Social Icons

PATA HABARI NA BURUDANI MBALI MBALI POPOTE ULIPO!

Friday, August 14, 2009

choka mbaya




Mchezeshaji muziki afahamikaye kwa jina la “DJ” ni moja kati ya nguzo za muziki wa Hip hop, hivyo ni vigumu kwa msanii anayefanya muziki wa mahadhi hayo asiwe na “Dj’.
Kwa msanii anayefanya hip hop kukosa kufanya na Dj ni sawa na kupika chakula pasipo kuwa na viungo.
Hivyo basi, msanii Joseph Haule ‘Profesa Jay’ aliamua kumtumia Hugoline Martin Mtambachuo, maarufu kama (Dj Choka), kuwa Dj wake.
Kwa wale mashabiki wa Profesa Jay ni vigumu sana kuhudhuria matamasha ya ndani na nje ya nchi ya msanii Profesa Jay na kukosa kumuona Dj Choka ambaye amekuwa akimtumia kwenye kazi zake.
Wawili hawa ni vigumu kuwatenganisha kutokana na kushabihiana katika kazi pindi wanapokuwa wanawapagawisha mashabiki.
Dj huyo amekuwa akitumiwa na Profesa Jay amekuwa akimtumia katika maonyesho yake yote ambayo anayofanya sehemu mbalimbali.
Historia fupi ya Dj huyu ni tofauti na madj wengine ambao wengi wao kabla ya kujikita huko huanzia katika kufanya kazi ya usanii na baadaye hugeukia katika kazi ya uchezeshaji muziki lakini Choka alikwenda moja kwa moja katika kazi hiyo.
Akizungumza na Tanzania Daima Wikiendi mwanzoni mwa wiki Choka anasema “Sikuwahi kujihusisha na usanii kabla ya kuwa Dj, ila nilianza moja kwa moja fani ya uchezeshaji muziki kazi ninayoimudu hadi sasa huku nikiwa nimefanikiwa nikiwa katika fani hii,” anasema.
Watu wengi ambao wanamfahamu DJ Choka wamekuwa wakidhani kwamba huenda yeye na msanii Profesa Jay ni ndugu jambo ambalo halina ukweli huku akisema wao ni marafiki.
“Kwangu Jay ni rafiki na amenifundisha mambo mengi hususani yahusuyo muziki, na kutokana na kukaa naye kwa muda mrefu imenisaidia kumuona kama kaka yangu,” alibainisha.
Kitu cha kushangaza hapa pamoja na umaarufu wake wote Choka hajawahi kufanya kazi nyingine nje ya kufanya kazi na Profesa Jay.
“Huwezi kuamini Bro, sijawahi kufanya kazi na mtu mwingine yeyote mbali na Profesa Jay,” anasema Dj huyo mkali wa kuchezea meza.
Akielezea historia ya kazi yake hiyo anabainisha kwa kusema aliianza mwaka 2004 mara tu baada ya kuhitimu elimu yake ya sekondari.
Choka anasema kwamba hiyo ilikuwa njozi yake tangu alipokuwa kinda. Anasema alikuwa akijihusisha na muziki tangu akiwa nyumbani kwao ambako kulikuwa na muziki mkubwa wa baba yake.
“Kila lilipokuwa likitokea tukio la kuhitaji kupigwa muziki nilikuwa nachaguliwa na mzee kuwa Dj hapo ndipo nilipoanza kupata uzoefu na kuchangia kupenda kuwa Dj,” anasema Choka.
Pamoja na kujikita katika fani hiyo mapema lakini msisimko zaidi aliupata kutoka kwa madj kama vile Dj Funk Master Flex, Dj Khalid na hapa nchini alivutiwa na John Dilinga ‘Matlou’ ambaye amekuwa akinipa moyo na kunifanya mpaka sasa kuwa juu.
Licha ya fani hii kusomewa na baadhi ya wachezeshaji muziki lakini Choka anasema, “Sijawahi kusomea fani hii ya muziki katika chuo chochote cha ndani au nje ya nchi bali, kinachonisaidia kuimudu kazi hii ni utundu wangu.”
Kiwango cha elimu cha Dj Choka ni cha kidato cha nne. Baada ya hapo hakuweza kuendelea ila amesema ana mpango wa kujiendeleza zaidi kielimu.
Aliwataja baadhi ya madj wa hapa nyumbani anaozikubali kazi zao katika kizazi hiki kuwa ni Dj PQ, Dj Steve B, Dj Kim na Dj Ziro.
“Nawazimia Madj hawa kutokana na jinsi wavyozimudu kazi zao ile kinoma kwa kifupi naukubali muziki wao pindi wawapo kazini huwa hawarembi,” alisema.
Kuhusu maslahi ya kazi hiyo hapa nyumbani, Choka anasema inalipa hasa kwa wale wanaojichanganya na kufahamika na watu wengi.
“Kazi hii inalipa kwa madj wanaojichanganya na watu wengi na kutangaza jina lao hivyo huwawia rahisi kupata dili kibao za kufanya.” Alibainisha na kuongeza, “Kwa wale wanaokuwa hawajichanganyi lazima wataona kazi hii ni ngumu na hailipi.”
Akielezea malengo yake katika siku za baadaye katika muziki huu, Dj Choka alisema anafikiria kujituma kwa kiasi kikubwa na kuufikisha mbali hasa kimataifa.
“Na kwa mawazo hayo naamini nitajitahidi kwa uwezo wangu na ndoto zangu naamini zitakuwa kweli,” alisema.
Nje ya kazi yake ya udj, Choka anajishughulisha na kazi ya kupasha habari kwa kutumia njia ya mtandao.
“Kazi nyingine ninayoshughulika nayo ni kusambaza habari kwa kupitia mtandao wangu wa Blogspot inayokwenda kwa jina http://www.djchoka.blogspot.com/,” alisema.

0 comments:

 

Sample text

Sample Text

PATA HABARI NA BURUDANI MBALI MBALI POPOTE ULIPO!

Sample Text