Social Icons

PATA HABARI NA BURUDANI MBALI MBALI POPOTE ULIPO!

Thursday, January 30, 2014

 Lipumba: Viongozi wabovu ni sababu ya uchumi tegemezi



MWENYEKITI wa Chama Cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba amesema kuwa sababu za kuwa na uchumi tegemezi zinachangiwa na kuongozwa na viongozi wabovu wanaoendesha nchi kwa kutokuwa na dira.
Akizungumza hivi karibuni jijini Dar es Salaam, Profesa Lipumba ambaye ni mtaalamu wa uchumi alisema uongozi bora ni jambo muhimu katika maendeleo ya kiuchumi.
Alisema kama uongozi unakuwa mbovu hauwezi kuwa na dira ya kuweza kujenga uchumi usiokuwa tegemezi ila utakachofanya ni kushiriki katika biashara.
Profesa Lipumba alifafanua kwa kusema “Uchumi tegemezi ni ule ambao serikali haina uwezo wa kuendesha shughuli zake za ndani ila kwa kupata misaada kutoka nje,”.
Akielezea matatizo ya uchumi yanayolikumba taifa kwa sasa alisema ni matatizo yaliyoanza mwanzoni mwa mwaka 1960 katika nchi nyingi za kiafrika kama Tanzani, Ghana, Guinea ambazo zilikuwa na mikakati ya kujaribu kujenga ujamaa.
Anasema kuwa katika ujenzi wa ujamaa Tanzania haikuweza kutoa fursa kwa wajasiliamali wa ndani kuwawezesha kuwa wawekezaji na kuwawezesha kujua mbinu za kibiashara kwa nia ya kuwawezesha kuongeza uzalishaji .
“Kwa mfano hapa Tanzania mkulima aliyekuwa na ekari 10 alihesabika kama Bepari na Kabaila, wakati heka hizo ni kidogo sana. Hali iliyosababisha kuwa na sera za kujenga ujamaa wa vijijini ambapo wakulima wote walitakiwa kuwa na shamba la pamoja la ujamaa ambalo lilitakiwa kuwa na manufaa kwa watu wote,”.
Anaongeza kuwa sera hizo ziliondoa motisha kwa wakulima wadogowadogo kuwekeza katika sekta ya kilimo ikiwamo kuweza kujiendeleza na kuweza kukuza kilimo chao.
Alisema kuwa “Matatizo zaidi yalionekana mwaka 1970, ingawa kulikuwa na matatizo ya uchumi wa dunia na kuanguka kwa bei ya bidhaa zetu ikiwamo kuongezeka kwa bei ya mafuta hali iliyotufanye tujikute tumeingia katika matatizo makubwa ya  ukosefu wa fedha za kigeni,”.
Alisema kuwa baada ya kujikuta katika hali hiyo ilibidi kujikuta nchi ikiangukia katika mikono ya mashirika ya Kimataifa ya Fedha hususani Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Benki ya dunia kwa sababu nchi haikuwa na fedha za kigeni hivyo ikawa inahitaji kupata misaada iweze kujiendesha.
“Tatizo hilo liliendelea kwa muda mrefu na kusababisha kushindwa kujinasua na kujenga uchumi ambao unatoa fursa kwa wananchi wenyewe kuwa wajasiliamali ili waweze kuwekeza na hapo ndipo tukaacha kilimo pembeni na wakulima wadogowadogo bila msaada,” alisema Profesa Lipumba.
Akielezea kuhusu aina za utegemezi Profesa anasema kuwa ni utegemezi wa masoko ambao nchi nyingi za Afrika zimekuwa zikizalisha mali ghafi na kuziuza katika nchi za Magharibi ikiwamo na zile za Asia ya Mashariki.
Utegemezi mwingine ni ule wa Teknolojia ambazo huagizwa kutoka nchi za nje na mwingine ni ule wa mitaji kutoka kwa wawekezaji wa nje hasa katika sekta binafsi unafanyika kwenye maeneo ya madini na viwanda.
Utegemezi mwingine ni misaada ambayo huingia katika bajeti za serikali ambayo karibu theluthi moja inategemea misaada kutoka nje pamoja na kujitawala katika miaka 52, nchi imeshindwa kujinasua katika wimbi la utegemezi kutoka nchi za Magharibi.
Utegemezi mwingine aliouzungumzia ni ule ambao hauepukwi wa kushirikiana katika kujenga uchumi wa kisasa ambao ni kushirikina katika biashara na nchi zilizopiga hatua katika Maendeleo makubwa.
“ili uweze kuendelee lazima ushirikiana nazo ili uweze kujijengea uwezo, jambo ambalo tumeshindwa ni kuweka mkakati wa kujenga uwezo wa ndani, wa kuweza kuwa na viwanda vinavyotengeneza bidhaa kwa kuweza kuongeza thamani ya malighafi tunazozalisha ndani ya nchi, na kuweza kutrumia vizuri rasilimali zetu na kuweza kujiletea maendeleo, tumekuwa na udhaifu katika matumizi ya fedha za umma, tumekuwa na udaifu katika ukusanyaji wa mapato ya serikali na kutumiwa kwa tija ili kuongeza uzalishaji, kukipa kipaumbele kilimo cha mkulima mdogomdogo ili aweze kuongeza uzalishaji kwa kuwa anakuwa soko la bidhaa za viwandani,” alisema.  



 

Sample text

Sample Text

PATA HABARI NA BURUDANI MBALI MBALI POPOTE ULIPO!

Sample Text