Sifa za asiyeruhusiwa kufunga na anayeruhusiwa
Shabani Matutu
LEO ikiwa ni funga ya 25 katika mwezi huu wa Ramadhani, tunazungumzia Waislamu wanaopaswa na wasiopaswa kufunga.
Kuna mambo yanayomharibia swaumu yule aliyeruhusiwa kufunga kama hatafuatilia masharti aliyowekewa, kwa hiyo ni vema kujiepusha na mambo hayo.
Waislamu wanaoruhusiwa kufunga
Moja ya sharti la mfungaji ni umri, kwa sababu mfungaji anayekubalika kwa mujibu wa sheria ni kijana aliyebalehe (aliyefikisha umri wa utu uzima).
Ingawa wapo watoto wadogo wanaofunga si vibaya, ila si wajibu wao kufunga, hata kama akiwa na akili na uwezo wa kupambanua mambo. Ila kama atakuwa anahitaji kwa ridhaa yake asikatazwe kufunga.
Inawapasa wazazi wawazoeze watoto wao kufunga ili wawe tayari kutimiza wajibu wao pindi wafikiapo umri wa utu uzima wa kufunga.
Iwapo mtoto yeyote atayekuwa hajafunga katika mwezi huu kwa sababu tu, hajabalehe na hali ya kubalehe ikimtokea wakati Ramadhani imebakia siku mbili mwezi uishe, anapaswa kuendelea kufunga.
Kubalehe huko pia kunategemea muda, kama mtoto atabalehe kabla ya adhana ya alfajiri, ni lazima aanze kufunga siku hiyo, na kama atakuwa amebalehe mchana wa mwezi wa Ramadhani akiwa amefunga anaruhusiwa kula na atalipwa kutokana na swaumu yake hiyo.
Pia kundi jingine lililohalalishiwa kufunga ni watu walio na akili timamu na kwa wale walio na ugonjwa wa akili hawaruhusiwi kabisa kufunga au kuwalazimisha kufunga.
Mtu anayetakiwa kufunga ni yule aliye na afya njema, asiye na ugonjwa utakaomdhuru pindi awapo katika mfungo.
Katika kitabu cha Qur’an, Mwenyezi Mungu anasema: “Kwa atakayekuwa mgonjwa kwa maradhi yale ambayo akifunga swaumu itamdhuru au anahofia atazidiwa kwa njia zozote zile, haruhusiwi kufunga, kwani akilazimisha na akadhurika, swaumu yake haitakubalika na atatakiwa kuilipa baada ya mwezi kuisha.”
Pia mfungaji anatakiwa kuwa ndani ya mji wake ‘Al-iqaa-ma’ na asiwe nje au safarini, ambako patamsababishia kumpunguzia sala zake za kuswali.
Kwa mfano, mfungaji afike mahali ambako anahitaji kukaa zaidi ya siku 10 au zaidi, basi kwa sheria mtu huyo anajulikana kama ‘Muqeema’, huyo itamlazimu afunge.
Katika funga hili, Mwenyezi Mungu anasema: “Atakayekuwa katika mji si mgonjwa na wala hayupo safarini katika mwezi wa Ramadhani afunge. Na kwa yule ambaye anakuwa mgonjwa katika mwezi mzima au baadhi ya siku au aliye safarini, basi wote hao wanatakiwa walipe siku hizo watazokuwa hawajazifunga.”
Kwa sababu Mwenyezi Mungu ametutakia yaliyo mepesi na si mazito, ndiyo sababu anaamua kuwaruhusu wagonjwa na wale walio safarini kuacha kufunga na kulipa baadaye.
Kusafiri katika mwezi huu haikatazwi, hasa kwa safari za kikazi, lakini isiwe safari ya kuikimbia swaumu. Kwa kufanya hivyo muumini huyo hatapata msamaha na atatakiwa kufunga saumu hiyo.
Katika kuonyesha kuwa kufunga ni zawadi kubwa katika umma huu wa Mtume Mohammad (S.A.W), kuna hadithi ya Mtume inasema: “Mwenyezi Mungu amenituza mimi na umma zawadi ambayo hakumtuza mtu yeyote katika umma wowote uliotangua, ni heshima kutoka kwa Mola juu yetu.”
Waumini waliokuwa naye wakamuuliza ni zawadi ipi hiyo? Akajibu kuwa ni, kufuturu katika safari na kupunguziwa swala na asiyefuata hayo atakuwa amerejesha tuzo hiyo kwa Mola.
Mwanamke asiwe katika hedhi na nifasi (siku zake) kwa sababu haitasihi swaumu yake, hata kama hedhi itamjia kwa muda kidogo kabla ya kuingia magharibi (wakati wa kufuturu), saumu ya siku hiyo lazima ailipe.
Mtu mwingine anayestahili kufunga na kukubaliwa swala zake ni Muislamu, lakini kwa yule asiyekuwa Muislamu akifunga na kufuata ibada zote, funga yake haitakubaliwa.
Kwa nini Quran inasema kuwa wasio Waislamu hawatakubaliwa swaumu zao? Hii ni kwa sababu Waislamu kabla ya kuswali ni lazima kwanza watawadhe au watayamamu, kitendo ambacho kwa mtu asiye Muislamu hakifanyi.
Kwa mwenye kufunga, jambo jingine analohitaji kufanya ni kuweka nia kwa makusudio ya kufunga na kujizuia na kila kinachoharibu swaumu yake.
Kila muumini afungapo ni lazima aweke nia kwanza usiku wa kuamkia siku inayofuata, ila ni vizuri zaidi iwapo mwenye kufunga akitia nia ya mwezi mzima katika siku moja kabla ya Ramadhani.
Wakati wa kuweka nia ya swaumu, ni kutoka mwanzo wa usiku hadi mwanzo wa asubuhi (alfajiri).
Kwa mfungaji yeyote anayefunga kwa nia ya kujionyesha kwa watu wengine au kwa kumfurahisha mtu mwingine, basi ajue swaumu yake haitakubaliki kwa Mwenyezi Mungu.
Waislamu wasioruhusiwa kufunga
Vikongwe ambao si wagonjwa, wasifunge ila watoe fidia ya robo tatu ya kilo, kwa kila siku kwa wale wenye uwezo na kwa wale wasio na uwezo, si lazima bali ni bora.
Na kwa wale wagonjwa wanaoshindwa kujizuia na kiu, wanaruhusiwa kunywa maji, lakini isiwe kila wakati na wanatakiwa kulipa fidia hiyo kwa aliye na uwezo na asiyekuwa na uwezo halazimishwi, kama baadaye akijisikia vizuri anatakiwa alipe swaumu hizo.
Mwanamke mwenye mimba naye haruhusiwi kufunga ila atoe fidia kwa kila siku na baada ya kuzaa atafidia.
Mwanamke anayenyonyesha, naye ameruhusiwa kutofunga, lakini amalizapo kunyonyesha ahakikishe anazilipa swaumu hizo alizoziacha, ikiwa ni pamoja na kwa wale wenye uwezo wa kutoa fidia kila siku.
Mwisho.
Hivi ndivyo Sikukuu ya Idd inavyotakiwa kusherehekewa
Shabani Matutu
IDD EL FITR ni Sikukuu ya Kiislamu inayosherehekewa baada ya kumalizika kwa mfungo wa mwezi Mtukufu wa Ramadhani kumalizika.
Siku hii Waislamu huitumia katika kufurahi na kumshukuru Mwenyezi Mungu sambamba na kuomba wakubaliwe funga zao kwa kuwafutia madhambi yao na hatimaye kuwafikisha kwenye heri.
Sikukuu ya Idd huhitimishwa kwa kuswaliwa swala ya Idd el Fitr wakati wa asubuhi sambamba na kumtukuza Allah (S.W) kwa takbira (Allahu Akbar).
Swala ya Idd el Fitr inaswaliwa kwa rakaa mbili ikifuatiwa na khutba mbili kama zile zilizosomwa kabla ya swala ya Ijumaa. Swala hii ina takbira 12.
Takbira saba hutolewa katika rakaa ya kwanza kabla ya kusoma Suratul Faatiha na takbira tano hutolewa katika rakaa ya pili kabla ya kusoma Suratul Faatiha.
Mahali panapofaa kuswaliwa swala ya Idd panatakiwa pawe pakubwa, ingawa kuswali msikitini si dhambi ila ni bora sehemu kubwa iliyo wazi, patakaposaidia kukusanyika Waislamu wengi zaidi kutoka sehemu tofauti.
Katika hadithi ya Anas (Radhi yallahu Anhu-R.A) anaeleza kuwa Mtume Muhammad (SAW) alikuwa haswali Idd el Fitri hadi ahakikishe amekula japo tende katika idadi ya witri yaani namba zisizogawika kwa mbili na yenyewe.
Hadithi ya Burayda (R.A) inasema kwamba kipenzi cha Mwenyezi Mungu Mtume Muhammad (SAW) alikuwa hatoki kwenda kuswali swala ya Idd el Fitr hadi awe amefuturu kitu.
Ni sunna pia kuleta takbira mara kwa mara kuanzia pale mwezi unapoandama hadi baada ya swala ya Idd el Fitr.
Mambo yanayotakiwa kufanywa Siku ya Idd
Ni jambo la heri kwa Mwislamu Siku ya Idd kuoga, kuvalia nguo nzuri ikiwa ni pamoja na kupaka uturi (manukato) mazuri kwa wanaume.
Pia ni siku inayofaa kwa Waislamu kupika vyakula vizuri na vinywaji visivyokuwa na kilevi, na kwale wafugaji na walio na uwezo ni sunna kumchinja mnyama aliye bora zaidi kuliko wengine katika mifugo yake.
Hadithi ya Hassan Asibbit (R.A) inasema kwamba Mtume (SAW) ametuamrisha katika Idd mbili kuvaa vizuri zaidi kadri tuwezavyo, tupake uturi bora zaidi kuliko wote tulionao na tuchinje wanyama wenye thamani zaidi kuliko wote tulionao.
Ni sunna pia kuwakaribisha ndugu, marafiki, majirani, maskini, yatima na wengine wasiojiweza.
Pia ni sunnah kuwatembelea wagonjwa, maskini na watu wasiojiweza ikiwa ni pamoja na kupeana zawadi.
Mwisho wa Ramadhan isiwe mwanzo wa maasi, ila iwe kipimo cha kuendeleza kufanya mema kwa Waislamu na kuachana na maovu.
Zakatul Fitr
Hii ni zakat inayotolewa baada ya Waislamu - wake kwa wanaume - kumaliza funga yao ya Ramadhan na hutolewa kabla ya swala ya Idd el Fitr.
Kwa wale wasio na uwezo watalipiwa na mawalii wao kwa mfano mume atawatolea wazazi wake kama hawana uwezo wa kujilipia na baba atalazimika kuwalipia Zakatul Fitr wale wote walio chini yake iwapo kama anauwezo.
Umuhimu wa Zakatul Fitr ni faradhi iliyoambatanishwa na faradhi za mwezi wa Ramadhani. Mtume amsema ili kuiwezesha swaumu yako ipokelewe vizuri na Allah ni lazima kwa mwenye uwezo aitolee Zakatul Fitr.
Anayestahili kutoa Zakatul Fitr ni mwenye chakula cha kuwatosha watu wake anaoishi nao na kuwa na ziada ya kutosha usiku na ile ziada nyingine ndiye anayetakiwa kutoa Zakatul Fitr.
Kiwango cha Zakatul Fitr
Kwa mujibu wa hadithi iliyotolewa na Ibn Umar (R.A) anasema kwamba kiwango kinachotakiwa kutolewa kwa kila mtu ni ‘sai’ moja ya chakula kinachopendwa sana katika sehemu husika.
Kwa mfano, pwani wakati wa sikukuu hupendelea kula wali au pilau na sai inayozungumziwa hapa kwa nyakati hizi ni sawa na kilo mbili na nusu za bidhaa husika.
Kutokana na hali halisi ya kimaisha ni vyema zaidi mtoaji atoe fedha kuliko bidhaa ili kumsaidia mhusika unayemtolea kununua bidhaa ambayo anaipenda mwenyewe.
Muda unaofaa kutolewa Zakatul Fitri umebainishwa kwenye hadithi iliyotolewa na Ibn Umar (R.A). Inasema kwamba Mtume (SAW) aliwaeleza watu kuwa watoe Zakatul Fitr kabla ya kuswali Idd el Fitr.
Kulipa Zakatul Fitri mapema kabla ya kuswali Idd au mapema zaidi ya hapo kutamwezesha unayempatia kufurahia Idd na Waislamu wengine.
Iwapo itatokea sababu ya msingi kama vile kusahau hadi Idd ikaswaliwa, huna budi kuitoa baada ya swala na iwapo ataacha kutoa kwa makusudi au kwa uzembe basi ajue kutoa kwake huko hakutamnufaisha kwa chochote.
Watu wanaostahili kupewa Zakatul Fitr
Ni chakula cha maskini na wale wasiojiweza kujipatia chakula pamoja na wale walio chini ya uangalizi wao kwa Siku ya Idd na usiku wake, ili na wao wajisikie na kufurahia Idd na Waislamu wenzao wenye uwezo.
Iwapo Zakatul Fitr atapewa mtu aliye na uwezo na kuachwa asiye nao, wote watakaokuwa wametoa na kupokea Zakatul Fitr hiyo watakuwa wameidhulumu haki ya anayestahili kupewa. Hivyo watakuwa wamekwenda kinyume na matakwa ya Mwenyezi Mungu.
Sikukuu ya Idd itasherehekewa kufuatana na mwandamo wa mwezi na iwapo mwezi hautaonekana, basi Waislamu wanatakiwa waendelee kufunga hadi kukamilisha siku 30 kamili ndipo watakaporuhusiwa kufungua.
Sikukuu ya Idd haistahili kusherehekewa kwa kupiga muziki, ngoma, kunywa mapombe na kufanya mambo yaliyokatazwa na Mwenyezi Mungu, kwani utakiwa umemuasi.
Siku ya Idd si siku ya kufanya maasi, kwani Mtume (SAW) anasema: “Kumuasi Mwenyezi Mungu Siku ya Idd ni sawa na kufanya uasi siku ya kiyama”.
*Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa barua pepe; kimyamatutu@yahoo.com.
Mwisho………
Ishara ya kufunga na kufungua mwezi wa Ramadhani
Shabani Matutu
IDD Mubarak ndugu zangu Waislamu mliosherehekea Idd el Fitr jana na mnaosherehekea siku hiyo leo nyote mliokuwa katika nia ile ile moja ya kutafuta amali za Mwenyezi Mungu.
Pamoja na kwamba leo ndiyo siku inayotambulikana kiserikali, lakini wapo baadhi ya Waislamu wa madhehebu mengine waliofungua tangu jana.
Katika makala ya leo nitazungumzia juu ya ishara zinazotuwezesha kujua siku ya kufunga au siku ya mwisho tunayotakiwa kula Idd.
Hapa sitapenda kuzungumzia kwa wale waliofungua jana wana makosa au wanaofungua leo wana makosa, ila nia ni kueleza alama zinazotuongoza kujua siku hizo.
Kumekuwa na maswali mengi inapofika Ramadhani ya 29, wengi wakijiuliza kama siku ya pili yake itakuwa Sikukuu ya Idd el Fitri.
Maswali hayo pia hupatikana katika mwanzo wa kufunga mwezi wa Ramadhani lakini jibu ni rahisi, kwani tumelezwa kwamba tunatakiwa kufunga kwa kuuona mwezi na kufungua kwa kuuona mwezi.
Katika kuuona mwezi unatakiwa kuuona mwenye kwa kuushuhudia, ndipo unaporuhusiwa kufunga au kufungua kama utakuwa umefunga.
Unapouona mwezi uwe mdogo au mkubwa kusiwe na mabishano ya kutaka kuonyesha kuwa ulikuwa wa jana au wa juzi tuanatakiwa kuepusha mabishano ya aina hiyo.
Njia nyingine ni ya kupewa taarifa na ndugu yako Mwislamu muadilifu atakayekuthibitishia kuwa ameuona.
Iwapo Waislamu watakuwa wamefunga siku 29 na mwezi ukawa haujaonekana basi wanaambiwa waendelee kufunga siku moja zaidi ili wakamilishe siku 30.
Idd el Fitr ni sikukuu ya Kiislamu inayosherehekewa baada ya kumalizika kwa mfungo wa mwezi wa Ramadhani.
Siku hii Waislamu huitumia katika kufurahi na kumshukuru Mwenyezi Mungu sambamba na kuomba wakubaliwe funga zao kwa kuwafutia madhambi yao na hatimaye kuwafikisha kwenye heri.
Sikukuu ya Idd huhitimishwa kwa kuswaliwa swala ya Idd asubuhi sambamba na kumtukuza Allah (SW) kwa takbira na kuswaliwa rakaa mbili ikifuatiwa na khutba mbili kama zile zinazosomwa kabla ya swala ya Ijumaa. Swala hii ina takbira 12.
Takbira saba hutolewa katika rakaa ya kwanza kabla ya kusoma suratul Faatiha na takbira tano hutolewa katika rakaa ya pili nayo kabla ya kusoma kusoma suratul Faatiha.
Mahali panapofaa kuswaliwa siku ya Idd ni mahali pakubwa ingawa kuswali msikitini si dhambi ila ni bora sehemu kubwa iliyo wazi ambapo patasaidia kukusanyika waislamu wengi zaidi kutoka sehemu tofauti.
Katika hadithi ya Anas (RA) anaeleza kuwa Mtume (SAW) alikuwa haswali Idd el Fitri mpaka ahakikishe amefuturu japo tende katika idadi ya witri yaani namba zisizogawika kwa mbili na yenyewe.
Ni sunna pia kuleta takbira mara kwa mara kuanzia pale mwezi unapoandama mpaka baada ya swala ya Idd el Fitr
Mambo yanayotakiwa kufanywa siku ya Idd
Ni jambo la heri kwa Mwislamu siku ya Idd kuoga, kuvalia nguo nzuri ikiwa ni pamoja na kupaka uturi (manukato) mazuri kwa wanaume.
Pia ni siku ambayo inafaa kwa Waislamu kupika vyakula vizuri na vinywaji visivyokuwa na vilevi na kwale wafugaji na walio na uwezo ni sunna kumchinja mnyama aliyebora zaidi kuliko wengine katika mifugo yake.
Hadithi ya Hassan Asibbit (RA) inasema kwamba Mtume (SAW) ametuamrisha katika Idd mbili kuvaa vizuri zaidi kadri tuwezavyo, tupake uturi bora zaidi kuliko wote tulionao na tuchinje wanyama wenye thamani zaidi kuliko wote tulionao.
Pia ni sunna kuwatembelea wagonjwa, majirani, yatima, maskini, na watu wasiojiweza ikiwa ni pamoja na kupeana zawadi.
Mwisho wa Ramadhani isiwe mwanzo wa maasi ila iwe kipimo cha kuendeleza kufanya mema kwa waislamu na kuachana na maovu.
Tunatakiwa zakatul Fitri
Hii ni zakat inayotolewa baada ya Waislamu wanawake na wanaume kumaliza funga yao ya Ramadhani na hutolewa kabla ya swala ya Idd el Fitr.
Kwa wale wasio na uwezo watalipiwa na mawalii wao kwa mfano mume atawatolea wazazi wake kama hawana uwezo wa kujilipia na baba atalazimika kuwalipia zakatul Fitri wale wote walio chini yake iwapo kama anauwezo.
Umuhimu wa Zakatul Fitr ni faradhi iliyoambatanishwa na faradhi za mwezi wa Ramadhani, Mtume (SAW) ili kuiwezesha swaumu yako ipokelewe vizuri na Allah ni lazima kwa mwenye uwezo uitolee Zakatul Fitr.
Anayestahili kutoa Zakatul Fitri ni mwenye chakula cha kuwatosha watu wake anaoishi nao na kuwa na ziada ya kutosha usiku na ile ziada nyingine ndiyo anatakiwa kutoa zakatul Fitri.
Kiwango cha Zakatul Fitri
Kwa mujibu wa hadithi iliyotolewa na Ibn Umar (RA) anasema kwamba kiwango kinachotakiwa kutolewa Zakatul Fitr kwa kila mtu ni sai moja ya chakula (kwa sasa ni sawa na kilo mbili na nusu ya bidhaa husika) hasa kinachopendwa sana katika sehemu husika.
Kutokana na hali halisi ya kimaisha ni vyema zaidi mtoaji atoe fedha kuliko bidhaa ili kumsaidia mhusika unayemtolea kununua bidhaa ambayo anaipenda mwenyewe.
Muda unafaa kutolewa Zakatul Fitr umebainishwa kwenye hadithi iliyotolewa na Ibn Umar (RA) inasema kwamba Mtume (SAW) aliwaeleza watu kuwa watoe Zakatul Fitri kabla ya kuswali el Idd Fitr.
Kulipa Zakatul Fitri mapema kabla ya kuswali Idd au mapema zaidi ya hapo, kutamuwezesha unayempatia kufurahia Idd na Waislamu wengine.
Iwapo itatokea sababu ya msingi kama vile kusahau mpaka Idd ikaswaliwa hana budi kuitoa baada ya swala na iwapo ataacha kutoa kwa makusudi au kwa uzembe basi ajue kutoa kwake huko hakutamnufaisha kwa chochote.
Watu wanaostahili kupewa Zakatul Fitr ni maskini na wasiojiweza kupata chakula pamoja na wale walio chini ya uangalizi na wale waliochini yake ili wajisikie kufurahia Idd na waislamu wenzao wenye uwezo.
Iwapo Zakatul Fitr atapewa mtu aliye na uwezo na kuachwa asiye nao wote ambao watakuwa wametoa na kupokea Zakatul Fitr hiyo watakuwa wameidhurumu haki ya anayestahili kupewa hivyo watakuwa wamekwenda kinyume na matwakwa ya Mwenyezi Mungu.
Sikukuu ya Idd haistahili kusherehekewa kwa kupiga miziki, ngoma, kunywa vilevi na kufanya mambo yaliyokatazwa na Mwenyezi Mungu kwani utakiwa umemuasi.
Siku ya Idd si siku ya kufanya maasi kwani Mtume (SAW) anasema kuwa “Kumuasi Mwenyezi Mungu siku ya Idd ni sawa na kufanya uasi siku ya kiyama”.
Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa barua pepe; kimyamatutu@yahoo.com.
Mwisho………….
Faida za kumi la mwisho mwezi wa Ramadhani
Shabani Matutu
ASALAM aleykum ndugu zangu wa imani katika Uislamu, ambao mmebarikiwa afya njema kwa kuendelea kufunga kumi hili la mwisho la mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Hivi sasa Waislamu wako katika siku za mwisho za kukamilisha funga ya mwezi mtukufu wa Ramadhani kwa ajili ya toba na pia kumrejea Mwenyezi Mungu kwa kuacha mabaya na kutenda mema.
Mtume wetu Muhammad S.A.W anasema mwezi wa Ramadhani una makumi matatu, na kila moja linatoa neema zake kwa mfungaji.
Mtume SAW anasema kumi la kwanza ni kumi la rehema, linaloanzia chungu cha kwanza hadi cha kumi. Fungu hili humuangukia mfungaji yule aliyefunga kwa kufuata masharti ya kufunga, si kila mfungaji bora tu kafunga, ila ni yule aliyefunga kwa kufuata funga inavyotaka.
Mfungaji awe amehakikisha ameacha matendo yasiyompendeza Mwenyezi Mungu, mfano kuacha kusema maneno machafu, uongo, fitina, kusengenya, kuiba, kuua, kuzini, kunywa pombe na yote mengine yaliyokatazwa.
Iwapo mfungaji atakuwa anajiamini kuwa alikuwa ni mmoja kati ya watu waliokuwa wamefunga pasipo kutenda moja ya mambo yanayomchukiza Mwenyezi Mungu, ajue atakuwa ni mmoja wa watu waliopata rehema hiyo.
Kumi la pili ni kuanzia siku ya 11 ya kufunga hadi ya 20. Kumi hili ni la kutoa msamaha kwa wafungaji, waliofunga na swaumu zao zikawa zimekubalika, Mwenyezi Mungu anasema kila nafsi iliyo hai hukubaliwa msamaha na msamaha haukubaliwi kwa nafsi iliyokufa.
Hata Firauni alimuomba Mwenyezi Mungu amsamehe wakati alipokuwa anakatisha bahari ya Shamu akimfuta Mussa alipokuwa anaondoka na wana wa Israel akiwa anawaongoza kuwapeleka Kaanan.
Maji yalipokuwa yanamkaribia Firauni, alisema amemkubali Mungu wa Mussa kuwa alikuwa ni Mungu wa kweli, lakini Mwenyezi Mungu hakutaka kumsikiliza kwa kuwa alishaahidi kutosamehe roho zilizokwishafikia hali ya umauti.
Hakuna binadamu asiyekuwa na dhambi, hivyo ni wajibu wa kila muumini kutumia muda wake kumuomba msamaha Mwenyezi Mungu wakati akiwa hai, kwani Mungu hatoi msamaha kwa maiti.
Kumi la tatu ndilo kumi lililoanza siku ya 21 ya mwezi mtukufu wa Ramadhani. Kumi hili ndilo linasemwa lilikuwa ni kumi ambalo Mtume S.A.W alikuwa anahamia msikitini na jamaa zake kwa ajili ya ibada.
Kumi hili linasemwa na wasomi wa Kiislamu kuwa ndilo bora ambalo ndimo Mtume alishushiwa Wahayi (Ujumbe wa Quran) na malaika Jibril. Katika kumi hili ndimo kunakopatikana usiku wa Laila tul Kadir.
Waislamu wamehusiwa kusoma Quran katika usiku wa kumi hili la Laila tul Kadir kwa sababu Quran inasema Mungu hutoa ruhusa kwa malaika kuteremka kwenye nyumba ya muumini anayesoma Quraan, huku wakiongozwa na Jibril, na hukaa katika nyumba hiyo mpaka alfajiri.
Pia Mwenyezi Mungu anaendelea kusema katika Quran kwamba nyumba zinazosomwa Quran hutembelewa na malaika ikiwa ni pamoja na kusamehewa madhambi yao waumini wanaoishi ndani yake, na kwa wale wasiojua kusoma, hata kwa kusikiliza yatosha kupata thawabu hizo.
Iwapo Mtume wa Mungu asiye na shaka na pepo anakesha akiswali, sembuse muumini mwenye madhambi unashindwa kuswali swala hata moja?
Je, ni vipi utaijua hii ndiyo siku ya Laila tul Kadir? Quran inatueleza kuwa siku hiyo ni siku ya namba witiri katika siku 10 za mwisho (kumi la mwisho) za mwezi wa Ramadhani, ikimaanisha namba 21, 23, 25, 27 na 29.
Katika siku hizo utajuaje siku hiyo imekufikia? Vitabu vinasema alama ya kwanza ya kujua kuwa siku hiyo imekukuta, ni kuota waumini wakiwa wanaswali, pili ukisikia adhana, tatu ukiota watu wakiwa katika siku ya mwisho (Kiyama).
Ukiona ishara hizo, basi ujue ndani mwako kuna malaika, hivyo amka uswali na uombe shida zako zote utasaidiwa kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Mara nyingi unashauriwa kulala ukiwa na udhu katika siku hizi.
Siku hii inasemekana kuwa Mtume SAW alikuwa anafunga kibwebwe kiunoni na kuwaamsha watu wake na wakeze kukesha wakiswali kwa salama yao ya kutafuta pepo.
Hivi sasa imekuwa tofauti na nyakati za Mtume SAW, wao katika kumi la mwisho ndilo walikuwa na bidii katika kuswali na kukesha, lakini Waislamu wa sasa wamekuwa na bidii katika kumi la kwanza, lakini siku zinavyokwenda mbele, waumini huwa wachache sana misikitini.
Jamani naihusia nafsi yangu na nafsi za Waislamu kwa kumcha Mwenyezi Mungu, ili tufanikishe dhumuni la Ramadhani la kutuondolea takataka au uchafu ulioganda nafsini mwetu.
Ramadhani itumike kusafisha nafsi yetu, hasa kwa kutoa zaka. Muumini unapotoa zaka, angalia ni aina gani unayoitoa. Toa zaka ambayo itakuwa na msaada kwa waumini wengine.
Kwa mfano, unapotaka kumsaidia fundi ujenzi mpatie vifaa vya ujenzi, au mpiga picha mpatie kamera, kila mtu asaidiwe kitu kitakachomuwezesha kujisaidia kwa muda mrefu na si msaada wa muda mfupi.
Mtume anatuambia pia kwamba, tunaweza kusafisha nafsi zetu kwa kutoa sadaka, kusoma Quran au kusikiliza, kuswali swala za tasbihi au kukaa itikafu misikitini.
Swaumu zetu zimekuwa na matatizo ya hapa na pale. Kuna wakati futari inapatikana katika njia ambazo si za halali au kuna wakati umeteleza kidogo ukasema uongo, kwa kulitambua hilo, Quran inatuelekeza mambo ya kufanya ili kuzisafisha swaumu zetu.
Quran inasema tutoe zaka iitwayo Zakatul Fitr ili kusafisha makosa kama hayo ili kuifanya Swaumu ikubalike.
Ni vipi inatolewa hii Zaka tul Fitr? Zaka hii hutolewa baada ya mwezi kuonekana, siku moja kabla ya Sikukuu ya Idd el Fitr. Zaka hii hutolewa toka jioni hiyo mpaka asubuhi kabla ya jua kuonekana au kabla ya kusali swala ya Idd.
Quran inasema Mwenyezi Mungu ni msafi, hivyo basi, mtakapotoa, toeni vilivyo safi. Waislamu wanashauriwa iwapo wanatoa zaka kwa masikini, wawape miongoni mwa vitu wanavyovipenda na si vitu wasivyovipenda.
Pia Waislamu walio na uwezo wa mali wanaruhusiwa kutoa Zaka tul Fitr kwa ajili yao wenyewe na wazee wao, watoto na wake zao.
Zaka tul Fitr isitolewe baada ya jua kuchomoza, hiyo itakuwa ni sadaka ya kawaida, haitakuwa Zaka tul Fitr.
Mwisho.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
1 comments:
Good dispatch and this post helped me alot in my college assignement. Say thank you you as your information.
Post a Comment