Social Icons

PATA HABARI NA BURUDANI MBALI MBALI POPOTE ULIPO!

Tuesday, December 11, 2007

MAYWEATHER AMALIZA UBISHI KWA KUMCHAPA HATTON


KUNA usemi wa Kiswahili nyoka’. Basi katika mchezo wa masumbwi usemao ‘mtoto wa nyoka ni ya kulipwa msemo huo unakamilika ama kujidhihirisha kwa bingwa wa dunia wa uzito wa Super Welter, Mmarekani Floyd Mayweather.

Mayweather ambaye ametangaza kustaafu hivi karibuni, baada ya kumpa kichapo aliyekuwa bingwa wa uzito wa Super Welter, unaotambuliwa na WBC, Oscar De La Hoya.

Alikotoka:

Floyd Mayweather, alizaliwa Februari 24 mwaka 1977 baba yake akiwa ni bondia mstaafu wa ngumi za kulipwa uzito wa Welter, nchini Marekani Floyd Mayweather Sr.

Mayweather Sr, baada ya kustaafu kuzichapa hivi sasa ni kocha wa mchezo huo nchini humo.

Floyd, baba yake mdogo, Jeff Mayweather pia alikuwa bondia bingwa wa uzito wa juu unaotambuliwa na IBO, wakati baba yake mwingine, Roger Mayweather, naye aliwahi kutwaa ubingwa wa dunia mara mbili, kabla ya kuja kuwa kocha wake.

Floyd alianza kufuata mkondo wa baba zake, alipoanza kung’ara katika ngumi za ridhaa, ambako alicheza takriban mapambano 84.

Katika mapambano hayo ya ridhaa, Floyd alitwaa ubingwa wa taifa nchini Marekani ‘National Golden Gloves’ kwa miaka mitatu mfululizo kuanzia 1993, hadi 1996.

Floyd kutokana na ugumu wa kupigika, aliokuwa nao, wenzake walimpachika jina la utani ‘Bitch Boy’ kutoka na usugu wa uso wake, uliokuwa hauchubuki wala kuchanika akiwa ulingoni.

Alikuwa ni mjanja wa kukwepa makonde kama ilivyokuwa enzi za baba yake, Floyd Mayweather Sr na baba yake mdogo, Roger Mayweather, ambao ndio walikuwa makocha wake.

Bondia huyo alitwaa medali ya shaba katika mashindano ya Olimpiki ya Atlanta mwaka 1996, katika uzito wa feather, kilo 57.

Akiwa kati ya mabondia bora 31 katika mashindano ya wazi, Floyd alikuwa na rekodi ya kushinda mapambano 10 na kupoteza moja tu, alilopoteza kwa Bakhtiyar Tileganov wa Kazakhstan, baada ya mwamuzi kusimamisha pambano katika raundi ya pili.

Katika mzunguko wa pili wa mashindano hayo ya wazi, Floyd alimtoa kwa pointi 16-3 Artur Gevorgyan wa Marekani, huku robo fainali akimchapa Lorenzo Aragon kutoka Cuba kwa pointi 47-11 wakati nusu fainali alimgaragaza, Serafim Todorov wa Bulgaria.

Alichukuliwa na baba yake mdogo, Roger Mayweather, kumfundisha baada ya baba yake mzazi, Floyd Mayweather Sr. kuhukumiwa kwenda jela baada ya kukutwa na dawa za kulevya ndani ya gari lake mwaka 1993.

Floyd alipoongeza uzito na kucheza Super Welter kutoka Welter, pambano lake la kwanza alicheza na mgeni mwenzake katika uzito huo Roberto Apodaca, Oktoba 11, 1996.

Baada ya Mayweather Sr. kutoka jela alimchukua tena mwanawe na kumuwezesha kumshinda kwa KO, Sam Girard.

Mwishoni mwa miaka 1996, Floyd Mayweather alikuwa mwiba, kwa kutoa vipigo vya TKO au KO kwa wapinzani wake na pambano lake kubwa lilikuwa kati yake na bingwa wa zamani wa IBO, Tony Pep lililofanyika Juni 14, 1998.

Mwaka 1998, Floyd Mayweather alishinda ubingwa wa dunia Super Feather unaotambuliwa na WBC.

Januari 20, 2001, alimwadhibu kwa pointi Diego Corrales katika pambano la raundi kumi.

Floyd Mayweather alikumbana na kisiki kwa mara ya kwanza, Mei 26, 2001 baada ya kuchapwa na bingwa aliyekuwa akitambuliwa na IBF, Carlos 'Famoso' Hernández, katika raundi ya sita hadi kuteguka mkono wake.

Pambano lake la mwisho katika uzito wa super feather, lilikuwa kati yake na bingwa wa uzito huo, Jesús Chávez aliyemchapa katika raundi ya tisa.

Mwaka 2002, Mayweather aliingia katika uzani wa light, kupigana mapambano manne pekee ya uzito huo.

Kati ya mapambano hayo alishinda taji la WBC, dhidi ya José Luis Castillo, pambano lililoonekana kumwelemea, na kusababisha mashabiki kumtabiria kupoteza kabla ya kuwashangaza kwa kugeuza kibao na kumchapa, hivyo kutwaa taji hilo.

Pambano lake jingine lilikuwa Novemba mosi, 2003 nyumbani kwao, Grand Rapids, Michigan alipomchapa Phillip Ndou, wa Afrika Kusini kwa KO.

Floyd Mayweather aliongeza uzito tena na kuingia super light na kukutana na De Marcus Corley ambaye alimchakaza dakika ya kwanza raundi ya nne.

Januari 22, 2005, alimshinda Henry Bruseles wa Puerto Rico katika pambano la kuwania ubingwa wa WBC, super light, katika raundi ya saba.

Baada ya hapo alikutana na bondia Gatti, na kumchapa ambako baada ya mwezi mmoja baadaye, alikamatwa na kufunguliwa mashitaka na mpenzi wake wa zamani, Josie Harris, aliyedai kushambuliwa na bondia huyo kwa mateke nje kidogo ya Las Vegas katika ukumbi wa muziki mwaka 2003.

Novemba 19, 2005, alihamia uzito wa Welter na kwa kuanza alicheza na bondia, Sharmba Mitchell na kumdondosha katika raundi ya tatu.

Aprili 8, 2006, Floyd Mayweather aliomba pambano na Zab Judah akiwa na nia ya kujilimbikizia mataji ya dunia ya IBF na IBO uzito wa Welter.

Katika pambano hilo, kulikuwa na upinzani wa hali ya juu, ambao ulikuja kuwajumuisha makocha na wanafamilia wa mabondia hao katika vurugu zilizotokea ulingoni.

Katika raundi ya tano ya pambano hilo, Floyd alimtoa damu Judah na katika raundi ya kumi zikiwa zimebaki sekunde tano, Judah alimtandika Floyd Mayweather konde la kushoto, na kusabaisha kocha wake, ambaye ni baba yake mdogo, Roger Mayweather kuingia ndani ya ulingo na kumuonya Judah kuacha kumchezea rafu bondia wake.

Kutokana na tukio hilo, baba yake Zad, Yoel Judah ambaye pia naye ni kocha wa mwanawe naye aliingia ndani ya ulingo katika sekeseke hilo.

Floyd alibaki peke yake kwenye kona yake, wakati kona nyingine walionekana Yoel, Zab na Roger na kisha mashabiki wengine nao waliingia ulingoni kabla ya polisi kusaidia kuwaondoa.

Hatimaye Roger, alitoka nje na ulingo na pambano liliendelea na Floyd kuibuka na ushindi wa pointi 188-82.

Siku tano baada ya pambano hilo, Tume ya ngumi ya Nevada ilimpiga faini Roger Mayweather dola 200,000 na kufungiwa mwaka mmoja.

Baada ya hapo Floyd Mayweather aliitema ofa ya dola milioni 8 kucheza na Antonio Margarito na badala yake alikuwa akimtaka bingwa wa super light, Oscar de la Hoya.

Baada ya kulitema pambano hilo, aliandaliwa pambano na bingwa mwingine wa WBC uzito wa Welter, Carlos Baldomir, Novemba 4, 2006 lililochezwa Las Vegas, na kuibuka mshindi na kujizolea kitita cha dola milioni 8 huku Baldomir akiondoka na dola milioni 1.6.

Kustaafu:

Akiwa na miaka 29 tu mwaka jana, Mayweather aliviita vyombo vya habari na kuvieleza kuwa, anatarajia kustafu mara baada ya kucheza mchezo wake wa mwisho, ambao kwake atauona kama fainali.

Kwani alitamani kukutana na bondia bora wa wakati huo, ambaye angepambana naye katika mechi yake hiyo ya mwisho, maneno ambayo watu wengi hawakuamini, wakijua danganya toto, kutokana na umri wake huo. Floyd Mayweather aliongeza kuwa hakukuwa na bondia mwingine aliye bora isipokuwa Oscar De La Hoya.

Hatimaye Mei 5 mwaka huu, pambano kati yake na bingwa wa WBC, Light Middle, De La Hoya liliwadia ambako ilimlazimu Floyd kuongeza uzito kutoka pauni 147 hadi 154.

“Nilichokuwa nikikisubiri kimeshatimia, mtoto, mtoto,” alisema De La Hoya.

Nilifikiria hili, kinachonishangaza ni kuwa mtoto huyu hanisisimui, yaani nalichukulia pambano hili kama la kawaida kwa sababu kila wakati nilihitaji kumpata mpambanaji bora.

Na Floyd amejitokeza na kujiona ni bora ulimwenguni, nitamuonyesha, na sidhani kama pambano hili litakuwa la mwisho kwake, naamini baada ya kipigo nitakachompa ataendelea kupambana,” alitamba De La Hoya.

Kinyume chake, Mayweather, alishinda pambano hilo na kumfanya kuweka rekodi ya kushinda mapambano 38-0. Katika pambano hilo alishinda kwa 116-112, 115-113, huku jaji wa mwisho akimpa Mayweather 115-113.

Baada ya ushindi huo hatimaye Mayweather, alitangaza rasmi kustaafu masumbwi baada ya kunyakua taji hilo la super welter linalotambuliwa na WBC, Mei 6, 2007.

Huyo ndiye Floyd Mayweather, bondia aliyerithi vipaji vya wazazi wake, ukiwamo utukutu, ambaye amestaafu kiaina na kuacha butwaa kwa mashabiki wa masumbwi duniani.

Makala hii imeandaliwa na Shabani Matutu kwa msaada wa mashirika ya habari. Anapatikana kwa barua pepe: kimyamatutu@yahoo.com

0 comments:

 

Sample text

Sample Text

PATA HABARI NA BURUDANI MBALI MBALI POPOTE ULIPO!

Sample Text