Upinzani Zimbabwe
wakebehi baraza la mawaziri
WAPINZANI nchini
hapa umekosoa baraza jipya la mawaziri lililotangazwa na Rais Robert Mugabe,
ukisema kiongozi huyo ameteua watu walewale ambao wameshindwa kuleta mabadiliko
nchini humo.
Chama kikuu
cha upinzani nchini humo cha MDC-T kimesema kuwa mawaziri walioteuliwa kuunda
baraza jipya la mawaziri toka chama tawala cha ZANU-PF lina sura zilezile za
wazee na viongozi ambao wameshindwa kuleta mabadiliko nchini Zimbabwe.
Akizungumzia
hilo, msemaji wa MDC, Douglas Mwanzora amesema hakuna mabadiliko ambayo
yanatarajiwa kufanyika kwenye Serikali ya sasa kwa sababu uteuzi wa mawaziri
haukuzingatia vigezo na uwezo wa watu katika kuleta mabadiliko nchini humo.
Mwonzora
ameongeza kuwa wengi wa mawaziri wanaounda baraza jipya la mawaziri walikuwepo
kwenye Serikali ya umoja wa kitaifa iliyomaliza muda wake na wengi walishindwa
kuleta mabadiliko ambayo wananchi wa Zimbabwe wanayataka.
Wakati wa
sherehe za kuapishwa kwa mawaziri hao, Rais Mugabe ameahidi kuleta mabadiliko
kwenye Serikali yake na kudai kuwa atayashughulikia makampuni ya kigeni
yaliyoko nchini humo kukubali uwekezaji wa asilimia 51 kubaki kwa Zimbabwe na
wao kuchukua asilimia 49.
Rais Mugabe
amesema anataka kuona mabadiliko nchini mwake na kumtaka kila waziri
aliyemchagua kutekeleza kile ambacho wananchi waliwapa dhamana wakati wa
kempeni za urais.
Baraza jipya
la mawaziri limejaa nyuso za viongozi waliopigania uhuru wa Zimbabwe na watu
ambao ni wafuasi wa damu wa chama tawala cha ZANU-PF.
Katika hatua
nyingine, aliyekuwa waziri wa sheria, Patrick Chinamasa ameteuliwa kuongoza
wizara ya uchumi na biashara akiwa na jukumu la kuhakikisha uchumi wa Zimbabwe
unaimarika.
Kiongozi
mkuu wa upinzani nchini humo, Morgan Tsvangirai ameendelea kusisitiza kuwa
uchaguzi wa mwaka huu uligubikwa na mizengwe na ushindi wa rais Mugabe haukuwa
halali.

0 comments:
Post a Comment