Wanaume ‘Karolaiti’ za nini kwenye filamu?
KARIBUNI kwenye safu ya ‘Vunja vunja’ ambayo hukujia kila Ijumaa ikiwa maalumu kwa ajili ya kuchambua filamu za nyumbani, lengo likiwa kuziboresha na kuzifanya ziwe za kimataifa.
Mada ya leo inazuzungumzia kuhusu waigizaji wetu wa kiume kuingia katika mkumbo wa kujichubua, huku wengi wakidhani huenda kufanya hivyo kunaongeza ubora wa filamu.
Sababu kubwa ya kuandika makala hii ni kutokana na kuibuka kwa wimbi kubwa la wasanii wengi wa kiume hapa nyumbani kutumia mkorogo, maarufu kama ‘Karolaiti.’
Suala hili si geni kwa watazamaji wa filamu za hapa nyumbani ambao wamekuwa mashuhuda wakiwashuhudia baadhi ya waigizaji walioanza wakiwa weusi, tena wakiwa wanavutia kuwatazama, lakini hivi sasa wamejikoroga na kushindwa kuwatambua aina ya rangi zao kama ni weupe, njano au wekundu.
Tabia hiyo waliyojijengea wasanii wanaume, kufanya mambo ambayo hufanywa na mabinti ndiyo imenifanya nikose uvumilivu kama mdau.
Nadhani wengi hufanya tabia hii wakifikiri wanapojichubua ndipo filamu zao zitaongezeka ubora au kupiga bao nje ya nchi.
Swali ninalojiuliza ni kwamba, wanafanya hivyo ili wawe kama Wazungu ambao ndio wamefanikiwa katika fani hii ya uigizaji?
Wasanii hawa wasifikirie kwamba kupiga bao kwa filamu za Wazungu huchangiwa na weupe wao. Wajue kuwa huchangiwa na ubora wa filamu zao.
Kujipodoa hakukatazwi, lakini kitu cha muhimu ambacho wasanii hawa wanapaswa kuangalia ni kuepuka kujichubua ngozi zao.
Pia wao kama kioo cha jamii wakumbuke kuwa mbali ya kwenda kinyume na tamaduni za mtoto wa kiume, matumizi ya mikorogo ni hatari kwa ngozi ya binadamu.
Wasanii wetu wanatakiwa kuachana na dhana mgando za kutumia mikorogo kwa kutaka pengine kufanana na mwigizaji kutoka Nigeria, Nouh Ramsey.
Si vibaya kwa mtoto wa kiume kujipamba, lakini si busara wala hekima kujichubua ngozi kiasi cha kushindwa kujulikana mwanaume na mwanamke ni yupi?
Waigizaji wa hapa nyumbani wanatakiwa wajifunze madhara ya kujichubua kupitia kwa Mfalme wa Pop duniani, Michael Jackson kwa yaliyompata na kujikuta akimomonyoka huku akiwa hai, hadi kufariki dunia.
Wanachopaswa kujua wasanii wetu wa hapa nyumbani ni kwamba, wanatakiwa kuiga mambo yanayoelimisha na yasiyoathiri mila na tamaduni zetu.
Kinachosikitisha ni kwa wasanii hawa kupenda kuiga bila kujua faida au athari ya kile anachoiga kutoka kwa mastaa wengine, hasa yale yahusuyo muonekano wao.
Wasanii wetu wanachotakiwa ni kujali kufanya kazi kwa bidii kitendo kinachoweza kuwaletea umaarufu katika fani yao.
Kuna nyota kibao wanaofanya vizuri katika kiwanda cha filamu nchini Marekani, Hollywood, pamoja na kuwa na ngozi nyeusi, lakini heshima zao zimekuwa kubwa katika tasnia hiyo kuliko hata wazungu.
Mfano wa watu hao ni pamoja na Danzel Washington, Bill Branks ambao wamefanikiwa kupata umaarufu sana katika tasnia hiyo wakiwa na ngozi zao za asili.
Sasa kama ubora ungekuwa ni rangi, nyota hawa ndio wangeanza kupaka mikorogo kwa sababu kwao huuzwa kwa bei nafuu.
Kwa heri tuonane wiki ijayo…
.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment