Operesheni ya
kuwaondoa M23 yakamilika
KINSHASA,
DRC
MAOFISA wa
serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo(DRC), wametangaza kuwa jeshi la
nchi hiyo limedhibiti ngome ya mwisho ya waasi wanaoungwa mkono na Rwanda (M23)
mashariki mwa nchi hiyo, hatua inayotia matumani ya kumalizika uasi wa miezi 18
wa kundi hilo.
Msemaji wa serikali
ya DRC Lambert Mende amewaeleza wanahabari kuwa mafanikio hayo ya jeshi la
serikali kwa sasa yatakuwa yanatoa nafasi ya kuendelea kwa mazungumzo ya amani
kati ya kundi hilo na wajumbe wa serikali.
Ripoti
zinasema kuwa, waasi wa M 23 waliokuwa wanapiga kambi katika ngome yao ya
kijeshi ya Bunagana wanaelezwa kutorokea kusikojulikana huku kiongozi wa kundi
hilo Betrand Bissimwa akiripotiwa kukimbilia nchini Uganda nchi ambayo imekuwa
ikihusishwa na kuwasaidia waasi hao.
Serikali ya
Uganda imethibitisha kuwa Bissimwa yuko nchini humo baada ya kuitwa na
msuluhishi Mkuu wa mazungumzo ya amani kati yao na serikali ya DRC Crispus
Kiyonga.
Mwakilishi
wa serikali ya Kinsasha katika mazungumzo hayo ya amani Francois Muamba,
amedokeza kuwa ikiwa kundi la M 23 litakubali mapendekezo waliyotoa basi kuna
matumaini kuwa suluhu itapatikana mapema.
Rais Joseph
Kabila amesema kuwa bado kuna nafasi ya upatikanaji wa suluhu kupitia
mazungumzo ya kisiasa na diplomasia na waasi hao na hivyo wanastahili kuweka
silaha chini au wataendelea kushambuliwa kijeshi.
Mjumbe
maalum wa Umoja wa Mataifa (MONUSCO) katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo
Martin Kobler mapema wiki hii alilieleza Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa
kuwa kundi la waasi la M 23 sio tishio tena kijeshi Mashariki mwa nchi hiyo.
Kobler
alieleza kuwa waasi wa M 23 wametoroka katika kambi zao za kijeshi na sasa
wanajificha karibu na mpaka wa Rwanda baada ya kuelemewa na wanajeshi wa DRC wanaosaidiwa
na wale wa Umoja wa Mataifa.
Mapigano
kati ya waasi na majeshi ya serikali yalianza wiki iliyopita baada ya
mazungumzo ya amani kuvunjika jijini Kampala Uganda na kufikia siku ya Jumatatu
hali iliyolifanya jeshi la serikali kupambana nao na kufanikiwa kuchukua miji
ya Rutshuru, Kiwanja na Rumangambo yote ambayo hapo awali ilikuwa inadhibitiwa
na waasi hao kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Kuondolewa kwa
waasi hao kwa mujibu wa mwakilishi wa Umoja wa Mataifa nchini DRC ni ishara
tosha kuwa waasi hao wamedhoofishwa kijeshi na huenda huu ndio ukawa mwisho
wao.
Hata hivyo,
waasi hao wa M 23 wanasema kuwa wamejiondoa katika ngome zao kwa muda tu ili
kuuonesha ulimwengu kuwa wao hawataki vita kwa mujibu wa rais wa kundi hilo
Betrand Bissimwa.
0 comments:
Post a Comment