Social Icons

PATA HABARI NA BURUDANI MBALI MBALI POPOTE ULIPO!

Tuesday, September 24, 2013


Siku tatu za maangamizi ya Al shabaab Westgate 


KAMA kuna jambo ambalo kwa sasa linatikisa Afrika Mashariki na dunia kwa ujumla ni hili la vikosi vya al Shabaab kushambulia na kuteka raia waliokuwa kwenye jengo la kibiashara maarufu kama ‘Westgate’ nchini hapa. 
Hadi jana vikosi vya usalama nchini Kenya vinasema vimelidhibiti jengo zima la Westgate mjini Nairobi, ikiwa ni zaidi ya siku tatu baada ya jengo hilo kuvamiwa na wanamgambo.
Hadi jana asubuhi kulisikika milipuko ikifuatiwa na milio ya risasi kutoka ndani ya jengo hilo huku duru zikisema kuwa vikosi vya usalama vinaelekea kukamilisha operesheni hiyo.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari, magaidi sita waliokuwa wamebaki wameuawa na wengine watatu wakiwa wameuawa jana.
Serikali imesema zaidi ya watu 60 wameuawa na wengine zaidi ya 170 kujeruhiwa katika shambulio hilo ambalo Al shabaab imekiri kulitekeleza.
Wizara ya Mambo ya ndani imesema wanajeshi wanaendelea kulisaka jengo zima la Westgate kutoka ghorofa moja hadi nyingine kuhakikisha kwamba hakuna mateka aliyebakia.
Wakati huohuo, waziri wa mambo ya nje amesema kuwa wawili kati ya wanamgambo watatu waliofanya shambulio hilo ni raia wa Marekani pamoja na mwanamke mmoja Muingereza.
Kwenye mahojiano na kituo kimoja cha televisheni nchini Marekani, Amina Mohamed alisema kuwa Wamarekani walikuwa kati ya umri wa miaka 18 na 19 wenye asili ya kisomali na waliishi mjini Minnesota.
Mshtakiwa mwingine alikuwa mwanamke Muingereza ambaye inasemekana alikuwa amefanya vitendo vingi vya aina hii kwa niaba ya Al Shabaab.
Mpaka sasa inaelezwa na shirika la Red Cross kuwa watu 63, hawajulikani waliko.
Operesheni hiyo iliendelea usiku kucha ingawa kwa mujibu wa waziri wa usalama wa Kenya, ilikuwa katika hatua za mwisho na mateka wote wamefanikiwa kuokolewa.

Ruto apata afueni ya muda
Tatizo hilo lilimuwezesha Makamu wa Rais wa Kenya William Ruto kupewa ruhusa ya wiki moja na Jaji wa Mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita (ICC), kwa ajili ya kurejea nyumbani kushughulikia hali ya kiusalama inayokumba taifa hilo.
Ruto na Rais Uhuru Kenyatta, wanakabiliwa na tuhuma za za uhalifu dhidi ya binadamu baada ya kudaiwa kuhusika na ghasia za kikabila baada ya uchaguzi wa mwaka 2007-2008 ambapo watu zaidi ya elfu moja waliuawa.
Kauli ya Marekani
Rais Barack Obama amempigia simu rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta na kumpatia pole kwa niaba ya Wananchi wa Marekani kutokana na shambulizi walilofanyiwa na magaidi wa Ala Shabaab.
Taarifa ya Ikulu ya Marekani imeeleza kuwa Obama amemuahidi Uhuru kumuunga mkono katika jitihada za kuusambaratisha mtandao wa kundi la waislamu wenye msimamo mkali la al-Shabab.
Kundi hilo la al Shabaab limesema kuwa limefanya shambulio hilo kwa nia ya kulipa kisasi cha kupigwa na kuondolewa katika nchi ya Somalia wakati walipokuwa wameukalia mji wa Somalia mwaka 2011.
Nini na nani Al Shabaab?
Al-Shabab ni neno la kiarabu linalomaanisha Kijana.
Kundi hilo liliibuka kama tawi la vijana la muungano wa mahakama za kiislamu ambao baadaye muunganiko huo ulivunjika mwaka 2006.
Kuvunjika huko kulitokana na mapigano yaliyotokea baina ya wanajeshi wa Ethiopia waliokuwa wameingia nchini Somalia kuunga mkono serikali iliyokuwa dhaifu.
Kundi hilo likiwa Somalia liliweka sheria kali za kiisilamu katika maeneo ambayo linadhibiti ikiwemo wazinifu kupigwa kwa mawe hadi kufa na kutokubali mambo ya ndoa za jinsia moja (ushoga).
Je Al Shabaab linadhibiti sehemu gani ya Somalia?
Ingawa kundi hilo limepoteza udhibiti, wa miji mikubwa, bado linakita mizizi katika maeneo ya mashina.
Lililazimika kuondoka katika mji mkuu Mogadishu, Agosti mwaka 2011 na pia kuondoka katika mji wa bandarini wa Kismayo Septemba mwaka 2012.
Kismayo ulikuwa mji muhimu kwa kundi hilo, ambao ulikuwa unawezesha bidhaa kuwafikia wapiganaji wa kundi hilo pamoja na kuwatoza watu ushuru kwa shughuli zao.
 Hizi ni silaha za Al Shabaab walizonasa wanajeshi wa AU
Muungano wa Afrika, ambao unaunga mkono juhudi za majeshi ya serikali, ulisherehekea ushindi huo ingawa al-Shabab hufanya mashambulizi ya mara kwa mara ya kujitoa mhanga mjini Mogadishu na kwingineko.
Wadadisi wanaamini kuwa al-Shabab limeanza kufanya mashambulizi ya kuvizia baada ya kushindwa na majeshi ya Muungano wa Afrika wanaotumia nguvu dhidi yao.
Lakini linakabiliwa na tisho kubwa kutoka kwa wanajeshi wa Kenya walioanza harakati zao dhidi ya kundi hilo kuanzia mwaka 2011.
Kenya ilituhumu wapiganaji wa al-Shabab kwa kuwateka nyara wanajeshi wake pamoja na watalii na sasa wamekuwa katika msitari wa mbele kupambana na kundi hilo.
Nani kiongozi wa al-Shabab?
Ahmed Abdi Godane ndiye kiongozi wa kundi hilo ambaye wakati mwingine hujulikana kama Mukhtar Abu Zubair, na anatoka katika jimbo la Somaliland.
Kumekuwa na taarifa za mgawanyiko katika kundi hilo, ambazo hata hivyo zinapingwa vikali na kundi lenyewe.
Inaelezwa kuwa uongozi wake unapingwa, na wanachama wanaotoka maeneo ya Kusini na ambao ni wengi katika kundi hilo ambao wanadaiwa idadi yao kuwa ni kati ya wanajeshi 7,000 na 9,000.
Godane huwa haonekani hadharani kama ilivyokuwa kwa mtangulizi wake, Moalim Aden Hashi Ayro, aliyeuawa katika shambulizi lililofanywa na Marekani mwaka 2008.
Mahusiano yake kimataifa
Al-Shabab lilijiunga na al-Qaeda Februari mwaka 2012 na hilo lilibainishwa katika ujumbe wa Video uliooneshwa kiongozi wa al-Shabab Ahmed Abdi Godane akisema anaahidi kuunga mkono kingozi wa al-Qaeda Ayman al-Zawahiri.
Makundi hayo mawili yamekuwa yakifanya kazi kwa pamoja, na raia wa kigeni wamekuwa wakiunga mkono kundi hilo, na hata kuwasaidia katika harakati zao za mapigano.
Mwaka jana maofisa wa al-Shabab waliambatana na mtu aliyesema ni mwanachama wa al-Qaeda na kumtambua kuwa raia wa Marekani Abu Abdulla Almuhajir alipokuwa anatoa msaada wa chakula kwa waathiriwa wa njaa.
Maofisa nchini Marekani wanaamini kuwa wapiganaji wa Al Qaeeda waliokuwa Afghanistan na Pakistan wamekuwa wakitafuta hifadhi katika nchi ya Somalia.



0 comments:

 

Sample text

Sample Text

PATA HABARI NA BURUDANI MBALI MBALI POPOTE ULIPO!

Sample Text