Social Icons

PATA HABARI NA BURUDANI MBALI MBALI POPOTE ULIPO!

Friday, September 11, 2009

HASHEEM THABEET
Mtanzania aliyeula Ligi Kuu ya kikapu Marekani NBA

BAADA ya uamuzi wake wa kuamua kuacha kumaliza masomo yake katika Chuo Kikuu cha Connecticut hatimaye mchezaji wa Kikapu kutoka nchini Tanzania, Hasheem Thabeet Manka amepata bahati ya kusajiliwa na timu inayoshiriki Ligi kuu ya mchezo wa kikapu ya nchini Marekani (NBA) ya Memphis Grizzlies.

Mtanzania Hasheem Thabeet atakuwa ametufanya watanzania kutembea kifua mbele mara baada ya kutangazwa kucheza katika ligi ya mpira wa kikapu ya NBA.

Tanzania imepata bahati ya kuwa na mchezaji wa kimataifa wa kulipwa Hasheem Thabeet ambaye amechaguliwa kujiunga na timu ya Memphis Grizzlies yenye makao yake makuu huko Memphis katika jimbo la Tennessee nchini Marekani.

Hasheem anakuwa ameandika historia ya kuwa mtanzania wa kwanza kufikia hatua hiyo, ambayo kama watanzania na wapenda michezo tuna kila sababu ya kufurahia mafanikio yake na kumtakia kila la kheri.

Tanzania kwa sasa wanajivuna kwa kuwa na balozi katika ulimwengu wa michezo ya kikapu kwa kuwa na mchezaji wa kimataifa.

Kutokana na ushindi huo wa Hasheem, shirikisho la mpira wa kikapu tanzania (TBF), limetoa taarifa ya kupongeza uteuzi wake kwa kuwa mshindi wa pili kati ya wachezaji thelathini waliokuwa wakiwania kucheza NBA.

Katika taarifa yao tbf ilisema kuwa baada ya kupata taarifa ya kutangazwa kwa Hashem na Kamishna Mkuu wa NBA, David Stern kwao ilikuwa faraja.

Katika taarifa hiyo TBF iliwapongeza waliofanikisha kumuwezesha Thabeet, kufikia hatua hiyo ambao ni Chama Cha Mpira wa kikapu cha Mkoa wa Dar es Salaam, Mama Hasheem na ndugu zake pamoja na ubalozi wa Marekani kwa kutoa taarifa za mara kwa mara na kufuatilia maendeleo yake.

Hasheem Thabeet aliyeteuliwa kukipiga Memphis Grizzlies, akiwa amezaliwa Februari 16, 1987, jijini Dar es Salaam, Tanzania.

Kijana huyu anasifa kubwa ya urefu unaotisha kwani ana urefu wa futi 7 inchi 2.5, akiwa na uzito wa kilogramu 119.

Mchezaji huyo amesoma shule ya sekondari ya High school Cypress Christian School, Houston, Texas, Marekani.

Baada ya kumaliza masomo hayo alijiunga na Chuo Kikuu cha Connecticut kinachopika vipaji vya wachezaji wa mpira wa kikapu.

Kabla ya kuchaguliwa kuwa mchezaji wa Kimataifa Thabeet amewahi kupewa tuzo ya NABC kwa kuwa mzuiaji bora wa mwaka 2008.

Pia amewahi kupata tuzo ya kuwa Mchezaji bora wa Ukanda wa Mashariki wa mwaka tuzo aliyoipata mwaka huu.

Wakati Thabeet alipokuwa amekuja nchini Tanzania aliwahi kusema kuwa mwanzo alikuwa akiona urefu wake kama karaha.

Alisema kuwa aliona umbo lake ni bora kwa mara ya kwanza alipoanza kucheza katika shule ya sekondari ya Makongo iliyopo jijini Dar es Salaam, Tanzania na anamkumbuka mtu aliyemsaidia kuanza kucheza mcheza huo ni mchezaji maarufu wa nchini Tanzania, Henri Mwinuka.

anasema anamkumbuka sana kutokana na kumwambia kwa mara ya kwanza kuanza kucheza huku akimpatia viatu (raba) za kuchezea na hapo alifanikiwa kucheza mchezo huo kwa mara ya kwanza .

Alijikuta akiupenda mchezo huo hli iliyomfanya ajikute akipenda kucheza hata pindi anapokuwa mtaani.

Hali hiyo ilimsaidia kupewa namba katika timu ya shule yao ambayo ilikuwa ikishiriki katika Mashindano ya Michezo ya Afrika Mashariki iliyokuwa ikichezwa Nairobi, Kenya.

Wakati akiwa katika mashindano hayo alipata bahati ya kukutana na wakala aliyemuahidi kumsaidia ili akasome bure katika shule za kikapu za nchini Marekani.

Safari hiyo ndiyo ilikuwa mwanzo wa mafanikio yake katika mchezo huo wa kikapu.

Baada ya baba yake mzazi kufariki Thabeet aliondoa jina lake la mwisho na kuliweka kati kama kumbukumbu ya baba yake.

Kabla ya kijana huyo kujiunga na shule ya UConn, alijiunga na shule ya kikristo ya Cypress Christian School ya Houston, Texas ambako nako alikuwa akicheza mpira wa kikapu na kufanikiwa kupiga jumla ya vikapu 16.

Akiwa anapata wastani wa pointi 6.2 kwa kila mchezo, Desemba 3, 2006, Thabeet alijiunga na UConn akiwa na rekodi ya kupiga ‘blocks’ 10.

Kutokana na kuonyesha uwezo mkubwa na kujua kilichompeleka mwaka 2007, Thabeet alitajwa kuwa mchezaji mkubwa wa timu za Mashariki akiwa pamoja na mchezaji mwenzake Jerome Dyson.
Kila miaka ilivyokuwa inakwenda Thabeet alikuwa akiongeza ubora wake na kufanikiwa kujikusanyia pointi 10.5 kwa kila mechi kupiga mikuno 7.9.

Kutokana na kupiga mpira kwa makini Thabeet alitajwa kama mchezaji bora wa mwaka kwa upande wa Mashariki.

Akiwa mchezaji wa Timu ya Chuo Kikuu cha UConn, Thabeet aliongeza uwezo wake wa kiuchezaji aliweza kujiongezea wastani wa pointi 13.6 na akipiga mikuno 10.8

Januari 31, 2009, alikuwa amejihesabia jumla ya pointi 15, akiwa amepiga mikuno 11 na ‘blocks’ 10.

Hadi mwisho wa msimu alikuwa amefikisha jumla ya ‘blocks’ 152 akiwa anajua namna ya kufunga.

Thabeet aliishangaza dunia kwa kujikusanyia jumla ya pointi 1,000 Machi 26, 2009. alikuwa mchezaji bora wa tatu wa UConn wa msimu huo nyuma ya wachezaji Jerome Dyson na AJ Price.
Thabeet amekuwa akiisaidia UConn kuongoza katika fainali za kwanza za nne tangu kuingia kwake mwaka 2004.

Thabeet ambaye ni kijana wa marehemu Thabit Manka na mama yake Rukia Manka anayeishi Dar es Salaam.

Kijana huyu amezaliwa katika familia yenye watoto watatu akiwamo dada yake anayeitwa Sham, Kaka yake Ahkbar.

Juni 15, 2009, alishiriki katika maonyesho ya ‘Jim Rome Is Burning’ pamoja na kwamba yeye ni muislamu.

Kabla ya kujiunga katika mashindano ya NBA alianza kung’aa katika ligi ya NCAA inayohusisha vyuo, alifikia uamuzi huo baada ya kuzungumza na familia yake, marafiki pamoja na kocha wake Jim Calhoun.

Akizungumzia kuhusu uamuzi wake alisema “ Baada ya kutumia muda kuzungumza na familia yangu, marafiki na kocha Calhoun, nimeamua kuachana na mwaka wangu wa mwisho wa masomo pale Chuo Kikuu cha UConn na kuingiza jina langu kwenye mchakato wa wale wanaowania kucheza NBA kwa mwaka 2009,” alisema Thabeet na kuongeza kuwa amepata uzoefu mkubwa akiwa na Connecticut na hana maneno ya shukrani ya kuwapa makocha wake na wachezaji wenzake.

Amesema sasa anataka kupata changamoto mpya ya kucheza kikapu cha kulipwa kwani kwa muda aliokaa UConn ameandaliwa vema kwa ajili ya kupata mafanikio baadaye.

Pia aliwashukuru mashabiki wake wote ambao walikuwa wakimfuatilia kwenye uchezaji wake tokea akiwa Tanzania na ana matumaini wataendelea kumuunga mkono akiwa katika ngazi ya mchezaji wa kulipwa.

Thabeet alichaguliwa kwenye kikosi cha kwanza cha timu ya ‘All-American’ cha mwaka 2008-09.

Thabeet alikuwa mchezaji wa 11 kutoka UConn kutangaza kuingia kwenye mchakato wa kucheza ligi ya NBA na kati ya hao tisa waliingizwa kwenye raundi ya kwanza na nane kati ya hao waliingizwa kwenye hatua ya bahati nasibu ya raundi hiyo ya kwanza na hatimaye yeye amefanikiwa kutajwa kujiunga rasmi.

Hatua ya kuchaguliwa kucheza NBA imepokelewa vema na Rais Jakaya Kikwete, aliyezungumza kutoka Riyadh nchini Saudi Arabia kwa kumpongeza Thabeet.

Kikwete alisema amefurahishwa na hatua hiyo na kwamba heshima ya Tanzania itaongezeka na NBA ni fursa nzuri ya kuitangaza nchi na itachochea wachezaji wengine nchini kuongeza juhudi.

0 comments:

 

Sample text

Sample Text

PATA HABARI NA BURUDANI MBALI MBALI POPOTE ULIPO!

Sample Text