
NI ngumu sana kwa wanawake wa nchi za Afrika kukumbwa na kashfa za usagaji kama ilivyo kwa nchi za Magharibi lakini kwa hapa Tanzania kashfa ya aina hii imemkumba mwanadada Mamtei.
Akielezea kuhusu malalamiko hayo Mamtei anasema “mimi si msagaji jamani, nasingiziwa tu na watu wasiopenda maendeleo yangu, hasa ambayo huandikwa na vyombo vya habari, ambayo wengi hupenda kuviita magazeti pendwa.”.
Mamtei ambaye jina lake halisi ni Cesilia Sospeter Sengerema aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na Vision Tanzania yaliyofanyika hivi karibuni, Mamtei anasema kuwa anakosa amani mtaani kutokana na magazeti hayo kumwandika yakimuita msagaji.
Kutokana na shutuma hizo mwanadada huyo amekana na kusema “Jamani mimi ni mtu ninayejiheshimu na muumini mzuri wa kanisa, sasa mambo ya usagaji wapi na wapi, sijawahi na wala sitarajii kuwa msagaji.”
Mwanadada huyo mrembo anasema kuwa tangu magazeti hayo yamuandike amekuwa akipata shida ikiwa ni pamoja na kuteseka kwani kila anapopita anataniwa hasa na watoto ambao humuita msagaji.
Tabia hiyo imekuwa ikimchukiza na kumsababishia kukataa umaarufu wa aina hiyo.
“Umaarufu wa kupewa majina mabaya kama hayo siupendi kabisa, kwani unakuwa unanishushia utu wangu na heshima yangu kwa jamii,” alilalama.
Akielezea sababu ya kuitwa msagaji, anadai kwamba hafahamu kabisa.
“Sifahamu kabisa wapi jina hilo limetokea, kwani hata filamu za usagaji sijawahi kabisa kuigiza katika historia ya maisha yangu ya usanii,” alisema.
Anasema kuwa kitendo cha kuigiza kwenye tamthilia mbalimbali ikiwamo ya Jumba la Dhahabu iliyomng’arisha akiwa ameigiza kama mtu aliyewachanganya kimapenzi kina Cojak, Basupa na Mr Tues, alionekana kama mwanamke asiye muaminifu kwa mumewe na kila alipopita aliitwa tapeli wa mapenzi na mwizi wa waume za watu.
Mamtei anasema kuwa kutokana na kuigiza sehemu hiyo, watu walifikia kumtukana kutokana na kuhisi kama hiyo ilikuwa tabia yake katika mazingira ya maisha yake ya kawaida.
Pia alifafanua kuwa mara zote wasanii huwa wanavaa uhusika wakiwa na nia ya kufikisha ujumbe kwa watu ambao wanakuwa na tabia ya aina hiyo.
Mwanadada huyo kwa sasa yupo kwenye tamthilia mpya ya Jasmin inayotamba kwenye kituo cha televisheni cha TBC1, akiwa anaigiza kama mlinzi wa Jasmin binti wa mzee mmoja tajiri katika mchezo huo nafasi, ambayo inaigizwa na mzee Chilo.
Mwanadada huyo anaonekana akifukuzwa kazi na mzee Chilo baada ya kushindwa kumlinda Jasmin kwa umakini kama kazi yake ilivyokuwa ikimtaka kufanya.
Mpaka sasa Mamtei ameshaigiza tamthilia nyingi zikiwamo za Ua Jekundu, Jumba la Dhahabu na Jasmin.
Filamu nyingine ambazo ameshiriki ni pamoja na Safari, Dar es Salaam, Harusi ya kendi, Maiti ya Mwanangu, House Girl, Hosteli na nyinginezo nyingi.
Mara nyingi mwanadada huyo anaigiza filamu za kibabe na ujambazi japokuwa anamudu kuvaa uhusika vilivyo sehemu anayopangiwa.
Hali yake ya kuigiza kama jambazi imekuwa ikimpatia shida kubwa katika jamii ambako wengi wamekuwa wakimfikiria kuwa jambazi.
“Kama nikikaa mahali ambako ninakuwa peke yangu wengi huingiwa na mawazo kuwa ninapanga mipango ya kuvamia.
Naomba jamii inielewe kuwa nipo kazini kama wengine walivyo hivyo wasinichukulie vile ninavyoigiza ndivyo nilivyo kwani nafikisha ujumbe kwa njia hiyo,” anasema Mamtei.
Fani ya sanaa amekuwa akiipenda tangu akiwa kijana mdogo ambako alikuwa akipenda kucheza michezo kama ngoma, sarakasi, muziki wa asili na uigizaji.
Kutokana na kupenda kwake kuigiza tangu utotoni anaona uigizaji upo damuni kwake na anafurahi kwa kuwa ndiyo kazi hasa inayomuweka mjini.
Akizungumzia malengo yake, Mamtei anasema ni kuhakikisha na yeye anamiliki studio yake, ikiwa ni pamoja na kuwa msanii wa kimataifa.
Mwanadada huyo anasema kuwa anafahamu kuwa kama atajitahidi atakuwa na uwezo wa kumiliki studio, ikiwa sambamba na kutimiza malengo yote.
Anasema kuwa tabia iliyozuka ya kuchafuana si nzuri kwani ni hatari kama angekuwa na moyo mwepesi anaweza kufikia hatua mbaya ya kujiuzulu mwenyewe.
Akielezea historia yake kwa ufupi anasema kwamba amezaliwa miaka 25 iliyopita jijini Dar es Salaam.
Anasema kwamba pamoja na kuzaliwa Dar es Salaam, lakini yeye ni Msukuma.
Shule ya msingi amesomea Kunduchi katika mwaka 1988 hadi 1994 na elimu ya sekondari ameipatia katika Shule ya Sekondari ya Morogoro, mwaka 1996 hadi 1999.
Ni mtoto wa kwanza kati ya watoto wawili wa Sosypeter Sengerema na mama yao ambaye kwa sasa ni marehemu, Angelina Edward.
Baada ya kumaliza shule alijiunga na kundi la Fukuto Arts Professional group kabla ya kubadilishwa jina kwa sasa na kuitwa Tuesday production.
Huyo ndiye Mamtei, muigizaji anayehusishwa na kashfa za usagaji.
Mwisho
0 comments:
Post a Comment