Social Icons

PATA HABARI NA BURUDANI MBALI MBALI POPOTE ULIPO!

Friday, December 14, 2007

JAY: MUZIKI NI BIASHARA


“HAPO vipi? (hapo sawa), hapo vipi?, (hapo sawa),” ni kibwagizo kinachopatikana kwenye wimbo wa mwanamuziki wa Hip hop nchini Tanzania, Joseph Haule ‘Profesa Jay, Heavy weight Mc’, unaojulikana kama ‘Hapo sawa’.
Wimbo huu ni wimbo wa pili alioutoa msanii huyu, Julai mwaka huu katika studio za Mandugu Digital huku video ya wimbo huo ikiwa imetengenezwa na Kampuni ya Visual Lab na kuwa muendelezo wa utangulizi wa albamu yake mpya inayotarajiwa kutoka hivi karibuni ya ‘Aluta Continua’ (mapambano yanaendelea).
Katika mahojiano yaliyofanyika hivi karibuni na Tanzania Daima, msanii huyo alisema kwamba albamu hiyo ameitengeneza studio za Wow Pow Records, No End, Ketekul, Mandugu Digital, Bongo Records & MJ Production.
Aliwataja baadhi ya wasanii walioshirikishwa katika albamu hiyo kuwa ni pamoja na msanii Jose Mayanja ‘Chameleon’, ‘Farid Kubanda’ ‘Fid Q’ na msanii Nonini na makundi mawili ya Cleptomanic na Kolihombi, wote kutoka Kenya.
Wimbo wake wa kwanza alioutoa wa kutangazia albamu yake ulijulikana kama ‘Sivyo Ndivyo’ ambao alitoa Julai.
Profesa Jay ni mmoja kati ya wanaharakati wachache wa ‘Hip hop’ walioshinda katika mapambano ya muziki huo kwa kuhakikisha unaendelea kusimama.
Wapo baadhi ya wasanii ambao wamekuwa na mawazo kuwa muziki huu hauuzi sokoni na kuamua kuuacha na kuanza kuimba.
Kuhusu hilo, Jay anapingana nao kwa kusema muziki huu unauza kwa sababu ungekuwa hauuzi asingedumu katika muziki huo ambao unamsaidia kuendesha maisha yake na kujikusanyia mashabiki wa rika zote.
Akielezea historia yake kimuziki, Jay ambaye amezaliwa Desemba 29, 1975 anasema kwamba ameanza kujishughulisha na mambo ya muziki katika miaka ya 1990.
Kama ilivyo kwa wasanii walio wengi, hata Profesa Jay naye alianza kwa kupiga rapu za bure katika kumbi za starehe hadi mwaka 1994 alipojiunga na kundi la Hard Blasters Crew (HBC), wakati huo akifahamika kwa jina la ‘Niga Jay’.
Kundi hili la HBC lilijijengea heshima kubwa miongoni mwa makundi makali ya Hip hop jijini Dar es Salaam na nchini kwa ujumla.
Mwaka 1995 kundi hili lilionekana bora baada ya wimbo wao wa ‘Funga kazi’ kunyakua tuzo ya wimbo bora wa Hip Hop nchini.
Albamu ya kundi hilo iliyofahamika kwa jina la “Funga Kazi” iliingia sokoni mwaka 2000.
Albamu hii ilikuwa moja ya albamu iliyoleta mapinduzi makubwa kwenye soko la muziki wa Hip hop.
“Funga kazi, ni albamu ya Hip hop ambayo ilizoa mashabiki wa rika zote, wakiwemo watu wazima ambao walikuwa hawaupendi muziki huo kutokana na kuuona kuwa ni wa kihuni,” anasema Profesa Jay.
Alizitaja baadhi ya nyimbo zilizomo kwenye albamu hiyo ni pamoja na ‘Chemsha Bongo’, ‘Mamsapu’ na ‘Pigo la Mwaka’.
Mbali ya kupata mafanikio na kujizolea mashabiki, kundi hilo lilipatwa na pigo kubwa. Mara baada ya kutoa albamu hiyo, wasanii wake waliacha kufanya kazi pamoja na kulifanya kundi hilo kubaki historia mpaka leo.
Lakini kuhusu hilo, Jay bado ana ndoto za kufufuka kwa kundi hilo siku moja ambapo amepanga kukutana na wasanii wenzake huku akiwa na mipango ya kuwashawishi kufanya albamu nyingine kali ya pamoja.
Baada ya kila mmoja kuchukua hamsini zake hatimaye mwaka 2001 Jay aliamua kufanya kazi kama msanii wa kujitegemea na kutoka na albamu iliyojulikana kama ‘Machozi Jasho na Damu’.
Albamu hiyo ilikuwa imesheheni nyimbo kali kama ‘Ndiyo Mzee’, ambao ulifanikiwa kupata tuzo ya wimbo bora wa Hip hop nchini Tanzania. ‘Piga Makofi’ na ‘Bongo Dar es Salaam’.
Mwaka 2003 mchizi alitoa albamu yake ya pili iliyojulikana kama “Mapinduzi Halisi”.
Albamu hii ilimwongezea Jay umaarufu ambao ulimfanya apate tuzo ya Kili ya albamu bora ya Hip hop nchini Tanzania mwaka 2003.
Albamu ya ‘Mapinduzi Halisi’ ilikuwa na vibao vyake vikali kama ‘Zali la Mentali’, ‘Msinitenge’ na ‘Promota Anabeep’ ambazo zilifanikiwa kushika vilivyo na kuendelea kuwa matawi ya juu.
Jay anasema kwamba baada ya kupata mafanikio kwenye albamu yake ya pili alitoka na albamu nyingine ya tatu aliyoiachia Januari 2006, iliyokuwa ikijulikana kama ‘J.O.S.E.P.H’.
Wimbo uliokuwa umebeba jina la albamu wa ‘J.O.S.E.P.H’ ulifanikiwa kupata tuzo mbili za wimbo bora wa Bongo Fleva kwenye vituo vya BBC na Radio One.
Alizitaja nyimbo zilzokuwa kwenye albamu hiyo ni pamoja na ‘Nikusaidiaje’ aliomshirikisha Ferooz, ‘Nimeamini’ aliofanya na Judith Wambura ‘Lady Jaydee’, ‘Inatosha’ alioshirikiana na Mzee wa Kuchana, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ ‘Vuta raha’ kamshirikisha Ferooz, ‘Border kwa Border’ aliomshirikisha Nazizi wa kundi la Necessary Noise la Kenya na ‘Heka heka za star’.
Anasema kwamba mwaka 2006 albamu yake hiyo iliingia tuzo za Kili katika vinyang’anyiro huku akigombea tuzo nne ambazo ni albamu bora ya hip hop kwa albamu ‘J.O.S.E.P.H’, mwandishi bora, wimbo bora wa Hip hop kwa kupitia wimbo ‘Nikusaidieje’ na wimbo bora wa mwaka kwa kupitia wimbo ‘Nikusaidiaje’.
Katika mashindano hayo wimbo wa ‘Nikusaidiaje’ ulifanikiwa kuchukua tuzo ya kuwa wimbo bora wa mwaka, isitoshe mwaka huo wimbo huo ulichukua tuzo za Kisima, ambazo hutolewa Kenya kwa kuwa video bora nchini Tanzania

0 comments:

 

Sample text

Sample Text

PATA HABARI NA BURUDANI MBALI MBALI POPOTE ULIPO!

Sample Text