Mtoto ang'atwa na mamaye sehemu za siri
Wakizungumza kwa nyakati
tofauti na Tanzania Daima wilayani hapa juzi, wakazi hao, walisema mama huyo amekuwa
na tabia ya kumfungia ndani mtoto wake huku akimchapa zaidi ya nusu saa jambo
lililosababisha watoe taarifa kwenye dawati la haki za binadamu.
Walisema walifikia uamuzi
huo baada ya kuchoshwa na vitendo hivyo ikiwemo kumpiga mwanaye huyo kwa
kutumia nyaya za simu huku akimng’ata sehemu mbalimbali za mwili mtoto huyo na
kumsababishia maumivu makali.
Stella Musa alisema sehemu
za siri za mtoto huyo zimeharibiwa kutokana na kung’atwa na meno huku sehemu zake
za makalio zikiwa na vidonda ambavyo vinadaiwa vimetokana na kuchomwa
na ncha kali.
“Wazazi wa mtoto huyo ni
wanangu, siku moja mama wa mtoto huyo alishawahi kumuumiza mkono nilimchukua na
kukaa naye nyumbani kwangu kwa mwezi mmoja nikimuhudumia kwa kumkanda kwa maji
ya moto,”alisema Stela.
Mwalimu wa Shule ya Msingi
Mlongazila ambaye ni katibu wa dawati la kutetea haki za binadamu Paulo Idana
alisema suala hilo limewafikia hivyo wanachukua hatua za kisheria huku mtoto
huyo amewekwa chini yao kwa ajili ya matibabu zaidi.
“Tulimfuata mama huyo
Septemba 20 mwaka huu na tulifanya mahojiano mbele ya ofisa Mtendaji wa kijiji
hiki na alikiri akisema alifanya hivyo kwa sababu ya hasira lakini, sisi msimamo wetu tunafanya
utaratibu ili tuweze kumfikisha kwenye vyombo vya sheria,”alisema Idana.
Akisimuliwa taarifa hiyo mtoto
huyo, alisema wakati mwingine mama yake alikuwa akimwiita ili amfundishe kusoma
na aliposhindwa aling’atwa mgongoni, mapajani na sehemu za siri huku akisema
atafanyia hivyo hadi ajue kusoma ndipo ataacha kumwadhibu.
“Hivi vidonda vya mwilini mwangu
ni vya kung’atwa wakati mwingine napigwa na waya, hiki kidole mama alinikata
kutokana na kushindwa kusoma, alisema huku akilia kwa maumivu mtoto huyo.
Mama wa mtoto huyo, Moshi
Hamad alisema alikuwa akitoa adhabu kwa mwanaye huyo kutokana na kujisaidia haja ndogo na
kubwa hovyo wakati akirudi kutoka shule.
“Nafanya hivi kutokana na
hasira siwezi nikamuona mtoto wangu anajisaidia haja kubwa na ndogo kwenye nguo
nikamwacha tu lazima nimwadhibu mbona, kama jana alitapika kwenye sahani, je
mtoto kama huyu nitamwacha,”alihoji Moshi.
Mwenyekiti wa Kitongoji hicho,
Khadija Samizi alikiri kuwepo kwa tukio hilo hivyo serikali ya mtaa huo inafanya
utaratibu ili kuhakikisha anafikishwa kwenye vyombo sheria.
0 comments:
Post a Comment