IDD Mubarak ndugu zangu Waislamu mliosherehekea Idd el Fitr jana na mnaosherehekea siku hiyo leo nyote mliokuwa katika nia ile ile moja ya kutafuta amali za Mwenyezi Mungu.
Pamoja na kwamba leo ndiyo siku inayotambulikana kiserikali, lakini wapo baadhi ya Waislamu wa madhehebu mengine waliofungua tangu jana.
Katika makala ya leo nitazungumzia juu ya ishara zinazotuwezesha kujua siku ya kufunga au siku ya mwisho tunayotakiwa kula Idd.
Hapa sitapenda kuzungumzia kwa wale waliofungua jana wana makosa au wanaofungua leo wana makosa, ila nia ni kueleza alama zinazotuongoza kujua siku hizo.
Kumekuwa na maswali mengi inapofika Ramadhani ya 29, wengi wakijiuliza kama siku ya pili yake itakuwa Sikukuu ya Idd el Fitri.
Maswali hayo pia hupatikana katika mwanzo wa kufunga mwezi wa Ramadhani lakini jibu ni rahisi, kwani tumelezwa kwamba tunatakiwa kufunga kwa kuuona mwezi na kufungua kwa kuuona mwezi.
Katika kuuona mwezi unatakiwa kuuona mwenye kwa kuushuhudia, ndipo unaporuhusiwa kufunga au kufungua kama utakuwa umefunga.
Unapouona mwezi uwe mdogo au mkubwa kusiwe na mabishano ya kutaka kuonyesha kuwa ulikuwa wa jana au wa juzi tuanatakiwa kuepusha mabishano ya aina hiyo.
Njia nyingine ni ya kupewa taarifa na ndugu yako Mwislamu muadilifu atakayekuthibitishia kuwa ameuona.
Iwapo Waislamu watakuwa wamefunga siku 29 na mwezi ukawa haujaonekana basi wanaambiwa waendelee kufunga siku moja zaidi ili wakamilishe siku 30.
Idd el Fitr ni sikukuu ya Kiislamu inayosherehekewa baada ya kumalizika kwa mfungo wa mwezi wa Ramadhani.
Siku hii Waislamu huitumia katika kufurahi na kumshukuru Mwenyezi Mungu sambamba na kuomba wakubaliwe funga zao kwa kuwafutia madhambi yao na hatimaye kuwafikisha kwenye heri.
Sikukuu ya Idd huhitimishwa kwa kuswaliwa swala ya Idd asubuhi sambamba na kumtukuza Allah (SW) kwa takbira na kuswaliwa rakaa mbili ikifuatiwa na khutba mbili kama zile zinazosomwa kabla ya swala ya Ijumaa. Swala hii ina takbira 12.
Takbira saba hutolewa katika rakaa ya kwanza kabla ya kusoma suratul Faatiha na takbira tano hutolewa katika rakaa ya pili nayo kabla ya kusoma kusoma suratul Faatiha.
Mahali panapofaa kuswaliwa siku ya Idd ni mahali pakubwa ingawa kuswali msikitini si dhambi ila ni bora sehemu kubwa iliyo wazi ambapo patasaidia kukusanyika waislamu wengi zaidi kutoka sehemu tofauti.
Katika hadithi ya Anas (RA) anaeleza kuwa Mtume (SAW) alikuwa haswali Idd el Fitri mpaka ahakikishe amefuturu japo tende katika idadi ya witri yaani namba zisizogawika kwa mbili na yenyewe.
Ni sunna pia kuleta takbira mara kwa mara kuanzia pale mwezi unapoandama mpaka baada ya swala ya Idd el Fitr
Mambo yanayotakiwa kufanywa siku ya Idd
Ni jambo la heri kwa Mwislamu siku ya Idd kuoga, kuvalia nguo nzuri ikiwa ni pamoja na kupaka uturi (manukato) mazuri kwa wanaume.
Pia ni siku ambayo inafaa kwa Waislamu kupika vyakula vizuri na vinywaji visivyokuwa na vilevi na kwale wafugaji na walio na uwezo ni sunna kumchinja mnyama aliyebora zaidi kuliko wengine katika mifugo yake.
Hadithi ya Hassan Asibbit (RA) inasema kwamba Mtume (SAW) ametuamrisha katika Idd mbili kuvaa vizuri zaidi kadri tuwezavyo, tupake uturi bora zaidi kuliko wote tulionao na tuchinje wanyama wenye thamani zaidi kuliko wote tulionao.
Pia ni sunna kuwatembelea wagonjwa, majirani, yatima, maskini, na watu wasiojiweza ikiwa ni pamoja na kupeana zawadi.
Mwisho wa Ramadhani isiwe mwanzo wa maasi ila iwe kipimo cha kuendeleza kufanya mema kwa waislamu na kuachana na maovu.
Tunatakiwa zakatul Fitri
Hii ni zakat inayotolewa baada ya Waislamu wanawake na wanaume kumaliza funga yao ya Ramadhani na hutolewa kabla ya swala ya Idd el Fitr.
Kwa wale wasio na uwezo watalipiwa na mawalii wao kwa mfano mume atawatolea wazazi wake kama hawana uwezo wa kujilipia na baba atalazimika kuwalipia zakatul Fitri wale wote walio chini yake iwapo kama anauwezo.
Umuhimu wa Zakatul Fitr ni faradhi iliyoambatanishwa na faradhi za mwezi wa Ramadhani, Mtume (SAW) ili kuiwezesha swaumu yako ipokelewe vizuri na Allah ni lazima kwa mwenye uwezo uitolee Zakatul Fitr.
Anayestahili kutoa Zakatul Fitri ni mwenye chakula cha kuwatosha watu wake anaoishi nao na kuwa na ziada ya kutosha usiku na ile ziada nyingine ndiyo anatakiwa kutoa zakatul Fitri.
Kiwango cha Zakatul Fitri
Kwa mujibu wa hadithi iliyotolewa na Ibn Umar (RA) anasema kwamba kiwango kinachotakiwa kutolewa Zakatul Fitr kwa kila mtu ni sai moja ya chakula (kwa sasa ni sawa na kilo mbili na nusu ya bidhaa husika) hasa kinachopendwa sana katika sehemu husika.
Kutokana na hali halisi ya kimaisha ni vyema zaidi mtoaji atoe fedha kuliko bidhaa ili kumsaidia mhusika unayemtolea kununua bidhaa ambayo anaipenda mwenyewe.
Muda unafaa kutolewa Zakatul Fitr umebainishwa kwenye hadithi iliyotolewa na Ibn Umar (RA) inasema kwamba Mtume (SAW) aliwaeleza watu kuwa watoe Zakatul Fitri kabla ya kuswali el Idd Fitr.
Kulipa Zakatul Fitri mapema kabla ya kuswali Idd au mapema zaidi ya hapo, kutamuwezesha unayempatia kufurahia Idd na Waislamu wengine.
Iwapo itatokea sababu ya msingi kama vile kusahau mpaka Idd ikaswaliwa hana budi kuitoa baada ya swala na iwapo ataacha kutoa kwa makusudi au kwa uzembe basi ajue kutoa kwake huko hakutamnufaisha kwa chochote.
Watu wanaostahili kupewa Zakatul Fitr ni maskini na wasiojiweza kupata chakula pamoja na wale walio chini ya uangalizi na wale waliochini yake ili wajisikie kufurahia Idd na waislamu wenzao wenye uwezo.
Iwapo Zakatul Fitr atapewa mtu aliye na uwezo na kuachwa asiye nao wote ambao watakuwa wametoa na kupokea Zakatul Fitr hiyo watakuwa wameidhurumu haki ya anayestahili kupewa hivyo watakuwa wamekwenda kinyume na matwakwa ya Mwenyezi Mungu.
Sikukuu ya Idd haistahili kusherehekewa kwa kupiga miziki, ngoma, kunywa vilevi na kufanya mambo yaliyokatazwa na Mwenyezi Mungu kwani utakiwa umemuasi.
Siku ya Idd si siku ya kufanya maasi kwani Mtume (SAW) anasema kuwa “Kumuasi Mwenyezi Mungu siku ya Idd ni sawa na kufanya uasi siku ya kiyama”.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment