda Kundi la The Parlotones la Afrika kusini ambalo nalo limeteuliwa kuwania tuzo ya kundi bora la mwaka ndilo litakuwa wenyeji.
Wengine watakaoshiriki katika onyesho hilo ni pamoja na HHP wa Afrika kusini aliyeteuliwa kuwania tuzo ya muimbaji bora wa kiume, msanii bora wa hip hop na msanii bora wa mwaka.
Pia Cassette wa Afrika Kusini anayewania tuzo ya muimbaji bora mwenye uwezo wa kumilimiki jukwaa na mwingine ni Loyiso wa Afrika Kusini aliyeteuliwa kuwania tuzo ya msanii bora wa R&B.
Onyesho jingine litakuwa la Novemba 15, la Nairobi, Kenya litakalofanyika katika Ukumbi wa Bomas.
Katika onyesho hilo msanii mualikwa atatoka Nigeria, 2face Idibia ambaye naye anawania tuzo ya msanii bora wa kiume.
Wengine watakaosindikiza onyesho hilo ni pamoja na Kundi la East African Bashment Crew ambalo linaundwa na wasanii Naazizi, Bebe Cool na Wayre linawania tuzo ya kundi bora la mwaka.
Jua Cali wa Kenya atakuwemo akiwania tuzo ya msanii bora wa kiume na Wahu wa Kenya atakuwa akiwania tuzo ya msanii bora wa kiume.
Novemba 18, onyesho litahamia Lagos, Nigeria katika Ukumbi wa Planet One.
Baadhi ya wasanii watakaosindikiza onyesho hilo ni pamoja na 9ice wa Nigeria anayewania tuzo ya msanii bora wa Hip Hop.
D’Banj & Mo Hits All Stars wa Nigeria wakiwania msanii bora wa kiume, waimbaji bora wa mwaka na wasanii bora wa jukwaani na Naeto C wa Nigeria anayewania tuzo ya muimbaji mpya anayefanya kazi bora.
Pia atapanda jukwaani msanii Samini wa Ghana ambaye naye anawania tuzo ya mtumbuizaji bora jukwaani.
0 comments:
Post a Comment