BAGHDAD, Iraq
MASHAMBULIZI
kadhaa ya mabomu yametokea nchini hapa na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 50
na wengine kujeruhiwa.
Polisi nchini
humo wanasema kuwa mashambulizi hayo yalilenga ngome za Waislamu wa madhehebu
ya Kishia wakati walipokuwa katika harakati za kwenda kazini huku wengine
wakijishughulisha na mambo mengine.
Kiwango cha
machafuko kimeongezeka nchini Iraq katika siku za hivi karibuni kutokana na
uhasama unaoendelea kukithiri kati ya Waislamu wa Kishia na wale wa Wasunni.
Polisi
wanasema kuwa zaidi ya milipuko 10 ya mabomu ilitokea wiki iliyopita katika
maeneo mbalimbali ikiwemo Wilaya ya Jisr Diyala mjini Baghdad na mji wa Sadr.
Hadi sasa
hakuna kundi lililojitokeza kusema kujihusisha na mashambulizi hayo lakini
polisi wanashuku kuwa yalitekelezwa na wapiganaji wa Kisunni.
Waislamu wa
Kisunni wanasema kuwa wanatengwa na serikali ya Waziri Mkuu Nouri Maliki ambaye
anaongoza serikali ya Kishia tuhma ambazo serikali inapinga na kusema kuwa
wapiganaji hao wanatumiwa na makundi ya kigaidi.
Tangu kuanza
kwa mwaka huu, zaidi ya watu 4,000 wameuawa na wengine 10,000 kujeruhiwa
kutokana na mashambulizi hayo ya mabomu.
Takwimu za
Umoja wa Mataifa zinaonesha kuwa Julai ilikuwa mbaya kwa raia wa Iraq baada ya
watu 1,057 kupoteza maisha yao wengi wao wakiwa mjini Baghdad.
Operesheni ya kijeshi yanukia Syria bila UN
DAMASCUS, Syria
UWEZEKANO wa Umoja wa Mataifa (UN), kuidhinisha mashambulizi
dhidi ya Syria ni mdogo sana, lakini tayari Marekani na washirika wake
wanafanya maandalizi ya mashambulizi kupitia dhana ya uwajibikaji wa kimaadili.
Wiki moja baada kutokea shambulio linalodaiwa kuwa la
kemikali kufanywa nchini Syria, mataifa kadhaa yameanza kupeleka vikosi
kujiandaa na mashambulizi dhidi ya serikali ya Rais Al Assad.
Mwanzoni mwa wiki Waziri wa mambo ya kigeni wa Uingereza
William Hague alielezea uhakika kwamba gesi ya sumu ilitumiwa na vikosi vitiifu
kwa rais Assad.
Tukio hilo linaendelea wakati uchunguzi wa karibu juu ya
shambulio hilo unaendelea kufanywa na wakaguzi wa Umoja wa Mataifa.
Vikosi hivyo vinasubiri kauli ya wachunguzi wa Umoja wa
Mataifa ambao iwapo watabainisha kuwa gesi hii ya sumu ilitumiwa na upande wa
serikali, hakuna kitakachozuia mashambulizi ya kijeshi.
Muungano wa hiari
Kulingana na muktadha wa sheria hata hivyo, mashambulizi
hayo yatakuwa yanakiuka sheria za kimataifa, kwa kuwa uhalali wake unaweza
kutokana na baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, ambako China na Urusi
zinaweza kuzuia mpango huo kwa kutumia kura zao za turufu.
Kwa nchi hizo mbili, uingiliaji kijeshi kutoka mataifa ya
nje siyo njia ya kuleta suluhu.
Kama litafanyika shambulizi la kijeshi, haitakuwa mara ya
kwanza kwa Marekani kuchukua hatua kama hiyo pasipo idhini ya Umoja wa Mataifa
kwani hata wakati wa utawala wa Rais wa zamani wa Marekani George W. Bush,
kupitia kile alichokiita muungano wa hiari, aliyaongoza mataifa kadhaa kuivamia
Iraq mwaka 2003, kwa madai ya kuikomboa kutoka mikononi mwa Saddam Hussein.
Kabla ya uvamizi huo, Marekani ilijaribu kupitisha hoja yake
ndani ya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, kuonyesha kuwa kulikuwepo
silaha za maangamizi nchini Iraq, ambapo waziri wa ulinzi wa wakati huo Collin
Powell aliwasilisha ushahidi wa madai hayo katika baraza.
Hata hivyo, kulikuwa na mashaka makubwa kwa upande wa
Ufaransa, Urusi na Ujerumani kuhusiana na ushahidi huo, na waziri wa mambo ya
kigeni wa Ujerumani Joschker Fischer, alieleza bayana kuwa hakuridhika na
ushahidi wa Marekani.
Na kwa hakika mashaka yake yalikuja kutimia, baada ya
kubainika kwamba ushahidi uliyowasilishwa katika umoja wa mataifa ulikuwa wa
kughushi na Collin Powell alikiri kufanya makosa na kujiondoa katika ulingo wa
siasa.
Waziri mkuu wa Uingereza David Cameron anakutana na maofisa
wa juu wa serikalini na jeshi kujadili mikakati.
0 comments:
Post a Comment