Social Icons

PATA HABARI NA BURUDANI MBALI MBALI POPOTE ULIPO!

Tuesday, October 15, 2013




AU na mipango ya kumuokoa Kenyatta, Ruto ICC

ADDIS ABABA, Ethiopia
TANGU alipotangaza nia ya kuwania wadhifa wa urais wa nchini Kenya, Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake, William Rutto, walijikuta wakibanwa zaidi na hoja ya mashtaka ya mauaji baada ya uchaguzi wa nchi hiyo mwaka 2007, yaliyokuwa yamefikishwa mbele ya Mahakama ya kimataifa ya Makosa ya Jinai(ICC).
Wengi walikuwa wakijiuliza ni kwa namna gani viongozi hao wangeweza kuongoza nchi hiyo wakati upande mwingine wa sarafu waandamwa na mashtaka katika kesi yao iliyofunguliwa Hague, Uholanzi.
Rais Kenyatta (kushoto) na William Ruto
Raila Odinga aliyepata kuwa Waziri Mkuu na mpinzani mkuu Muungano wa Jubilee uliokuwa umewapa ridhaa viongozi hao alikuwa akionesha wasiwasi wake waziwazi na mara kadhaa ikiwamo kwenye mdahalo wao alisema bila kutafuna neno kwamba itakuwa vigumu kwa Uhuru Kenyatta kuongoza Kenya wakati akiwa kizimbani na pia itakuwa ngumu kuongoza kwa kupitia mtandao wa Skype (mawasiliano ya mtandao kwa njia ya video).
Mara kadhaa rais Uhuru Kenyatta alipokuwa akitafuta kura amekuwa akiahidi Wakenya na dunia kwamba kesi yake inayomkabili haitaathiri shughuli za kiuongozi kwani atakuwa akitumia muda wake wa ziada kujisafisha mbele ya mahakama hiyo ya ICC.
Lakini cha kushangaza filamu hii ya ICC inajikuta inahitimishwa katika wiki hii kwa Uhuru Kenyatta kuonesha wazi wazi kwamba hayuko tayari kuandika historia ya kuwa kiongozi wa kwanza katika ngazi ya urais kutinga kwenye mahakama hiyo kujibu mashtaka yake ya Jinai.
Kauli alizozitoa kabla ya kuanza kwa mkutano wa Umoja wa nchi za Afrika(AU), ziliashiria kabisa hana mpango wa kwenda Hague, Uholanzi kwa ajili ya kujibu mashtaka yanayomkabili.
Katika hotuba yake Rais Kenyatta ameishutumu mahakama ya ICC kwa kusema si chombo cha kutekeleza uadilifu bali ni mahakama ya kibaguzi na mwanasesere wa madola ya kibeberu.
Akaishutumu ICC kwa kusema ni wakala wa himaya ya kibeberu anayoiona kama chombo kinachosambaratika.
Anasema “Hata ingawa tuliongozwa na kudhibitiwa na mabeberu kwa maslahi ya kikoloni katika miaka iliyopita hivi sasa sisi ni mataifa yaliyo na huru na hatima yetu iko mikononi mwetu, na jambo muhimu kuliko yote ni kuwa macho dhidi ya mifumo inayoendelea kuwekwa na watu wa nje, wenye nia ya kuidhibiti hatima hiyo”.
Katika hotuba hiyo Kenyatta ameipongeza AU, kwa kumuunga mkono akisema “Nikiwa kama Rais wa Kenya, ninastahili kujivuna kwa kuwa naweza kuutegemea Umoja wa Afrika kwa kunisikiliza na kunisaidia wakati wa matatizo na pia naamini Afrika ipo pamoja nami”.
Rais Kenyatta ambaye anakabiliwa na tuhuma za kufanya jinai dhidi ya binadamu katika mahakama hiyo na amekishutumu chombo hicho kwa kufanya kazi kwa mujibu wa matakwa na maamuzi ya nchi za Ulaya na Marekani dhidi ya nchi zinazojitawala na mataifa ya Afrika.
Kiongozi huyo kwa kuonesha kwamba hatarajii wala hana mpango wa kwenda kujibu mashtaka yake Hague kama aliovyokuwa ameahidi hapo mwanzo alisema hayuko taari kujisalimisha katika mahakama hiyo.
Nyundo zaidi ya kuonesha kwamba kiongozi huyo hatakwenda kujibu mashtaka hayo ilipigiliwa na viongozi wa Afrika waliokutana Addis Ababa ambao kwa kauli moja waliitaka Mahakama ya Kimataifa ya Jinai kuahirisha kesi ya Rais Kenyatta na Makamu wake William Ruto.
Uamuzi wa mkutano huo ulimpa kichwa zaidi kwa kulitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutekeleza kifungu nambari 16 cha mkataba wa Roma ambacho kinaruhusu chombo hicho kuahirisha kesi, uchunguzi au kukamatwa kwa mtuhumiwa kwa kipindi cha mwaka mmoja ambao unaweza kuongezwa baada ya kumalizika.
Sababu ya viongozi hao kufikia katika makubalino hayo inatokana na ukweli kwamba viongozi walioko madarakani hawapaswi kuhudhuria mbele ya mahakama ya ICC.
Viongozi hao wa Afrika wanalalamikia ICC kwa kusema kuwa wamekuwa wakilenga bara la Afrika katika kesi zake.
Hayo yanajiri wakati ambao kesi ya Rais Kenyatta inatarajiwa kuanza Novemba huku kesi dhidi ya Makamu wake William Ruto tayari inaendelea katika mahakama ya ICC, The Hague.
Pamoja na kwamba AU imeunga mkono azimio linalosema kuwa hakuna kiongozi yeyote wa nchi barani Afrika atakayefika katika mahakama ya kimataifa lakini suala la kujiondoa kutoka ICC lilikosa uungwaji mkono wa kutosha na viongozi wengi.
Katika mkutano huo wa AU, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ethiopia ambaye pia ni mwenyekiti wa baraza kuu la AU, Tedros Adhamom Ghebreyesus, amekiri kuwa AU haina mamlaka ya kumzuia kiongozi wa taifa lolote kushtakiwa mjini The Hague akiwamo Kenyatta, ila wanachopanga kufanya kumsaidia rais huyo ni kuwasiliana na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa kulitaka ili licheleweshwe kabla ya mashtaka yake kuanza rasmi Novemba 12.
Anaeleza kuwa Baraza hilo la Usalama ndilo lenye mamlaka ya kuamuru kesi hiyo kucheleweshwa kwa mwaka mmoja na endapo itaona kuna uwezekano wa kuongeza muda zaidi litafanya hivyo.
Ghebreyesus amesema kuwa kama ombi lao halitafanyiwa kazi, AU itaomba kesi dhidi ya Kenyatta iahirishwe na kama hilo halitafanyika basi viongozi wa Afrika wataamua kwa pamoja kumzuia rais Kenyatta kufikishwa katika mahakama hiyo mjini The Hague.
Waziri Mkuu wa Ethiopia Hailemariam Desalegn, amesema kuwa katika maamuzi yao wameamua Kenyatta na Rais wa Sudan Omar al-Bashir ambaye pia anatakiwa na ICC kujibu makosa yake ya uhalifu wa kivita naye hatahudhulia katika mahakama hiyo wakati huu ambao bado yuko madarakani.
Baada ya kumalizika kwa mkutano huo wa AU, mara moja makundi ya kutetea haki za binaadamu, kutoka Kenya na maeneo mengine yalipingwa vikali.
Kwa upande wa Kenya Naibu mkurugenzi mkuu wa Tume ya Kutetea Haki za Binadamu nchini humo (KHRC) Davis Malombe amezungumzia wito wa AU kutaka kesi hiyo icheleweshwe.
Malombe anasema “Hili ni jaribio jingine la kuvuruga na kuchelewesha haki kwa waathiriwa wa Kenya na unasaliti madai ya ahadi ya AU ya kupambana na ukwepaji sheria”.
Rais Kenyatta pamoja na naibu wake William Ruto, wanakabiliwa na mashitaka ya uhalifu wa kivita kutokana na vurugu zilizofanyika mwaka 2007 na zaidi ya watu 1,000 waliuawa na wengine wengi kuachwa bila makazi.

0 comments:

 

Sample text

Sample Text

PATA HABARI NA BURUDANI MBALI MBALI POPOTE ULIPO!

Sample Text