Kenya yajigamba
kutoyumbishwa na ugaidi
NAIROBI,
Kenya
RAIS Uhuru
Kenyatta wa nchini hapa, amesema kuwa nchi yake haitatishwa na vitendo vya
ugaidi, wala shambulizi lililofanywa hivi karibuni halitaivunja moyo serikali yake.
Akizungumza
katika mkutano wake na wanahabari jijini jana, Rais Uhuru Kenyatta amewadhihaki
magaidi waliohusika na shambulizi la West Gate kama waoga na wahalifu ambao
njama yao ya kulitisha taifa na Wakenya imeshindwa.
Uhuru
amewapongeza wakenya kwa kusimama pamoja na bila kujitenga na kukataa
kutikishiwa na wahusika wa shambulizi la Westgate.Tamko hilo la Uhuru linakuja
wakati ambapo waziri wa usalama wa Kenya Joseph Ole Lenku anasema
wanawashikilia watu 8 wanaotuhumiwa kuhusika na shambulizi hilo la Westgate. Lenku amesema kati ya washukiwa 11, watatu walihojiwa na
kuachiliwa.
Lenku
ameongeza kuwa tayari wamewasiliana na polisi wa kimataifa Interpol kusaidia
kuwasaka magaidi wa kimataifa akiwemo muingereza Samantha Lewthwaite.
Aidha Lenku
ameongeza kuwa jumla ya watu 67 waliuawa kwenye shambulizi hilo wakiwemo maofisa
sita wa usalama.
Pamoja na
kutokea kwa tukio hilo lakini Kenya kwa kupitia waziri wake wa usalama wa ndani
Joseph Ole Lenku, ameapa kutoondoa wanajeshi wake nchini Somalia.
Aliendelea
kusema kuwa hawatafanya hivyo licha ya kuwepo kwa vitisho vya mashambulizi
zaidi ya kundi la kigaidi la Al Shabab wiki moja baada ya shambulizi kubwa
katika jengo la biashara la Westgate jijini Nairobi, lililogharimu maisha ya
watu zaidi ya 67.
Waziri Lenku
amewaambia waandishi wa habari kuwa hawatageuza mawazo kwa sababu walipeleka wanajeshi
wao Somalia kwa kuwa kundi la Al Shabab lilikuwa tishio kwa usalama wa taifa la
Kenya.
Alisema kwamba
nchi yake itaendelea kuchukua hatua hadi hapo usalama na matakwa ya nchi hiyo
yatakapolindwa.
Kauli
hizo ni majibu kwa Mkuu wa kundi la Al Shabab nchini Somalia Ahmed Abdi Godane
aliyesema kuwa shambulizi la Wastgate jijini Nairobi litafuatiwa na
mashambulizi mengine ya umwagaji damu zaidi, mpaka hapo Kenya itakapoondoa
wanajeshi wake nchini Somalia.
0 comments:
Post a Comment