Social Icons

PATA HABARI NA BURUDANI MBALI MBALI POPOTE ULIPO!

Wednesday, September 25, 2013



Al-Shabaab yadai mateka 137 wamefariki


KUNDI la Al-Shabaab limedai kuwa mateka 137 waliowachukua wamefariki katika uvamizi wa kituo cha biashara, idadi ambayo ni vigumu kuithibitisha na kubwa kuliko idadi iliyotangazwa kuwa hawajulikani walipo.
Wapiganaji hao walio na mafungamano na mtandao wa Al-Qaeda, katika ujumbe waliouweka katika mtandao wa kijamii wa twitter, walisema mateka 137 waliokuwa wanashikiliwa na mujahedeen walikufa.
Waliwashtumu pia wanajeshi wa Kenya kwa kutumia vifaa vya kemikali kukomesha mkwamo huo uliodumu kwa siku nne.
"Katika hatua ya uoga wa dhahiri, vikosi vya Kenya kwa makusudi vilitumia kemikali," ulisema ujumbe mmoja na kuongeza kuwa, “ili kufunika uhalifu wao, serikali ya Kenya iliendesha zoezi la kuliporomosha jengo, na kuuzika ushahidi na mateka wote chini ya vifusi."
Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta, alitangaza kumalizika kwa umwagaji huo wa damu uliodumu kwa saa 80 jioni ya Jumanne, ambao ulisababisha vifo vya raia 61 na maofisa sita wa vikosi vya usalama.
Polisi ilisema idadi hiyo ya vifo ingeweza kuongezeka, ambapo shirika la misaada la Msalaba mwekundu lilisema kuwa ni watu 63 ambao bado hawajulikani walipo.
Hakukuwa na kauli kutoka serikali ya Kenya kuhusiana na madai hayo, lakini Al-Shabaab wamekuwa wakitoa madai ya ajabu huko nyuma, hasa kupitia akaunti yao kwenye mtandao wa twitter.
Kundi hilo lilisema lilifanya shambulizi hilo katika kulipiza kisasi dhidi ya Kenya kutokana na kujiingiza nchini Somalia kupambana na wanamgambo hao.
Katika moja ya mashambulizi yaliyofanywa katika historia ya Kenya, wapiganaji hao waliingia katika jengo la maduka la Westagate lenye ghorofa nne, ambalo linamilikiwa kwa sehemu na raia wa Israel.
Kenya ilianza siku tatu za maombolezi rasmi jana, ambapo bendera za taifa zinapepea nusu mlingoti, huku wafanyakazi wa uokozi wakisafisha mabaki ya jengo la Westgate kutafuta miili ya wahanga wa tukio hilo.
Karibu watu 200 walijeruhiwa katika uvamizi huo wa siku nne, ambao ulishuhudia mapambano makali kati ya wapiganaji na vikosi vya usalama vya Kenya katika jengo hilo, ambalo ndicho kituo kikubwa zaidi cha biashara na maarufu kwa watu wenye uwezo nchini Kenya, wanadiplomasia, wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa na watalaamu wengine.

0 comments:

 

Sample text

Sample Text

PATA HABARI NA BURUDANI MBALI MBALI POPOTE ULIPO!

Sample Text