Sakata la
udukuzi, Marekani yaigeuka Ulaya
NEW YORK, Marekani
WAKUU wa
ujasusi nchini hapa wamewageuzia kibao washirika wao wa Ulaya katika mgogoro
unaohusu udukuzi wa mawasiliano ya simu, wakisema mashirika ya Ulaya ndiyo
yaliyokusanya taarifa na kuwapatia wadukuzi wa Marekani.
Hayo yamebainishwa
na Mkuu wa Ujasusi (NSA), Keith Alexander na Mkurugenzi wa usalama wa taifa
James Clapper wakati wakijibu maswali ya wabunge kuhusu mpango wa udukuzi wa
Marekani.
Wakuu hao wa
mashirika ya ujasusi ya Marekani waliyakanusha madai hayo kuwa ni ya uongo, kuhusu
mashirika yao kunasa mawasiliano ya mamilioni ya simu, na kusema magazeti ya
Ulaya yaliyochapisha madai hayo, hayakuelewa data walizokuwa wanazitumia kutoa
madai hayo.
Maelezo hayo
yamekuja wakati ofisa wa juu wa Marekani akisema Rais Barack Obama alikuwa
akitafakari kuwapiga marufuku majasusi wa Marekani kunasa mawasiliano ya simu
za viongozi wa mataifa washirika, kufuatia hasira za Ujerumani juu ya madai
kwamba mawasiliano ya Kansela Angela Merkel yalidukuliwa.
Mkuu wa NSA,
Jenerali Keith Alexander, na mkuruguenzi wa usalama wa taifa, James Clapper,
walitoa ushahidi mbele ya bunge la Marekani na kusema kwamba msingi wa ripoti
hizo ulikuwa kutolewa taarifa zilizokabidhiwa kwa magazeti ya Ulaya na Snowden.
“Madai ya
waandishi wa habari wa gazeti la Le Monde la Ufaransa, El Mundo la Uhispania na
L'Espresso la Italia kwamba NSA ilikusanya mamilioni ya taarifa za mawasiliano
ya simu hazina ukweli wowote. Kwa kuweka mambo wazi kabisa, hizo siyo taarifa
tulizozikusanya kuhusu raia wa Ulaya. Ni taarifa ambazo sisi pamoja na
washirika wetu wa NATO tulizikusanya katika kuhakikisha usalama wa mataifa yetu
na kusaidia operesheni zetu za kijeshi," alisema Jenerali.
Hayo yameibuka
saa chache kabla ya jarida la Wall Street kulipoti kwamba uchunguzi wa
kielektroniki ulifanywa na mashirika ya kijasusi ya Ufaransa na Uhispania nje
ya mipaka ya mataifa yao, na wakati mwingine katika uwanja wa vita na kutoa
taarifa zao kwa NSA.
Lilisema kuwa
iwapo madai hayo yatakuwa kweli, yanaweza kuzifedhehesha serikali za mataifa ya
Ulaya, ambazo zimeipinga kwa nguvu Marekani kwa madai ya kuwafanyia ujasusi
raia wake.
Mwenyekiti
wa Kamati ya Ujasusi ya bunge la Marekani, Dianne Feinstein, aliunga mkono utetezi
wa wakuu hao wa ujasusi na kusema kuwa Marekani haikuzichunguza Ufaransa na
Ujerumani, bali nchi hizo ndizo zilikuwa zinakusanya taarifa hizo, na kwamba
Marekani ilikuwa inakusanya taarifa katika maeneo ya kivita ya NATO kama vile
Afghanistan.
Wakati huo
huo, maafisa wa ujasusi wa Ujerumani wanatarajiwa kukutana na wawakilishi wa
mashirika ya ujasusi ya Marekani katika lkulu ya White House, kujadili madai ya
ujasusi wa Marekani katika ujumbe utakao kuwa umewahusisha mshauri wa sera ya
kigeni wa Kansela Merkel na mratibu wa idara ya ujasusi wa nchi hiyo.
Kwa upande
wa Marekani, ujumbe wake unaowajumuisha mshauri mkuu wa usalama wa Rais Obama,
Suzane Rice, mkurugenzi wa usalama wa taifa James Clapper na msaidizi wa rais
wa usalama wa ndani na mapambano dhidi ya ugaidi, Lisa Monaco.
0 comments:
Post a Comment