Sudan Kusini yatimiza utabiri wa
Nyerere
![]() |
| Bashir, Machar na Kiir |
KATIKA moja
ya hotuba zake, Rais wa Kwanza wa Tanzania, marehemu Julius K. Nyerere, aliwahi
kusema kuwa, dhambi ya ubaguzi ni mbaya kama ilivyo tabia ya kula nyama ya mtu,
kwamba ukianza kula nyama ya mtu, hutaacha.
Aliyasema
hayo mwaka 1995 alipokuwa katika Hoteli ya Kilimanjaro (kwa sasa Hyatt Regency
Dar es Salaam), jijini Dar es Salaam alipoonya juu ya madhara ya kutaka
kuuchezea na hatimaye kuuvunja Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliozaa
Tanzania.
Nyerere
akasema, “Watu wazima wameuzungumza Muungano kwamba tuuvunje au uendelee. Mtu
mwenye akili hawezi kufikiri Uzanzibari ni fahari.” Akasema kuwa, nje ya
Muungano, kuna Wapemba na Waunguja. “Mtamaliza kutengana na Watanganyika, mara
mtakuta kumbe sisi si Wazanzibari.”
Mwalimu
Nyerere akasema, “Mtajikuta kuna Wapemba na Waunguja. Wapemba watapata
msukusuko kidogo na mara mtakuta kuna Wazanzibari na Wazanzibara. Hamtakaa
salama. Hamuwezi mkakaa salama baada ya kutenda dhambi ya kuwabagua watu wa
nchi yenu ileile moja mkawaita wale wao na hao sisi. Dhambi ile haiishii
hapo….”,
Tofauti na
Mwalimu alivyokuwa akitabiria Tanzania, utabiri huo umetimia katika nchi mpya ya
Sudan Kusini iliyojipatia uhuru wake, Julai 9, 2011.
Uhuru huo ni
zao lililotokana na hatu ya Januari 2011 baada ya wakazi wa Sudan Kusini kupiga
kura juu ya swali la kujitenga na Sudan wakaamua karibu kwa kauli moja kuwa
nchi huru.
Sababu kubwa
inayoelezwa ya kujitenga kwa nchi hiyo inaelezwa kuwepo kwa tofauti kubwa kati
ya nchi hizo ni kwamba katika Sudan yenyewe idadi kubwa ya watu wamekuwa
Waislamu na utamaduni wao una mchaganyiko wa tabia za Kiarabu na Kiafrika na
wengi wakizungumza lugha ya Kiarabu.
Kumbe kusini
kuna Waislamu wachache, wengi ni wafuasi wa dini za jadi na wengine wakiwa wakristo.
Ukizungumzia
upande wa kiuchumi na elimu nchi ya kusini ilielezwa kuwa nyuma ukilinganisha
na nchi ya kaskazini.
Shinikizo la
kimataifa lilizidi kuuandama uongozi wa Bashir ambako mwaka 2001, viongozi wa
Umoja wa Mataifa walitoa wito kufanyika kwa jitihada za kumaliza mgogoro na
kuruhusu misaada ya kibinadamu na wafanyakazi wa kimataifa kutoa msaada kusini
mwa Sudan.
Amani
ilipatikana baada ya kusainiwa rasmi kwa Mkataba wa Amani jijini Nairobi kwa
pande zote mbili na Januari 9, 2005 na al-Bashir alikubali mkataba wa amani
uliomaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe na kuiwezesha Sudan Kusini kupata haki
ya kujitawala.
Lakini vita
vingine vya ndani vilianza katika eneo la Darfur (Sudan Magharibi) na kutokea
kwa mauaji mengi na kufanyika matendo ya kinyama dhidi ya raia hali iliyomfanya
al-Bashir mpaka leo kukabiliwa na mashtaka mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya
Makosa ya Jinai(ICC), kama mshtakiwa wa makosa ya jinai dhidi ya haki za binadamu.
Baada ya
kutengana kwa sababu hizo na nyingine nyingi na baadaye kufanikiwa kupata uhuru
wakagundua kuwa nchi hiyo lazima itawalike kwa kuchanganya viongozi wa makabila
mawiliu makuwa ambayo ni Lou Nuer analotokea aliyekuwa Makamu wa Rais Riek
Machar na kabila la Dinka analotokea Rais Silva Kiir.
Lakini baada
ya kuingia madarakani chokochoko zilianza na baada ya kufanyika kwa uchunguzi
iligunduliwa kwamba Machar alikuwa na nia ya kutaka kumpindua Rais Kiir hali
iliyofanya Julai mwaka huu achukue uamuzi mgumu wa kumtimua wadhifa huo.
Baada ya
kumtimua Machar alisahau kwamba nchi hiyo ilijengwa kwa misingi ya makabila
mawili hivyo ndani ya jeshi kulikuwa na makananda wengi waliokuwa wakitokea
katika kabila la kiongozi huyo.
Mara baada
ya kumuondoa wanajeshi hao walilichukulia suala hilo sawa na kutengwa na hivyo kumuona
Kiir kama msaliti wao kwa kutaka kutawala mwenyewe na kabila lake kwa kugawana keki
ya taifa.
Wanajeshi
hao waliamua kumuunga mkono Machar na kutangaza kuasi jeshi na kuingia msituni
kwa nia ya kuung’oa utawala wa Kiir.
Wanajeshi
hao kwa sasa wameshafanikiwa kuteka baadhi ya miji katika nchi hiyo hali
inayoweonesha uwezekano wa kuzuka kwa mapigano makubwa zaidi na kufanya hali
katika taifa hilo jipya changa kabisa duniani kutibuka kwa haraka ambapo hivi
sasa maelfu ya raia wakihama nchi hiyo kwa kukimbia vita.
Inaripotiwa
kwamba idadi ya vifo mpaka sasa imefikia 1,000 huku mapigano yakiendelea kwa zaidi
ya wiki.
Machar
ameapa kumuondowa Kiir madarakani na vikosi vyake tayari vimeuteka mji wa Bor
ambao ni mji Mkuu wa jimbo lenye vurugu la Jonglei ukiwa kama kilomita 200,
kaskazini mwa mji mkuu wa Juba na pia wameuteka mji wa Bentiu ambao ni mji mkuu
wa jimbo muhimu lenye kuzalisha mafuta la Unity.
Serikali ya
Juba imekiri kwamba waasi wamefanikiwa kuchukua udhibiti wa majimbo ya Joglei
na Unity huku maelfu ya watu wakikimbilia katika Mako Makuu ya Umoja wa Mataifa
(UN) kupata hifadhi.
Msemaji wa
jeshi la Sudan Kusini Philip Aguer mpaka jana alisema kuwa serikali imechukuwa
hatua kwa ajili ya kufanya mashambulizi ya kurejesha miji yao iliyotekwa na
waasi.
Anasema kuwa
wanajeshi wao wataukombowa mji mwa Bor kutoka kwa vikosi vya waasi ambao bado
unadhibitiwa na vikosi vya Machar lakini wanajiandaa kuudhibiti tena.
Matamshi
hayo yanaibuka licha ya kuwepo kwa juhudi za kidiplomasia za mataifa ya Afrika
na wito kutoka Marekani, Uingereza na Umoja wa Mataifa wa kutaka kusitishwa kwa
mapigano hayo.
Mratibu mkuu
wa masuala ya misaada ya kibinaadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini
Toby Lanzer ameutembelea mji huo wa Bor juzi na kusema kwamba hali inazidi kuwa
mbaya.
Amesema kuna
maelfu ya raia wa Sudan Kusini waliokimbilia vichakani au kurudi kwenye vijiji
vyao ili kuepuka madhara.
Ameongeza
kusema ana wasi wasi mkubwa wa vita vinavyounyemelea mji huo ambapo amekiri
kwamba ni jambo lisilofikirika kwa wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa
Mataifa kuwa katika uwezo wa kuwalinda raia wanaokadiriwa kufikia 15,000
wanaotafuta hifadhi katika kambi ya UN iliyoko huko.
Kwa mujibu
wa Lanzer raia wa Australia,Uganda na Ethiopia ni miongoni mwa watu wanaotafuta
hifadhi katika kambi ya UN huko Bor.
Ofisa huyo
mwandamizi wa UN pia amesema helikopta za kiraia zimewahamisha raia wa Marekani
kutoka mji huo ulioshuhudia mashambulizi mazito ya bunduki za rashasha lakini
kuna raia 3,000 wa nchi kama vile Canada,Uingereza na Kenya wameendelea kuwaondoa
katika mji huo.
Lanzer
ambaye anatafuta msaada wa kifedha wa haraka kutoka Jumuiya ya Kimataifa
amesema idadi ya wakimbizi wa ndani ya nchi inaweza kupindukia na kufikia 100,000.
Rais Barack
Obama wa Marekani mwishoni mwa wiki ametuma barua kwa viongozi wa bunge la nchi
hiyo akiwajulisha kwamba huenda akachukua hatua zaidi za kijeshi Sudan Kusini
ili kuwalinda raia wa Marekani, wafanyakazi na mali zao.

0 comments:
Post a Comment