Syria lazima ishambuliwe bila idhini
ya UN
DAMASCUS, Syria
MAREKANI na Uingereza wanapoamua kuishambulia nchi yoyote
duniani kwa sababu za kweli au uongo lazima watakamilisha jambo hilo pasipo
kuzuiliwa na chombo au nchi nyingine iliyo mwanachama au
Umoja wa Mataifa wenyewe kutokana na ukweli kwamba hata umoja huo hauwezi kusimama bila ya kupewa jeuri na Marekani.
Marekani ndiyo inayotoa mchango mkubwa wa kuusaidia Umoja wa
Mataifa (UN), tangu kuasisiwa kwake mwaka 1945, imekuwa ikichangia zaidi ya
asilimia 27 ya bajeti yake. Mwaka 2011 imefanikiwa kuichangia UN kiasi cha dola
milioni 516.3 ikiwamo na zaidi ya dola bilioni 2.182 kwa ajili ya bajeti ya
amani.
Ukiachilia kiasi hicho lakini pia imekuwa ikijihusisha moja
kwa moja katika kusaidia kwa hiari kutoa michango mbalimbali katika ya Umoja
huo.
Kwa sababu hiyo inaonesha kabisa nchi hiyo kusubiri idhini
ya UN ni geresha na ndiyo sababu hata katika nchi ambazo Marekani na washirika
wake waliamua kuzishambulia bila idhini yake hakuna hatua iliyoichukulia nchi
hiyo kwa kuogopa kukosa misaada wanayokuwa wanapewa.
Kauli za Uingereza na Marekani zinazoinyooshea kidole Syria
kutumia silaha za sumu zinaashiria kwamba wapo tayari muda wowote kuishambulia
nchi hiyo kama walivyofanya kwa Iraq na Libya pamoja na kuwepo kwa nchi
wanachama kuonesha kutokubalina nao.
Kwa kuthibitisha kwamba nchi hizo zimedhamiria kuichapa
Syria inatokana na matamko yao ambako jana washauri wataalamu wa masuala ya
sheria wa Uingereza wamemueleza rais wao, David Cameroon kwamba anaweza kuishambulia
nchi hiyo pasipo kusubiri kuungwa mkono na Umoja wa Mataifa (UN).
Washauri hao wamemueleza kwamba Uingereza itaingia
kushambulia kwa kigezo kwamba wanazuia raia wa Syria kuuawa zaidi, hata ikiwa
wanachama wa kudumu wa baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Urussi na Uchina ambao
ni washirika wa Syria wakitumia kura zao za turufu kupinga mikakati za kijeshi
dhidi ya utawala wa Syria haitakuwa na maana.
Maofisa wa ujasusi nchini Uingereza wamemueleza Waziri Mkuu,
David Cameron kuwa wanaushahidi wa kutosha unaoonesha serikali ya Syria
ilihusika na shambulio la kemikali wiki iliyopita mjini Damascus.
Pamoja na kwamba Serikali ya Syria imekuwa ikikana madai ya
kutumia silaha za kemikali katika shambulio mjini Damascus Agosti 21, iliyosababisha mamia ya watu kuuawa.
Wadadisi wengi wamekuwa wakielezea kuhusu ubabe unaofanywa
na nchi hizo kwa kuendelea kuishutumu nchi hiyo kutumia silaha za kemikali
wakati wakijua fika wao wenyewe wamekuwa wakipitisha silaha kwa waasi ili
wapigane na serikali jambo ambalo si sawa kwa sheria za kimataifa.
Kuwaunga kwao mkono waasi wa nchini humo inaonesha fika
mataifa hayo yameonesha nia ya kuishambulia nchi hiyo kwa sababu yoyote iwe ya
kweli au ya kutengeneza.
Ofisi ya Waziri mkuu wa Uingereza, imechapisha ripoti hiyo,
kuambatana na ushauri wa mkuu wake wa sheria Dominic Grieve, inayotoa idhini ya
mashambulio ya kijeshi kwa kisingizio cha kuzuia utumiaji wa silaha za kemikali
siku zijazo, kuambatana na sheria za kimataifa.
Rais Barack Obama
Pamoja na kwamba Marekani ndiyo iliyoelezwa kusogeza manuari
zake karibu na nchi ya Syria kitendo kinachotafsiriwa kuwa tayari kwa vita
dhidi ya nchi hiyo lakini rais wa nchi hiyo, Barack Obama hivi karibuni amesema
bado hajasaini mpango wa kuishambulia Syria.
Obama ametoa kauli hiyo huku akiweka wazi kama watahitaji
kuishambulia nchi hiyo watachukua hatua hiyo bila kuhitaji ruhusa ya Umoja wa
Mataifa (UN).
Shaka nyingine inayoonekana kuwa ni mpango wa kuishambulia
Syria ni kwa nini tukio hilo litokee baada ya Obama kuionya nchi hiyo kutotumia
silaha za sumu nchini Syria kwamba yatakuwa yamevuka mstari mwekundu uliowekwa
na Marekani.
Ofisa mwandamizi wa Ikulu ya Marekani ameliambia shirika la
habari la AFP kwamba serikali itawataarifu wabunge waandamizi kuhusu taarifa za
kijasusi juu ya shambulio hilo la silaha za sumu na kuona hatua ya kuchukua.
Alipoulizwa kama anapanga kuamuru shambulio dhidi ya Syria,
Obama amekiambia kipindi cha televisheni cha Marekani cha PBS katika mahojiano
kwamba bado hajafikiria kufanya uamuzi huo.
Lakini ametoa kauli ya kutisha na kuogofya akisema Marekani
imepanga kuiadhibu Syria ili kuhakikisha nchi hiyo haitorudia tena jambo hilo.
Diplomasia ndio
suluhisho
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ameyataka
mataifa makubwa kuepusha mzozo huo wa Syria na kusema kwamba wakaguzi wa Umoja
wa Mataifa inapaswa kupewa muda zaidi na kutowa ombi jipya kwa Baraza la
Usalama la Umoja wa Mataifa kundokana na tofauti zao kuhusu Syria.
Rais Vladimir Putin wa Urusi na mwenzake wa Iran Hassan
Rouhani wanakubali kwamba matumizi ya silaha za sumu ni jambo lisilokubalika
lakini wanapinga kuingiliwa kijeshi katika nchi hiyo ambayo ni mshirika wao.
Taarifa ya Ikulu ya Urusi imesisitiza haja ya kutafuta njia
za kuutatuwa mzozo huo kwa njia ya kidiplomasia na marais wa nchi hizo mbili
wameujadili mzozo huo wa Syria kutokana na ombi la Iran.
Marekani wa washirika wake wamekuwa wakionekana kuwa
miongoni mwa nchi zinazochangia kuchochea vurugu duniani kwa kivuli cha kulinda
amani, ila baada ya kufanya shughuli zake hizo wanaziacha nchi hizo zikiishia
katika machafuko zaidi kabla ya kuingia kwao kwa mfano nchi za Afghanistan,
Iraq, Libya na Misri.


0 comments:
Post a Comment