
Muungano wa Bongo Movie, Taff wote mmesadiki..
KWA wale ndugu zangu katika imani tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kuumaliza mwezi mtukufu salama salimini na kutuwezesha kuwa na siha njema na kutukutanisha tena siku ya leo kutazama yaliyojiri katika tasnia ya filamu kwenye safu hii ya Vunjavunja.
Kati ya habari ambazo nimepata kuzisoma katika kipindi hiki hasa zinazohusiana na tasnia ya filamu za hapa nyumbani ni iliyokuwa ikizungumzia ndoa iliyofungwa kati ya mahasimu wawili wa Bongo Movie na Shirikisho la Filamu nchini (TAFF) ambao nimepata kuwaandika wikimbili zilizopita nikielezea utengano wao kuwa kikwazo katika kuwasaidia kwenye vita yao na wezi wa kazi zao.
Hivyo baada ya kusoma habari iliyokuwa ikielezea kuhusu kuungana kwao kwa ajili ya kuhakikisha wanapunguza na kama si kuondoa kabisa wezi wa kazi zao.
Katika habari hiyo ilionesha kwamba muungano huo ulihusisha wadau mbalimbali wanaojihusisha kwa namna moja au nyingine katika tasnia hiyo ikiwamo Makampuni ya usambazaji wa kazi hizo, TAFF, Bongo Movie, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), wameungana ili kukabiliana na wezi wa kazi za wasanii ili kukomesha vitendo hivyo.
Hawa walikutana kwenye mkutano uliofanyika mwishoni hapoa jijini Dar es Salaam kwa kuhusisha viongozi wa pande zote mbili ambako kwa pamoja walisema umefika wakati wa kukomesha tatizo hilo ambalo limekuwa likiwakatisha tamaa wadau wa sanaa nchini.
Akizungumza katika mkutano huo, Rais wa TAFF Simon Mwakifwamba, alisema wameona njia ya kukomesha hilo ni kufanya kazi kwa pamoja katika kulishughulikia tatizo hilo huku akishangazwa na kukithiri kwa wizi wakati ipo sheria ya udhibiti wa jambo hilo.
Alitpoa wito kwa serikali kutekeleza ahadi yake ya kuwasaidia wasanii kupambana na wezi hao ambao alidai wapo kila pembe ya nchi wakifanya uhalifu wao kwa kujiamini kana kwamba wapo juu ya sheria na hakuna anayeweza kuwakamata.
Aliongeza kwa kusema kwamba angalau anaona kazi za wasanii zitasimamiwa vizuri na kuwezesha kuliongezea taifa pato kubwa kwa vile soko la sanaa kwa sasa limekuwa na mafanikio na lina mafanikio makubwa ingawa bado inawanufaisha wachache.
Naye Mwenyekiti wa Bongo Movie, Jacob Steven 'JB' alisema sanaa inaweza kuchangia pato la taifa kama wizi wa kazi za wasanii utakamoshwa vilivyo.
Katika mkutano huo Meneja wa Usimamizi wa TRA, Msafiri Ndimbo alisema mamlaka hiyo imejipanga kudhibiti wizi wa kazi hizo kuanzia Januari mwakani baada ya serikali kupitia Bunge lake kukubaliana kuweka mikakati ya kupamba na suala hilo.
Wasambazaji waliohudhuria katika mkutano huo wa Steps Entertainment, PAPAZI, Msama Promotions wakajinasibu kwa kusema kuwa wamekuwa wakishirikiana na TRA, Bongo Movie na TAFF ili kulinda maslahi ya wasanii ambao wamenyonywa kwa muda mrefu.
Ningependa kumalizia vunja vunja ya leo kwa kuwapongeza wale waliotafuta suluhu hiyo kwa manufaa ya wasanii na taifa kwa ujumla na nautakia muun gano wao mafanikio zaidi.
Kama waswahili wanavyosema katika ‘msafara wa mamba, kenge nao wamo’ wasijikute wanatafunwa na msemo huu jambo ambalo siliombei kabisa liwatokee watanzania hawa wenye nia hiyo njema.
Wasiwasi ninao upata katika muungano huu ambao nauona kwa jicho la tatu kama unafiki, kwani fikra zangu nilikuwa nikiamini kwamba umoja wa wasanii utakuwa imara iwapo kama kutavunjwa makundi madogomadogo yaliyomo ndani ya tasnia hiyo.
Naamini kwamba hakuna jambo lolote lililo na adui likapata kufanikiwa kwa kupitia muungano wa makunbdi ambayo bado viongozi wake hawataki na hawana mpango wa kuyavunja hivyo naamini hata adui zao wataendelea kutumia upenyo huo.
Kwa ushauri wangu wa bure ningependa kuwapatia kundi la Bongo Movie kama lina nia thabiti ya kutaka kuunganisha nguvu na TAFF ingekuwa bora walivunje na kuingia moja kwa moja na kuanzisha mapambano kwa kauli moja na si kauli moja katika makundi mawili.
Siamini kama kweli wasambazaji huwa wanapenda kuona wasanii wale ambao wamekuwa wakiwalalamikia kila uchao kuwaingiza mikataba ya kilaghai ya kununua hakimiliki zao (nikimaanisha kuuziwa master), wakawa mstari wa mbele kuhakikisha wanapata haki ile wanayoililia kwa muda sasa.
Nawaasa wasanii waachane na makundi kwani hata Tanzania mwanzo wa uhuru ilikuwa na vyama vingi lakini tulipopata uhuru vyote vilivunjwa na kuwa kimoja hasa ndiyo ikawa silaha ya kufikia malengo yao na wale wanaopinga muungano wa kuvunja Bongo Movie na kutumia mwamvuli wa TAFF naamini hao ndio watakuwa kenge wenyewe.
Namaliza kwa kusema muungano wa Bongo Movie, Taff safi lakini wote wanaohusika wamesadiki au wengine wametumwa kama mamluki.
0 comments:
Post a Comment