Social Icons

PATA HABARI NA BURUDANI MBALI MBALI POPOTE ULIPO!

Friday, August 30, 2013

Diamond amzawadia gari Muhidini Gurumo



Dimaond kushoto akimkabidhi Muhidini Gurumo gari alilomnunulia.

MKALI wa Bongo Flava nchini, Naseeb Abdul, juzi alifanya uzinduzi wa video ya kibao chake kiitwacho My Number One, iliyokwenda sambamba na kumkabidhi zawadi ya gari la kutembelea aina ya Toyota Fun Cargo, mkongwe wa dansi aliyestaafu hivi karibuni, Muhidini Maalim Gurumo.
Uzinduzi na makabidhiano hayo vilifanyika, kwenye Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam, ambapo Diamond Platinum alikiri kutambua na kuthamini mchango wa wanamuziki waliomtangulia, akiwamo Gurumo ndio maana akampa zawadi hiyo.
Gurumo aliyekuwa mwanamuziki wa bendi ya Msondo Ngoma wiki iliyopita alitangaza kustaafu muziki akiwa na umri wa miaka 73, ambapo amekuwa ndani ya tasnia hiyo kwa miaka 53 na kusema anastaafu kutokana na umri, ingawa alikiri kumaliza zama zake akiwa hana hata baiskeli.
Ndipo Diamond alipofanya uzinduzi na kukabidhi gari, ambapo baada ya kuzindua na kutambulisha rasmi video yake ya ‘My Number One’, mkali huyo alitumia fursa hiyo kumkabidhi Gurumo ambaye alikuwa mmoja wa waalikwa.
Akizungumza baada ya kukabidhi gari hiyo yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni saba, Diamond alisema kuwa anathamini mchango wa wanamuziki waliotangulia, kwa kuwa wao ndio chagizo la wasanii wachanga na sanaa yao izidi kukua.
"Katika safari yangu ya kimuziki nilikuwa nikitamani sana kuwa na jina na kutunga nyimbo kama baba yangu Gurumo. Nampenda na wanamuziki wengine wote wa Tanzania, maana bila wao sisi wa kizazi kipya tusingejua njia za kupita ili kufikia malengo,” alisema Diamond.
Baada ya kukabidhiwa funguo na kuambiwa dhamira ya kualikwa kwake, Mzee Gurumo alisema kuwa, hana neno linalotosha kulezea hisia zake juu ya tukio hilo la kukabidhiwa gari alilonunuliwa na msanii Diamond, ambaye ni msanii anayemkubali zaidi katika Bongo Fleva.
"Namshukuru sana huyu kijana (Diamond) kwa kitendo chake hiki ambacho ni cha kushtua na kushangaza wengi, namuombea kwa Mungu ampe mafanikio makubwa zaidi katika tasnia ya muziki wa kizazi kipya, ili aendelee kuwa juu zaidi," alisema Gurumo.
Gurumo aliyezaliwa mwaka 1940, alianza muziki mwaka 1960 na Bendi ya Kilimanjaro Chacha, kisha mwaka 1962 kuhamia Rufiji Jazz Band aliyofanya kazi kwa mwaka mmoja na kutimkia Kilwa Jazz mwaka 1963.
Mwaka 1964 akawa mmoja wa waasisi wa Nutta Jazz iliyobadili majina kadhaa kabla ya kuitwa Msondo Music, ambapo mwaka 1978 aliihama na kuanzisha DDC Mlimani Park, kisha akatimkia Orchestra Safari Sound na mwaka 1990 kurejea Msondo Music aliyostaafu nayo.

Na Salum Mkandemba



0 comments:

 

Sample text

Sample Text

PATA HABARI NA BURUDANI MBALI MBALI POPOTE ULIPO!

Sample Text