Sudan: Juba iheshimu maamuzi ya AU
KHARTHOUM, Sudan
SERIKALI ya nchini hapa imemtaka jirani yake
Sudan Kusini iheshimu na kufungamana na maazimio na maamuzi yaliyopitishwa na
Umoja wa Afrika(AU).
Al-Khair Al-Fahim, Mwenyekiti wa Kamati ya
Pamoja ya Usimamizi na Uongozi wa eneo la Abyei amesema kuwa, Sudan Kusini
inapaswa kuheshimu maamuzi ya Umoja wa Afrika na isijichukulie maamuzi ya
upande mmoja kuhusiana na kura ya maoni ya kuainisha hatima ya eneo la Abyei.
Hivi karibuni Baraza la Amani na Usalama la
Umoja wa Afrika liliitaka Sudan Kusini kutojichukulia maamuzi ya upande mmoja
kuhusiana na kura ya maoni ya kuainisha hatima ya jimbo la Abyei.
Taarifa ya Baraza la Amani na Usalama la AU
iliitaka Juba kushirikiana kikamilifu na Khartoum kuhusiana na suala hilo.
Sudan inaishutumu Sudan Kusini kwa kuitisha kura
ya maoni kuhusu mustakbali wa eneo hilo mnamo Oktoba mwaka huu bila ya
kuishirikisha Khartoum.
Eneo la Abyei linalozozaniwa na Sudan na Sudan
Kusini ni jimbo lenye utajiri mkubwa wa mafuta ambalo liko katika mpaka wa nchi
mbili.

0 comments:
Post a Comment